Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleiman Jafo amemvua
madaraka Meneja wa Mamlaka ya Maji Mji Mdogo wa Kisarawe mkoani Pwani,
Listen Materu kwa kile alichodai ameshindwa kusimamia majukumu yake
kikamilifu.
Pia, Jafo ameuagiza uongozi wa halmashauri hiyo kuondoa kero zinazolalamikiwa na wananchi hasa idara za ardhi, afya na elimu.
Akisikiliza
kero za wapigakura wake juzi, Jafo alisema uchunguzi alioufanya
ameubaini kwa miaka mitano iliyopita kuwa baadhi ya watendaji wa vitengo
na idara wa halmashauri hiyo walikuwa hawawajibiki kwa makusudi, lengo
lao lilikiwa ni kujenga chuki baina ya mbunge na wananchi jambo ambalo
limefikia kikomo.
“Kuna watu waligeuza wilaya hii kama shamba la
bibi, walikuwa wanatumia mali za umma kwa kufanya ubadhirifu sasa
wasiseme kuwa wamesalimika, kama wamehama au wamehamishwa tutawafuata
kokote walipo na watawajibishwa kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Naibu
waziri huyo alisema, kuwavua madaraka na kuwawajibisha watendaji wabovu
hakutaishia kwa watumishi waliopo wilayani hapa, bali hata waliofanya
ubadhirifu na kuhama au kuhamishiwa maeneo mengine.
Katika
kuboresha wilaya hiyo na kuharakisha maendeleo, Jafo alisema ni wajibu
wa halmashauri kuhakikisha inatenga maeneo ya ujenzi wa stendi,
machinjio na utekelezaji wake ufanyike haraka na kuwataka iwapo
watakabiliwa na changamoto za kukwamishwa mpango huo wasisite
kuwasiliana naye.
0 comments:
Post a Comment