Sunday 14 January 2024

MFUKO WA JIMBO WAWEKA ALAMA - MTATURU

...



MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amewaongoza wajumbe wa mfuko wa jimbo kukagua miradi iliyotengewa na kutekelezwa kwa fedha za mfuko huo kiasi cha Sh 67,498,970 kwa mwaka 2022/2023.

Ziara hiyo ameifanya baada ya kumaliza kikao cha kupokea na kujadili maombi ya fedha za mfuko huo.

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo Mbunge Mtaturu amesema Kamati ya mfuko wa Jimbo baada ya kutembelea miradi hiyo imeridhishwa na hatua ya utekelezaji.

"Kamati hii iligawa miradi katika Kata 13 na tumepata nafasi ya kuitembelea baadhi ya miradi hiyo na tumeridhika na hatua ya utekelezaji iliyofikiwa,na tukiendelea na kasi hii tutakuwa tumeunga mkono kwa kiasi kikubwa dhamira ya Rais wetu mpendwa Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo,tunafahamu Rais wetu halali kwa ajili ya watanzania,hivyo na sisi tulio chini yake tunawajibu wa kumuunga mkono kwenye jukumu hilo,".amesema.

Mtaturu ameainisha miradi waliyotembelea kuwa ni pamoja na ujenzi wa M Matundu ya vyoo katika shule ya Msingi Ulyampiti ambayo utekelezaji wake imetengewa Sh 2,000,000.

"Tumetembelea na kujionea ujenzi wa Zahanati Kijiji cha Ighuka iliyotengewa Sh 2,000,000 ambayo kwa sasa wamekamilisha ufungaji wa renta na Serikali Kuu imetenga Sh Milioni 50 kwa ajili ya umaliziaji ili huduma zianze kutolewa,Kamati pis imetembelea ujenzi wa vyumba viwili vya maabara ambapo walitengewa Sh Milioni 5,katika ujenzi huu tayari wameshajenga msingi na kufunga mkanda wa renta chini na sasa wanatarajia kuanza kunyanyua ukuta,"amebainisha.

Mbali na miradi hiyo amesema wametembelea pia ujenzi wa nyumba ya Mganga Zahanati ya Ujaire ambayo ilitengewa Sh Milioni 1.5 na wameshajenga boma na kufunga renta.

Aidha,wametembelea na kujionea ujenzi na ukarabati wa madarasa ya Shule ya Msingi Ujaire ambayo ilitengewa Sh Milioni 2 na kwa sasa ukarabati na ujenzi wa maboma ya madarasa umekamilika ambapo pia serikali kuu ilipeleka Sh Milioni 41 kumalizia madarasa mawili na ofisi.

Mtaturu amewapongeza wananchi wakiongozwa na viongozi kwa kujitolea kwenye miradi hiyo na kuishawishi serikali kupeleka fedha za umaliziaji.

"Ndugu zangu niwatie moyo na kuwahimiza kuwa tuendeleze juhudi hizi tulizozianza na jitihada tulizozionyesha katika kiradi hii tuziendeleze katika miradi mingine tunayoisimamia,"amesema.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Madiwani wa Kata za Ikungi na Lighwa wamempongeza Mbunge na Kamati yake kwa kuwatengea fedha za kusaidia miradi kwenye sekta ya elimu na afya ambayo sasa matunda yake yanaonekana kwa kuwa baadhi ya miradi imeanza kufanya kazi.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger