Tuesday 30 July 2019

MFANYAKAZI WA WIZARA YA FEDHA AKUTWA AMEFARIKI DUNIA JUU YA MTI WA MWEMBE


Msemaji wa Wizara ya Fedha na Mipango Benny Mwaipaja, ameeleza kutokea kwa kifo cha mfanyakazi mwenzao, aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Fedha za Nje, Mhandisi Leopold Lwajabe, ambaye mwili wake umekutwa ukiwa umening'ínia juu ya mwembe Wilayani Mkuranga.

Mwaipaja akitoa taarifa hiyo amesema, mtumishi huyo kwa mara ya kwanza alitoweka Julai 16 na kupatikana, na baadaye alitakiwa kwenda kuripoti kituo cha polisi Mburahati kwa lengo la kueleza ni kipi kilimsibu.

''Ni kweli tukio limetokea alikuwa ni mtumishi wa Idara ya Fedha za Nje, Julai 25 aliaga ofisini kwamba anaenda polisi Mburahati na toka hapo hakuonekana tena, ndio leo tumepata taarifa tumefika eneo la tukio tumekuta mwili wake umening'ínia juu ya mwembe, sasa mwili wake unapelekwa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi kisha masuala mengine ya mazishi yafuate'' amesema Mwaipaja.

Kwa upande wake Mkuu wa Polisi Mkoa wa kipolisi Rufiji RPC Onesmo Liyanga, amethibitisha kutokea kwa kifo hicho, lakini bado wanaendelea kufuatilia ili kujua alikuwa na nafasi gani wizarani.

''Hatujapata data vizuri kama alikuwa na nafasi gani katika utumishi wake, kwa sababu hata kuutambua huo mwili imechukua muda, kwahiyo bado na ndugu ndio walikuwa wanakuja, kwahiyo naomba tupeane muda kwa kusaidiana na ndugu zake tutatoa taarifa na taarifa zote zitapatikana'' amesema RPC Liyanga.
Share:

KAMPUNI YA JATU PLC YAENDESHA MAFUNZO KWA VIJANA 100,YAWAASA KUACHA KUTEGEMEA KUAJIRIWA


KAMPUNI I ya Jenga Afya Tokomeza Umaskini (Jatu PLC), imeendesha mafunzo kwa vijana 100 lengo likiwa ni kutokomeza umaskini kupitia rasilimali watu.

Meneja mkuu wa Jatu, Mohamed Simbano akizungumza wakati wa mafunzo hayo alisema mkakati wa taasisi yao ni kusaidia kuondoa kutu vichwani mwa vijana kwa kuacha kutegemea kuajiriwa na badala yake waangalie fursa zilizopo na kuweza kujiajiri.

“ Tukiwa hapa kwenye mafunzo, una diploma, degree weka pembeni kwa sababu hazina maana sana kama huna uwezo wa kubuni wazo na kutengeneza pesa,” alisema Simbano na kuongeza

“Aliyejaribu na akashindwa, anafaida kubwa kuliko asiyejaribu, kufeli haina maana umeshindwa bali utatafuta namna nyingine ya kujaribu.” Alisema

Akimnukuu mwanafalsafa Joseph Chilton Pearce aliyeelezea thamani ya ubunifu aliyosema, ‘to live a creative life we must lose our fear of being wrong’ kwa tafsiri isiyo rasmi alimanisha kuishi maisha ya ubunifu kunahitaji kuondoa hofu ya kukosea.

Simbano alisema elimu ambayo wanawapatia vijana hao itawaondoa katika dhana ya kusaka ajira au kubweteka majumbani na badala yake watachukua hatua na kujiikingiza kwenye ujasiriamali wa kilimo na masoko.Alisema mafunzo hayo ni bure kwa kila kijana mwenye ndoto za kujikwamua kiuchumi,bila kujali elimu.

Alisema mara baada ya mafunzo hayo watatoa nafasi kwa vijana katika masoko kwa kuwaajiri na kuimarisha kitengo chao cha masoko, hadi kufikia mwaka 2022 kila anayetumia soko bidhaa za Jatu aweze kupata manufaa na kwamba chakula kinacholiwa kiwe suluhisho la masoko.

“Mafunzo haya ni endelevu, vijana 100 tutakaowapa ajira ni fursa pekee kwao kwa kuimarisha kitengo cha masoko cha Jatu, na kazi yao kubwa ni kuhakikisha kila mwanachama wa jatu aweze kutumia bidhaa.” Alisema

Alisema mafunzo hayo yanaenda sambamba na mpango mkakati na kufikia malengo, waliojiwekea ikiwemo kutokomezaz umaskini kupitia rasilimali watu, kilimo na viwanda, ikiwa ni pamoja na kuingia kwenye soko la hisa (DSE) mwezi Septemba.
Share:

TCRA KUHAKIKISHA HUDUMA BORA NA ZA UHAKIKA ZA MAWASILIANO KWENYE UJENZI MRADI WA UMEME MTO RUFIJI




Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jones Killimbe (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Mhandisi James M. Kilaba (wapili kushoto) na mmoja wa wajumbe wa bodi, wakiwa kwenye eneo la Mto Rufiji ambako kunajengwa bwawa la kufua umeme wa maji Megawati 2115.
******
NA K-VIS BLOG/Khalfan Said, Rufiji

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeagiza kuwepo kwa huduma bora za Mawasiliano katika eneo la Mradi wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme wa maji Mto Rufiji Mkoani Pwani.



Akizungumza wakati wa ziara ya Wajumbe wa Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA, pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati ya maudhui ya Mamlaka hiyoh kwenye eneo la Mradi huo Julai 28, 2019, ambapo ujenzi ukikamilika bwawa Hilo litaitwa bwawa la Nyerere, Mkuru Mkuu wa TCRA Mhandisi James M. Kilaba alisema, Mradi huo mkubwa ni mradi wa kimkakati na TCRA kama msimamizi wa sekta ya Mawasiliano hapa nchini inaamini hakuna uwekezaji unaotendeka bila ya uwepo wa mawasiliano, jamii na watu watakaokuwa wanatekeleza ujenzi wa mradi huo wanapaswa kuwa na mawasiliano ya uhakika wakati wote wakiendelea na kazi ya ujenzi.

Ujenzi wa Mradi huo wenye thamani ya Shilingi za Kitanzania Trilioni 6.5 fedha za Serikali, ulizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli juzi Ijumaa Julai 26, 2019 na utakamilika mwaka 2022 ambapo utakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme Megawati 2115.

Akieleza zaidi Mhandisi Kilaba alisema, Shirika la TTCL kama Shirika la Serikali pamoja na watoa huduma wengine ya mawasiliano wanaowajibu wa kuhakikisha mawasiliano yapo na TCRA wajibu wake ni kuhakikisha watoa huduma wanafanya yale wanayopaswa kufanywa.

“Hapa umesema zaidi ya wafanyakazi 6,000 watakuwa kwenye eneo hili, lakini pia hata watakaokuwa wanakuja kufanya utalii kwenye National Park ya Nyerere ni lazima wawe na mawasiliano na mawasiliano ya sasa ni Data, kwahiyo tunachoweza kuagiza hususan TTCL ni kuhakikisha wanaenda kwa kasi kubwa kuweka mawasiliano katika eneo hili na mawasiliano tunayotaka sisi kama wadhibiti ni 4G as Minimum.” Alifafanua Mhandisi Kilaba na kuongeza

“Kwa hiyo 4G siyo isubiri mpaka turbines (mitambo ya kufua umeme)zianze kuzunguka, la hasha, ujumbe tunaowapa kwakweli mwisho wa mwezi wa Nane (Agosti) mwaka huu, watu waanze kupata huduma za 4G katika maeneo haya.” Alisisitiza.

Aidha Mwenyekiti wa Bodi ya TCRA, Dkt. Jones Killimbe alisema Mradi huo utakuwa na faida kubwa kwa nchi na kwamba TCRA imekuwa ikitembelea miradi mikubwa (Flagship Project), kama vile ujenzi wa SGR, Jengo la tatu la abiria la kiwanja cha ndege cha Julius Nyerere Terminal III na leo tumekuja hapa kutembelea mradi huu mkubwa wa kimakakati wa bwawa kubwa la kufua umeme wa maji ambao utachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi, alifafanua Dkt. Kilimbe.

Alimshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa juhudi kubwa anazofanya kuhakikisha nchi inaelekea kwenye uchumi wa viwanda kwa uhakika zaidi kwa kuimarisha miundombonu wezeshi kama vile nishati ya Umeme wa uhakika na wa bei nafuu.

Nae Mhandsi Mkazi wa ujenzi wa bwawa hilo, Eng.Mushubila Kamuhambwa kutoka kampuni ya TECU, ambayo ni kampuni tanzu ya TANROADS, alisema bwawa hilo litakuwa ni miongoni mwa mabwawa makubwa yaliyotengenzwa na binadamu na litakuwa na urefu wa kilomita 100.

Akieleza faida za bwawa hilo licha ya kuzalisha umeme, pia shughuli za uvuvi wa samaki katika maeneo yatakayoainishwa, ongezeko la Mamba na Viboko ambao wanapatikana kwenye mto Rufiji lakin I pia kuwa kivutio cha utalii.
Hata hivyo alieleza changamoto za mawasiliano ya simu inayowakabili eneo la mradi na kuomba TCRA kuyahimiza makampuni ya simu kuboresha huduma zao.
 "Umbi letu, tunaomba muwasukume hawa wanaotoa huduma za mawasiliano ya simu, kwakweli mawasiliano ni changamoto kubwa sana kwenye eneo hili." Alisisitiza Mhandisi Kamuhambwa.
Baadhi ya wajumbe wa bodi na menejiment ya TCRA wakiwa kandokando ya Mto Rufiji Julai 28, 2019 wakati wa ziara ya kutembeela ujenzi wa Mradi wa umeme wa Mto Rufiji.
 

 Mwenyekiti wa Bodi, TCRA, Dkt. Jones Killimbe akifafanua jambo.
 Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Mhandisi Jmes M. Kilaba, akizungumza mwanzoni mwa ziara hiyo.
 Msafara wa TCRA ukipatiwa maelezo ya utekelezaji wa Mradi.
 Msafara wa TCRA ukiwa eneo la mradi












Share:

Membe Kakiri Sauti Iliyovuja na Kusambazwa Mitandaoni ni ya Kwake

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Bernard Membe, amesema sauti zilizovuja hivi karibuni kupitia mitandao ya kijamii ikihumusisha yeye akifanya mazungumzo na mtu asiyefahamika wakijadili juu ya sintifahamu ndani ya CCM ni ya kwake.

Membe ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na vyombo habari, ambapo amesema ni kweli sauti iliyodukuliwa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii ni ya kwake asilimia 100 huku akiomba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kuingilia kati suala hilo.
 

"Sauti ni za kwangu, ni mimi 100 kwa 100 na nimeifanyia kazi na ninajua imetoka wapi kwa sababu nina miiko ya kuzingatia sisemi.

"Ni sauti ya kwangu kabisa na ninaelewa kila kilichotokea. Unaweza kuingia ugonjwa wa udukuzi, kama wale wanaotoa taarifa hizi za udukuzi hawachukuliwi hatua, 'hackers' (wadukuzi) wapo duniani, wanataka fedha tu.

"Ni kosa la jinai kudukua mawasiliano ndiyo maana dunia nzima huwasikii wanadukuana waziwazi. Hapa kwetu watu wenye wajibu wa kukataza udukuzi ni TCRA (Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano) mitandao yote ipo chini yao.

"Tuna sheria zipo, sheria mpya ya mwaka 2013, sidhani kama imerekebishwa, inakataza katakata udukuzi na dunia nzima hamuisikii ikifanya hayo ". amesema Membe.


Share:

Wasiooga na Kufungua Nguo Wapigwa Marufuku Jijini Dar

Mkuu  wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amepiga marufuku watu wasiooga na kuwa nadhifu kuingia katikati ya jiji hilo wakati wa mkutano wa 39 wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) mwezi ujao.

Tayari vijana 130 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mgambo 300 wamesambazwa maeneo mbalimbali ya jiji hilo kusimamia usafi wa mazingira.

Akizungumza jana wakati wa kuzindua kampeni ya usafi wa mazingira kama sehemu ya maandalizi ya mkutano huo, Makonda alisema wamejipanga vyema, hasa katika suala zima la usafi kuepuka kumtia aibu Rais Dk. John Magufuli mbele ya marais wenzake.

“Wakati wa mkutano huu hatutarajii kuona watu wachafu mtaani. Tabia ya kuja mjini hujafua, hujaoga, hujanyoosha nguo ni marufuku, mpumzike tu majumbani kwenu.

“Kwa kipindi hiki tuvumiliane, kama hufui nguo, huogi, pumzika kidogo kuja mjini usitutie aibu, na siyo kwamba tunataka usafi tu wa mazingira hapana, usafi pia wa wananchi wetu, watu wamejaa chawa tu hapa,” alisema Makonda.

Pia aliagiza kuanzia sasa wenye magari binafsi watakaotupa taka ovyo wasitozwe faini badala yake wapewe eneo la kufanya usafi kwani baadhi yao wamekuwa na jeuri ya fedha na kwamba kwao faini si adhabu.


Share:

Agra Kuimwagia Mamilioni Tanzania Katika Utekelezaji Wa Mpango Wa Pili Wa Maendeleo Ya Sekta Ya Kilimo [ASDP II].

Na.Faustine  Gimu Galafoni ,Dodoma.
Serikali ya Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania inatarajia kupokea zaidi ya Ya  Dola za Marekani laki sita kutoka Taasisi ya Mapinduzi ya kijani Barani Afrika ( Alience Green Revelotion in Afrika   AGRA)  Katika utekelezaji wa mradi wa mpango wa Maendeleo  ya  sekta ya kilimo  awamu ya pili[ASDP  II]. 

Hayo yamesemwa Julai 29,2019  jijini Dodoma  na Katibu Mkuu ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhandisi . Joseph Nyamhanga wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kikao kazi cha Ofisi ya TAMISEMI ,Wizara ya Kilimo pamoja na AGRA Kilicholenga mpango mkakati wa maendeleo ya sekta ya kilimo awamu  ya pili[ASDP II  ambapo  amesema kuwa  kuna hatua kadhaa zitafanywa kabla ya kusaini mkataba huo ikiwa ni pamoja na kupata maoni ya Mwanasheria mkuu wa serikali na kuwasiliana na wizara ya fedha na mipango.

Hivyo,Mhandisi Nyamhanga amesema mradi huo utashirikikisha ngazi mbalimbali za Utawala ikiwa ni pamoja na  vijiji,kata,halmashauri,mikoa huku pia akisema  kuwa fedha hizo  ofisi ya TAMISEMI itasimamia ipasavyo kupitia maafisa kilimo na uongozi serikali za  mitaa. 

Naibu katibu mkuu Wizara ya kilimo Siza Donald Tumbo amesema kuwa mpango wa pili wa maendeleo ya kilimo lengo lake kuu  ni kuongeza uzalishaji pamoja na  kuondoa udumavu  na kuondoa dhana ya kilimo kwa ajili ya kuhimili njaa peke yake bali ni kujikita katika kilimo biashara. 

Malengo mengine ya ASDP II ni kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo bora za kilimo kwa bei rahisi huku akibainisha kuwa changamoto ya usafirishaji wa Mazao kwa sasa haipo kwani miundo mbinu ya barabara iko vizuri na kilichobaki ni kuzalisha mazao bora  na upatikanaji wa masoko kwa urahisi zaidi.

Vianey Luendela ambaye ni  Meneja wa AGRA Nchini Tanzania amesema  AGRA imekuwa mdau wa maendeleo ya kilimo kwa miaka 15 nchini Tanzania na AGRA imesha wekeza  Dola Milioni 60 za Tanzania toka imeanzishwa katika eneo la kilimo.

Ikumbukwe kuwa ASDP ni mchakato wa muda mrefu uliobuniwa kutekeleza (ASDS), na ndiyo nyenzo kuu (main tool) ya Serikali katika kuratibu na kufuatilia maendeleo ya kilimo ambapo Programu hii inaoanisha utekelezaji kati ya wizara za sekta ya kilimo na wadau wengine na kuleta ufanisi katika mfumo wa usimamizi.  

Aidha, ASDP inaunganisha mahitaji halisi shambani katika ngazi ya wilaya na kuoanisha ufuatiliaji na uimarishaji wa uwekezaji katika ngazi ya kitaifa na kimataifa katika sekta ya kilimo huku Mtazamo mkuu wa ASDS na ASDP ni kuwapa uwezo wazalishaji wadogo, wa kati na wakubwa wa sekta ya kilimo kupata faida kutokana na kuongeza uzalishaji na tija katika shughuli zao. 


Share:

Waziri Mkuu Akagua Ujezi Wa Ofisi Za Halmashauri Na Hospitali Ya Wilaya Ruangwa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa na ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo.

Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa na yuko jimboni kwake kwa mapumziko mafupi, alikagua ujenzi huo jana jioni (Jumatatu, Julai 29, 2019). Jengo hilo linalojengwa na SUMA JKT, linahitaji sh. bilioni 3.77 hadi kukamilika kwake.

Akiwa kwenye eneo la ofisi hizo, Waziri Mkuu alielezwa kwamba Halmashauri hiyo imepokea shilingi milioni 500 kutoka Serikali Kuu kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mpya ya Halmashauri hiyo.

Ujenzi wa ofisi hiyo ambayo ikikamilika itakuwa na ghorofa moja, ulianza Juni mosi, 2019 na unatarajiwa kukamilika Julai, mwakani. Jengo litakuwa na ofisi 33 za chini, ofisi 26 za ghorofa ya kwanza na kumbi mbili za mikutano.

Kazi ambazo zimeshafanyika hadi sasa ni usafishaji wa eneo kwa ajili ya ujenzi; upimaji wa sampuli ya udongo (Geotech Survey); uingizaji wa maji eneo la ujenzi; uchimbaji wa kisima kikubwa cha kuhifadhia maji  na uvutaji wa umeme eneo la ujenzi.

Kazi zinazoendelea kwa sasa ni ufyatuaji wa tofali ambapo hadi sasa jumla ya matofali 10,000 yamekwishafyatuliwa ambayo ni sawa na asilimia 50 ya mahitaji ya matofali yote. Pia ukusanyaji wa vifaa vya ujenzi eneo la ujenzi unaendelea.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu jana alikagua ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo na kukiri kwamba ameridhishwa na kazi iliyokwishafanyika hadi sasa.

Akiwa hospitalini hapo, Waziri Mkuu alielezwa na Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt. Mahela Njile kwamba hadi kukamilika kwake, hospitali hiyo itakuwa na majengo 22 yanayokisiwa kugharimu jumla ya sh. bilioni 7.5 kulingana na maksio ya OR-TAMISEMI.

Dkt. Njile alisema katika awamu ya kwanza Serikali imetoa sh. bilioni 1.5 na kuelekeza yajengwe majengo saba ya kipaumbele ambayo ni jengo la uzazi, la wagonjwa wa nje (OPD), maabara, la X-ray, la utoaji dawa, la kufulia nguo na la utawala.

“Serikali imeelekeza ujenzi huu ufanyike kwa kutumia njia ya manunuzi inayoitwa ‘Force Account’ ambapo Halmashauri inanunua vifaa vya ujenzi na kuajiri mafundi wa kujenga majengo yaliyoelekezwa wakisimamiwa na wataalam wa halmashauri na kamati mbalimbali,” alisema.

Akizungumza na wakazi waliojitokeza kumsikiliza hospitalini hapo, Waziri Mkuu aliwapongeza viongozi wa Halmashauri hiyo kwa kusimamia vizuri ujenzi na kwa kuamua kutumia force account ambayo alisema inapunguza sana gharama za manunuzi.

Aliitaka Halmashauri hiyo isisubiri hadi kazi ya ujenzi ikamilike, na badala yake wahusika wajipange na kuanza kufanya usafi wa eneo linalozunguka hospitali hiyo. “Halmashauri tusikae tu kusubiri ujenzi uishe. Tufanye usafi kuzunguka eneo lote, tupande miti na maua ili mandhari ianze kupendeza,” alisema.

Kuhusu muda wa kukamilisha kazi hiyo, Waziri Mkuu aliwashauri mafundi wazidishiwe muda wa kufanya kazi. “Badala ya kufanya kazi mchana peke yake, bora waongezewe muda wafanye hadi usiku ili kufidia muda uliopotea, na uliobakia ni mfupi mno,” alisema.

Alisema anaamini kazi hiyo itakamilika ndani ya muda mfupi ili huduma zianze kutolewa hapohapo Ruangwa na kuwapunguzia wananchi adha ya kwenda hadi hospitali ya Ndanda.

 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,       


Share:

Rais Magufuli Atengua Uteuzi wa Mkurugenzi wa Shirika la Bima la Taifa (NIC)




Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumanne July 30




Share:

Monday 29 July 2019

Mhagama Aagiza Maafisa Vijana Wazembe Watimuliwe Mara Moja

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Waziri wa Ofisi ya Waziri  mkuu,sera Bunge kazi vijana ,Ajira na Watu wenye Ulemavu ,Mhe.Jenista Mhagama ametoa agizo kwa  katibu mkuu wa Wizara hiyo kuhakikisha anasimamia na kuwaondoa kazini Maafisa Vijana wanaofanya uzembe wa utekelezaji wa Majukumu yao ndani Ya  Halmashauri husika. 

Mhe.Mhagama ametoa maagizo hayo leo Julai 29,2019  jijini Dodoma Katika uzinduzi wa Mafunzo ya  siku tatu ya  ujasiriamali na Usimamizi wa biashara kwa vijana . 

Mhe.Mhagama amesema pamekuwa na kazi ya mazoea kwa baadhi ya maafisa vijana ngazi ya halmashauri na wamebaki kusubiri fedha za mikopo pekee kutoka serikalini badala ya kuwajibika kutafuta fursa kwa vijana hivyo amesema viongozi wa namna hiyo hawana nafasi kinachotakiwa ni kuwaondoa tu. 

Aidha,Mhe.Mhagama ameziagiza taasisi za kifedha hapa hapa nchini kuwa na masharti nafuu ya mikopo kwa vijana kwani sharti la kigezo cha kuweka dhamana ya nyumba kijana hawezi kumudu kwa sababu asilimia kubwa ya vijana wanaishi nyumba za wazazi wao. 

Katibu mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji kiuchumi Bi.Beng’i Isa amesema   kwa miaka mitano wameweza kuwafikia vijana  elfu kupitia program mbalimbali za mafunzo. 

Katibu mkuu Ofisi ya Waziri mkuu,kazi,vijana,ajira  na wenye ulemavu Bw.Andrew Masawe mafunzo ya kurasimisha ujuzi  na mafunzo  mtambuka ya kilimo cha kisasa cha kitalu nyumba yamefikia halmashauri 87  hadi sasa huku kila halmashauri ikifikia vijana mia moja [100]. 

Manaibu mawaziri Ofisi ya Waziri mkuu,kazi,vijana,Ajira na Wenye Ulemavu,Stella Ikupa amesema  Programu hiyo itakuwa jumuishi kwa vijana wote wakiwemo wenye ulemavu  huku Anthony Mavunde akisema vijana wa kitanzania wanatakiwa kujiamini katika suala la maendeleo.

Mafunzo ya Ujasiriamali na Usimamizi  wa Biashara kwa vijana yanakutanisha kutoka mikoa 26 Tanzania bara huku kaulimbiu ikiwa ni “Wezesha vijana kujiunga na Msingi Endelevu wa ajira”.


Share:

Mbowe azuiwa kufanya mikutano Kumpisha DC Sabaya

Jeshi la Polisi Wilaya wa Hai limemtaka Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe kusitisha mikutano aliyopanga kuifanya kwa sababu DC Lengai Ole Sabaya anafanya ziara, hivyo mikutano itaingiliana, jambo linaloweza kusababisha uvunjifu wa amani.

 Ziara hiyo ya Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema ilitakiwa ianze leo lakini iliahirishwa jana Jumapili Julia 28, 2019 baada ya mbunge huyo kufiwa na kaka yake, Meja Jenerali Alfredy Mbowe.

Leo Jumatatu Julai 29, 2019 barua iliyotolewa na Mkuu wa Polisi wilayani ya Hai, Lwelwe  Mpina yenye kumbukumbu namba MB/JH/27/07/2019  kwenda kwa katibu wa mbunge (Mbowe) imezungumzia kusitishwa kwa ziara hizo za Mbowe.

Zuio hilo litakoma DC akimaliza ziara yake; “Kwa busara, sitisha ziara na mikutano unayotegemea kuifanya  hadi mkuu wa wilaya atakapomaliza ziara yake,” inasomeka barua hiyo


Share:

KASI YA UTENDAJI WA RAIS DKT MAGUFULI YAMKIMBIZA DIWANI WA CUF PANGANI ...AJIUNGA CCM SHANGWE ZIKIRINDIMA


Katibu wa Idara ya Organization ya Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa Pereira Silima kulia akipokea kadi ya Chama cha wananchi (CUF) kutoka kwa aliyekuwa Diwani wa Kata ya Pangani Mashariki (CUF) Akida Boramimi baada ya kujiunga na chama hicho kwenye mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) Jumaa Aweso ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji 

Katibu wa Idara ya Organization ya Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa Pereira Silima kulia akimkabidhi kadi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyekuwa Diwani wa Kata ya Pangani Mashariki (CUF) Akida Boramimi baada ya kujiunga na chama hicho juzi kwenye mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) Jumaa Aweso ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji
Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) Jumaa Aweso ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye eneo la sokoni wilayani Pangani.
Katibu wa Idara ya Organization ya Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa Pereira Silima akizungumza wakati akimpokea aliyekuwa Diwani wa CUF Kata ya Pangani Mashariki Akida Boramimi kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Pangani Rajabu Abdallah.
 Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Pangani Rajabu Abdallah akizungumza wakati wa mkutano huo wa Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) Jumaa Aweso ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji 
Katibu Tawala wa wilaya ya Pangani Mwalimu Hassani Nyange akizungumza wakati wa mkutano huo
Katibu wa Idara ya Organization ya Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa Pereira Silima akivishwa skafu mara baada ya kuwasili  wilaya ya Pangani
Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Pangani Mashariki Akida Boramimi(CUF) akizungumza ambapo alisema kasi na utendaji mzuri wa Rais Dkt John Magufuli umemvutia na kuamua kujiunga na CCM
Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) Jumaa Aweso ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji kushoto akimkabidhi vifaa vya kujikingia na jua ikiwemo kofia na vitu vingine kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa ngozi wilayani humo kiongozi wao kulia 
Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) Jumaa Aweso ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji  kushoto akiwa na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Pangani Rajabu Abdallah mara baada ya kukabidhi baiskeli kwa watoto wenye ulemavu 
 Sehemu ya wananchi wakimsikiliza  Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) Jumaa Aweso ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji 
Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Pangani Mashariki kupitia tiketi ya chama cha Wananchi (CUF) Akida Boramini ametangaza uamuzi wa kuachana na chama hicho na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Akida alitangaza uamuzi huo mwishoni mwa wiki iliyopta mjini Tanga wakati wa mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM) Jumaa Aweso ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji uliofanyika eneo la Sokoni.

Baada ya kutangaza uamuzi huo ambao uliibua shangwe na nderemo kwa wana CCM ambao waliohudhuria mkutano huo na baadae kulazimika kutembea kwa maandamano mpaka zilizopo ofisi za CCM wilaya hiyo na kwenda kumkabidhi kadi.

Diwani huyo ambaye ni mahiri kwenye kujenga hoja hususani anapokuwa kwenye vikao mbalimbali vya kimaendeleo kwenye baraza na hata vile vya kawaida alipofika kwenye ofisi hiyo alikabidhiwa kadi na Katibu wa Idara ya Organization ya Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa Pereira Silima.

Alisema kubwa ambalo limepelekea kuamua kujiunga na chama hicho ni kutokana na kasi ya utendaji ya Rais Dkt John Magufuli ya kuhakikisha wanatanzania wanapata maendeleo na ndio sababu iliyompelekea kuamua kuchukua maamuzi hayo

“Kwa kweli Rais Dkt John Magufuli amefanya mambo mengi makubwa sana na ndio maana nimeona nimuunge mkono kwani kwenye masuala ya barabara na maji yanayopatikana hakuna haja ya kuendelea kuwa mpinzani…Lakini mimi niseme kwamba nimekuwa kada ya CUF tokea mwaka 1999 na ndio nimekabidhiwa kadi”,alisema.

“Lakini katika kuhamia CCM sijaja pekee yangu nimeambatana na wanachama wengine wa ACT akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi (ACT) Pangani Ally Mbwaro ,Wanachama kutoka Chadema na vijana wa bodadoda Pangani lengo kubwa ni kuhakikisha tunashirikiana kwenye hali ya kuijenga Pangani mpya”,alisema.

Akida Boramimi ambaye ni mzaliwa wa wilaya ya Pangani alikuwa diwani wa Kata ya Pangani Mashariki (CUF) tokea mwaka 2015akimshinda aliyekuwa mpinzani wake Leopard Abeid kwa kuwa zaidi ya kura 500.

“Nimekaa nimejitafakari kwa namna mambo ya nchi yanavyokwenda nikaona sina budi kutangaza rasmi kurudi CCM na ni sikuja pekee yangu nimekuja na wenzangu wapatao 50 hivyo ninaomba mtupokee na kututhamini ",alisema.

Naye kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Pangani Aweso alisema kwamba serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Magufuli imefanya mambo mengi makubwa ambayo yamekuwa chachu kubwa ya maendeleo kwa watanzania.

Alisema kwamba tangu alipochaguliwa kuwa mbunge wa Jimbo hilo ameweza kuhakikisha sekta ya elimu inaimarika wilayani humo ikiwemo kupandisha kiwango cha ufaulu kutoka kuwa wilaya ya mwisho kupanda kwenye nafasi za juu.

Alisema pia licha ya hivyo lakini pia amesimama imara kwa kuhakikisha wanaanzisha madarasa ya kidato cha Tano na Sita hali ambayo imepelekea wanafunzi wanaofaulu kupata fursa ya kupata elimu.

“Lakini pia niwaambie tumeweza kushghulikia kwa asilimia kubwa suala la maji ambapo mkataba wa milioni 575 umesainiwa kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya maji na utekelezaji wake umefikia asilimia 90”Alisema Mbunge Aweso ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji.

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger