Monday, 31 December 2018

WAHAMIAJI HARAMU 13 WAFARIKI BAADA YA KUTUPWA MOROGORO

Wahamiaji 13 kati ya 26 raia wa Ethiopia wamefariki dunia baada ya kutupwa eneo la Sangasanga mkoani Morogoro Barabara Kuu ya Iringa- Morogoro na gari aina ya lori ambalo halijajulikana.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumapili Desemba 30, 2018, Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa alisema tukio hilo liliripotiwa saa 9 alasiri jana na Vyombo vya usalama kwenda eneo la tukio na kukuta raia 26 kati yao 13 wakiwa wamepoteza maisha.


Mutafungwa amesema watumiaji wa barabara hiyo waliiona miili ya raia hao pembeni mwa barabara na kutoa taarifa kwa askari wa kikosi cha usalama barabarani eneo la Sangasanga.


Kamanda huyo amesema kati ya raia hao yumo mtoto wa miaka minane na polisi wanaendelea na uchunguzi ili kulibaini lori na wahusika wa tukio hilo.
Share:

MAMA MJAMZITO NA MWANAE WAFARIKI KWA UZEMBE WA WAUGUZI

Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo
** 
Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo, ametoa saa 72 sawa na siku tatu kwa uongozi wa hospitali ya wilaya, kuwachukulia hatua kali watumishi wanaodaiwa kusababisha
kifo cha mjamzito.


Milo Peter (29), mkazi wa mtaa wa Masanga, Igunga, alifariki Desemba 29, mwaka huu na kuzikwa katika makaburi ya Masanga.

Baadhi ya wajawazito waliolazwa katika hospitali hiyo, waliwalalamikia watumishi wawili kufanya kazi kizembe, hali inayodaiwa kusababisha kifo cha Milo na mtoto.

Mbele ya diwani wa kata ya Igunga Charles Bomani, wajawazito hao, walidai mwenzao hakupata matibabu yanayostahili mapema, licha ya kuomba msaada kwa wauguzi waliokuwa zamu.

Kwa nyakati tofauti Blandina Enock, Rahel John, Rusia Ramadhani na Sikudhani Mrisho, walidai mwenzao alifikishwa hospitalini hapo Desemba 27, mwaka huu saa mbili usiku kwa ajili ya kujifungua.

Walisema kuwa, Milo alipofika alipewa kitanda huku ndugu zake waliomfikisha hospitalini, wakipewa ruhusa kuondoka.

"Jamani mnajua ufike wakati tuseme ukweli kwani kifo cha mama mwenzetu, kinaonekana kabisa uzembe umechangia.

"Sisi wenyewe tumeshuhudia kabisa namna ambavyo alikuwa akiomba msaada kwa wauguzi," alidai Rahel kwa niaba ya wenzake.

Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Amada Kasigwa, alikiri kutokea kwa kifo hicho cha mjamzito na mtoto mchanga mwenye uzito wa kilogramu 3.8.

Alisema kuwa vifo hivyo vilitokea Desemba 28, mwaka huu na kudai hali hiyo imetokana na uzembe wa muuguzi wa zamu, Matinde Muhonye. 

Kwa mujibu wa Amada, mtumishi huyo alionywa kuhusu madai hayo ya ufanyaji kazi kizembe.
Share:

TATIZO LA AJIRA KWA VIJANA NI KUBWA KULIKO TATIZO LA KIKOKOTEO CHA MAFAO YA KUSTAAFU


Ameandika Dotto Bulendu kwenye ukurasa wake wa Facebook
Tatizo la ajira kwa vijana nchini Tanzania ni kubwa kuliko tatizo la kikokoteo cha mafao ya kustaafu.

Kama tulivyopiga kelele kuitaka Serikali itazame upya uamuzi wake wa kuwalipa wastaafu asilimia 25 ya mafao yao ya kustaafu na kilichobaki walipwe kidogo kidogo,kelele hizo hizo zinatakiwa kupigwa ili tupate ufumbuzi wa tatizo la ajira nchini maana tunajitengeneza bomu wenyewe.

Ikiwa kati ya Mwaka 2015 mpaka Disemba 18.2018 Jumla ya vijana Laki tano ,tisini na nne elfu na mia tatu(594,300)waliomba kazi serikalini na waliopata kazi walikuwa ni elfu sita na mia tano hamsini na nne(6,554) ukiwa ni wastani wa watu mia moja(100) wanaoomba kazi serikalini ni mmoja tu ndiye mwenye uhakika wa kupata kazi,tunahitaji kupiga kelele,kushauri,kuonya juu ya athari za kuwa na kundi kubwa la vijana wanaosaka kazi.

Rafiki yangu mmoja aliandika mtandaoni kuwa vijana wengi ni "Book Smart" huku wakikosa ujuzi wa namna ya kukabili changamoto za mtaani (Street smart)ndiyo maana tuna kundi kubwa la vijana waliokata tamaa na maisha huku wakiwa na shahada zao mkononi.

Kama ni hivyo lazima tuje na mpango wa haraka utakaobadili elimu yetu ili vijana hao wenye shahada zinazovutia ila wanahangaika mtaani wanapokuwa vyuoni mpaka vyuo vikuu wapate vyote, yaani wawe "Book smart" na "street smart",wazijue fursa zilizopo mtaani na namna ya kuzitumia ili tujinasue na hatari ya kuwa na kundi kubwa la vijana wasio na kazi.

Kama ndani ya miaka mitatu vijana zaidi ya laki tano na nusu walipambana kusaka kazi serikali na wakapata watu elfu sita na mia tano, hii maana yake nini?kufikia mwaka 2020 tunaweza kubwa na kundi kubwa linalopindukia vijana milioni moja wenye sifa za kitaaluma na wapo nyumbani hawana cha kufanya,maana vyeti vyao vyenye GPA haviwapi kazi wala hawawezi vitukia kupata mkopo benki wala serikalini.

Hivi karibuni,shirika la afya duniani lilipata kusema vijana milioni 3.7 wanaugua ugonjwa wa Sonona(Depression),kutokana na changamoto za maisha wanazokutana nazo ikiwemo ukosefu wa ajira na ugumu wa maisha,achilia mbali sababu za kimahusiano na usaliti kwenye ndoa zao.

Vijana nchini Tanzania sasa wanakutana na fursa chache za ajira huku wale waliomo makazini wakikumbana na changamoto za kulipwa kidogo,kukopwa mishahara yao huku wakifanyishwa kazi kwa muda mrefu na katika mazingira magumu.

Vijana wengi walio makazini wanakilio cha kukaa kazini muda mrefu bila kupandishiwa malipo yao huku ukali wa maisha ukipanda kila kukicha,lakini hili ni kundi dogo,kundi kubwa lipo mtaani.

Nilipokuwa namsikiliza Rais John Magufuli wakati akizungumzia sakata la kikokoteo ,alisema mpaka mwaka 2023 kutakuwa na wastaafu takribani elfu 58 watakaotakiwa lipwa mafao,hawa kilio chao kimesikika.

Tujiulize kwa pamoja,kama kati ya mwaka 2015 mpaka Disemba 2018 vijana zaidi ya laki tano waliomba kazi serikalini na laki tano na zaidi wakakosa,je mpaka kufikia mwaka 2023 tutakuwa na kundi la vijana wangapi wanaopambania kazi serikalini?

Sasa hivi sekta binafsi imepunguza kasi ya kuajiri ,inachokifanya sasa ni kupunguza wafanyakazi wake na kimbilio lake ni serikali ambayo watu ambao imewaajiri hawafiki hata milioni moja!

Tunawasaidiaje vijana wetu wenye changamoto ya kuwa "Book smart"?je tuwalaumu tu kuwa wamesoma na hawajui maisha ya mtaani?na je ni kweli shuleni,vyuoni mpaka vyuo vikuu vijana wetu hawafundishwi namna ya kuyaishi maisha ya mtaani na changamoto zao?kama ndiyo nani alaumiwe?je ni wao ndiyo waliotengeneza mtaala ambao mwisho wa siku unawaacha wakiwa "Book smart" wasiojua maisha ya mtaani?

Tunawasaidiaje vijana wetu?

Juzi nilikuwa nasafiri kati ya Mwanza na Shinyanga nikapita eneo linaitwa Mabuki nikaambiwa wakati wa Nyerere kulikuwa na mashamba makubwa ya mazao na mifugo leo pamebaki hamna kitu,tukifufua hapo tutaajiri vijana wangapi?

Nilipofika Shinyanga nikaona kiwanda cha Nyama kimefungwa,nikauliza mbona wasukuma wanafuga na watu wanakula nyama kwa nini hakifanyi kazi?sikupata majibu na ninaambiwa kiwanda hiki kilijengwa mwaka 1974 na Mwalimu Nyerete,tukifufua hiki tutaajiri vijana wangapi?
Hapa Mwanza kila nikienda Airport napita kiwanda cha Ngozi Ilemela,huwa nakumbuka siku moja kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015,Rais Magufuli akiwa mgombea alisema akishinda atahakikisha kiwanda hicho kinafufuka na akatoa siku saba kianze kazi.

Kiwanda hicho kilijengwa na Serikali ya Nyerere,lakini jana nimepita hapo sioni kinachoendelea,najiuliza kwani wasukuma hawafugi tena?kwani watanzania hawavai viatu vya ngozi?tukifufua hiki kiwanda tutaajiri vijana wangapi?
Kila napoenda Nyakato hupita kiwanda cha nguo ya Mwatex,nchi kilijengwa na Serikali ya Nyerere lakini sasa sioni kinachoendelea,najiuliza dada na mama zetu hawavai tena kanga?wasukuma hawalimi tena pamba?tukifufua hiki kiwanda tutatengeneza ajira ngapi?

Ni kama nilipokwenda Tabora wiki mbili zimepita nikaambiwa kile kiwanda cha nyuzi kilichokuwa kinaajiri kundi kubwa la vijana pale Tabora nacho ni kama kishaenda halijojo kitambo,nikajiuliza hivi watanzania hawashoni? siku hizi?nguo zao hazichaniki?nikaambiwa nyuzi siku hizi zinatoka China,nikajiuliza hivi tukifufua hiki tutaajiri vijana wangapi?

Bahati mbaya sana,fikra za viongozi wetu ni kuwa wanadhani serikali itajenga viwanja,itarejesha,italima na kuendesha mashamba makubwa ,Itafuga mifugo,itavua yenyewe.
Tusipoamua kuotekeleza Sera ya ubia kati ya serikali na sekta binafsi,sera ya wazawa ili kuhakikisha tunatengeneza matajiri wakubwa wazawa wakashikilia njia kuu za uchumi kwa ubia na serikali huku tukiwa wakali kwenye Rushwa hatutatoka abadani.

Tunawalaumu vijana na kuwataka wajiajiri,je tumewapa mitaji?maana siku hizi utawasikia watu wanasema wewe ukiwa na wazo tu unatoka,unabaki na maswali hivi hawa vijana laki tano wote hawana mawazo ya kujiajiri kweli?
Ukimsikiliza anayesema hivyo yeye alianza na mtaji wa zaidi ya milioni kumi,tena yupo kazini,kachukua mkopo kwa dhamana ya kazi yake,hawa vijana masikini hawa tunawasaidiaje na vyeti vyao vya chuo kikuu?

Hebu serikali ijaribu kuwaambia hawa vijana kuwa Cheti chako cha stashahada,shahada,shahada ya uzamili ama uzamivu kinaweza kuwa dhamana ya kuchukuliwa mkopo kwa Riba ndogo na tuwe na mpango kabambe wa kuwafanya vijana wetu wazijue fursa zilizopo ndani na nje ya nchi kutoka sekta ya kilimo,uvuvina ufugaji tuone kama utawaona wa akimbizana Wizara ya Utumishi kuomba kazi.

Vijana wetu wanahitaji zaidi ya hiki wanachopata vyuoni,wanahitaji "Skills" zaidi na binafsi wengi naowafahamu mimi wana "Skills" za kutosha katila maeneo waliyoyasomea lakini wanakosa mtaji ili wajiajiri wenyewe.
Tunaweza jidai hatuoni,hatusikii sauti zao,lakini ukweli ni kwamba tatizo la ajira kwa vijana tukilibeza na kubaki kupigana vijembe,tunatengeneza bomu kubwa na kuongeza idadi ya vijana wanaougua Sonona.

Wasalaaam
Muwe na maandalizi mema ya mwaka mpya wa 2019.
soma maoni hapa
Share:

Sunday, 30 December 2018

MWANAUME AFARIKI KWA KUBANWA KATIKATI YA MAPAJA YA MWANAMKE


Mwanaume mmoja katika kijiji cha Gionsaria,kaunti ya Kisii Nchini Kenya amefariki dunia baada ya mwanamke mmoja kumbana /kufungia kichwa cha mwanaume huyo katikati ya mapaja. 




Mkasa huo wa aina yake umetokea siku ya Ijumaa Disemba 28,2018. 


Chifu wa eneo hilo Bwana Oganda Matego amesema mwanaume huyo anayejulikana sana kwa jina ‘Doctor’,ambaye pia ni taniboi wa magari ya kusafirisha majani chaieneo hilo, alishikiliwa kichwa katikati ya mapaja/miguu na mwanamke mmoja huku rafiki wa mwanamke huyo ambaye pia ni mwanamke akiwa ameshikilia miguu ya ‘Doctor’na kumuinua hewani.


Bwana Oganda amesema inashukiwa kuwa wawili hao walikuwa wapenzi na kifo cha ‘Doctor’ kilitokea wakicheza ambapo Baada ya dakika moja mwanaume akaachilia kichwa na kugonga kichwa barabarani



Inaelezwa kuwa wanawake hao walimpeleka ‘Doctor’ katika hospitali ya wilaya ya Nyamache na madaktari walipompima wakabaini kuwa tayari alikuwa amefariki dunia.



Tayari wanawake hao wanashikiliwa na polisi kwenye kituo cha polisi cha Nyangusu huku wakisubiri kufunguliwa mashtaka.



Aidha baada ya habari ya kifo cha ‘Doctor’ kuwafikia majirani wa wanawake hao,waliamua kuchoma nyumba nne zinazomilikiwa na hao wanawake. 


Hali ya utulivu imeshuhudiwa kwa sasa na Chifu wa eneo hilo Bwana Oganda Matego amewasihi wakazi wa eneo hilo kutochukua sheria mikononi mwao kiholela.




Share:

WAZIRI AWAPIGA MARUFUKU TRA KUFUNGIA BIASHARA ZA WADAIWA KODI

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amepiga marufuku Mamlaka ya Mapato nchini TRA kuwafungia wafanyabiashara, biashara zao kwasababu ya madeni ya kodi wanayodaiwa.

Ametoa kauli hiyo jijini Dodoma  Desemba 30, 2018 wakati akitoa taarifa ya hali ya uchumi wa taifa na utekelezaji wa bajeti ya serikali kwa kipindi cha miezi sita katika mwaka wa fedha 2018/19.

"Ninaukumbusha uongozi wa Mamlaka ya Mapato utekeleze maagizo ya Mhe Rais aliyoyatoa wakati wa ufunguzi wa kikao cha utendaji kazi wa mamlaka kilichofanyika ukumbi wa Mwl Nyerere tarehe 10 Desemba 2018," amesema.

"Utaratibu wa kumfungia mfanyabiashara biashara yake ili kushinikiza alipe kodi anayodaiwa, usitishwe isipokuwa kwa mkwepaji sugu na kwa kibali cha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania," ameongeza.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Mpango amesema makusanyo ya ndani yameongezeka na kufikia shilingi trilioni 7.37 sawa na asilimia 88.9 huku mapato yatokanayo na kodi yakiwa ni trilioni 6.23 sawa na asilimia 88 ya lengo lililowekwa kwa kipindi hicho.

Waziri Dk Mpango pia amesema mapato yasiyo ya kodi yamevuka zaidi ya lengo na kufikia asilimia 121 kwa kukusanya bilioni 936.03 ambayo ni zaidi ya lengo la shilingi bilioni 775.36 huku mapato ya halmashauri yakifikia bilioni 203.8 ikitokana na kuimarishwa kwa mfumo wa ukusanyaji mapato wa serikali hasa kwa njia za kielektroniki.

Aidha Wziri Mpango ameitaka mamlaka ya mapato nchini TRA kuhakikisha inatoza kodi kwa mujibu wa sheria na kanuni zake na kuondoa manyanyaso kwa wafanyabiashara ili wahamasike kuchangia kodi
Chanzo:Eatv

Share:

KATIKA KUFUNGA MWAKA UWT PWANI YAFUNGA 2018 NA HILI

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoa wa Pwani,Bibi Farida Mgomi, ametoa shukrani nzito kwa viongozi wote wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali kwa kuonesha ushirikiano mkubwa kipindi ambacho walikuwa ziarani katika wilaya zote za mkoa huo. UWT Mkoa wa Pwani walianza ziara yao mwanzoni mwa mwezi wa saba (7)na kumaliza mwanzoni mwa mwezi wa Kumi na mbili (12) Wakiwa katika Ziara zao huko wilayani walipokelewa vizuri na Viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Chama wa Wilaya, Mkuu wa Wilaya,Mwenyekiti wa Halmashauri, Mbunge wa Jimbo husika, Viongozi wa Jumuiya…

Source

Share:

MBUNGE NJOMBE ASIMAMA JUU YA KITANDA KUTAFUTA MTANDAO WA SIMU

Na.Amiri kilagalila Changamoto ya mawasiliano kwa Njia ya simu ni moja ya shida ambayo imekuwa ikiyakumba baadhi ya maeneo hapa nchini hususani katika maeneo ambayo ni mapya kiutawala kama ilivyo katika maeneo machache ya wilaya ya Ludewa na jimbo la Lupembe mkoani Njombe. Kutokana na changamoto hiyo,Mbunge wa jimbo la Lupembe lililopo halmashauri ya wilaya ya Njombe kaskazini mwa mkoa huo mh.Joram hongoli,amemuomba Naibu waziri wa ujenzi Elias kwandikwa wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Lupembe kuwasaidia kutatua changamoto hiyo kwa kuwa yeye ni miongoni mwa waathirika wakubwa wanaokosa…

Source

Share:

SERIKALI YATOA UFAFANUZI KUHUSU SAKATA LA MWANANCHI KUKAMATWA AKISAFIRISHA VITANDA VIWILI

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umepokea taarifa kupitia mitandao ya kijamii na wadau mbalimbali zinazohusisha namna Afisa Misitu wa Wilaya ya Korogwe alivyokuwa akitekeleza majukumu ya kusimamia Sheria ya Misitu Na. 14 ya Mwaka 2002 pamoja na Kanuni zake za Mwaka 2004.

 Afisa huyo alikuwa akitekeleza majukumu hayo kwa mujibu wa kifungu cha 93 (Powers of officers with respect to offences) inayompa mamlaka Afisa Misitu au Afisa wa Jeshi la Polisi kukagua, kukamata na kuzuia mazao yanayodhaniwa kupatikana kinyume na sheria.

Kufuatia taarifa hizo, uongozi wa TFS umefanya uchunguzi wa haraka na kubaini kuwa abiria mmoja alikuwa akisafirisha vitanda viwili (2) vipya kwa basi. Vitanda hivyo vililipiwa ushuru wa Serikali kupitia mfumo wa Kielektroniki wa Malipo Serikalini (GePG) na kupewa stakabadhi halali ya tarehe 26 Disemba, 2018 katika kituo cha Mkata, Handeni Mkoani Tanga.

Katika kutekeleza majukumu yake, Afisa wetu alimtaka abiria huyo kuonesha Hati ya Kusafirishia (Transit Pass) bidhaa hizo kwa mujibu wa Kanuni ya 13(4) ambayo inakataza mwenye chombo chochote cha usafiri kusafirisha mazao ya misitu ambayo hayana hati ya usafirishaji ambapo abiria huyo hakuwa nayo. 

Hata hivyo, Afisa wetu alishindwa kutafsiri masharti ya kifungu hiki na mahitaji ya utoaji wa Hati ya Usafirishaji kwani kama msafirishaji binafsi kwa matumizi ya nyumbani asingeweza kukidhi vigezo vya kuwa na hati hiyo. 

Hati ya Usafirishaji huhitaji msafirishaji kuonesha usajili, leseni ya biashara, utambulisho wa mlipa kodi na namba ya usajili wa chombo kinachotumika kusafirisha mazao hayo pamoja na kuonesha vituo atakavyopaswa kukaguliwa.

Kufutia tukio hilo, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania unamwomba radhi abiria huyo na umma wa watanzania kwa tukio hilo na usumbufu uliojitokeza. Wakala unaendelea kufuatilia suala hili, na utahakikisha kuwa tukio kama hili halijirudii tena.

 Aidha, hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa mujibu wa Kanuni za utumishi wa umma dhidi ya mtumishi aliyehusika na utoaji wa lugha isiyo na staha wakati akitekeleza sheria ya misitu ambapo alitegemewa kutoa elimu stahiki kwa umma. Hivyo, TFS inapenda kufafanua mambo yafuatayo:- 2

1. Kwamba ikiwa mwananchi yeyote amenunua samani mpya kutoka kwa watengenezaji au wauzaji mahali popote kuhakikisha anapatiwa risiti halali kwa malipo aliyofanya. Hivyo, mmiliki wa samani mpya kwa matumizi binafsi halazimiki kuwa na Hati ya Usafirishaji anaposafirisha toka eneo moja kwenda jingine isipokuwa awe tayari kuonesha uthibitisho wa nyaraka za malipo halali ya samani hizo kwa ukaguzi pale itakapohitajika.

2. Mwananchi yeyote anayesafirisha samani zilizotumika kutoka eneo moja hadi jingine halazimiki kuwa hati za malipo wala kuwa na hati ya kusafirishia samani hizo.

3. Serikali itaendelea kufanya mapitio ya Sheria ya Misitu na Kanuni zake ili kuepuka mkanganyiko wowote wa tafsiri ya sheria unaoweza kujitokeza na kuondoa usumbufu kwa wananchi.

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania unapenda kutoa rai kwa wananchi wote kuendelea kuzingatia Sheria za uhifadhi wa misitu. Aidha, Wakala hauna nia ya kuzuia utengenezaji, usafirishaji na matumizi ya samani za mbao mahali popote nchini ilimradi tu upatikanaji wa malighafi zake uwe umefuata utaratibu. Lengo ni kuhakikisha kuwa rasilimali za misitu zinatunzwa na kutumika kwa njia endelevu kwa maendeleo ya Taifa. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania utaendelea kutoa elimu kwa umma pamoja na watumishi wake kuhusu taratibu za uvunaji, usafirishaji na biashara ya mazao ya misitu nchini kupitia njia mbalimbali na kuhakikisha huduma bora kwa wananchi.

IMETOLEWA NA
KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO KWA UMMA
WAKALA WA HUDUMA ZA MISITU TANZANIA (TFS)
Share:

TETESI ZA SOKA JUMAPILI DEC, 30 2018

Christian Pulisic
Chelsea wametoa ofa ya hadi pauni milioni 45 kumsaini mshambuliaji wa Borussia Dortmund Christian Pulisic msimu ujao lakini klabu hiyo ya Ujerumani itacheleweza uamuzi wake inaposubiri ofa kutoka kwa vilabu vingine kwa mchezaji huyo raia wa Marekani mwenye miaka 20. (ESPN)

Meneja wa Newcastle Rafael Benitez anataka kumwendea straika wa Leeds Kemar Roofe, 25, ikiwa atapewa pesa mwezi Januari. (Sunday Mirror)

Meneja wa muda wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer amewashauri kipa wa Uhispania David de Gea, 28, na mshabuliaji Mfaransa Anthony Martial, 23, kusaini mikataba mipya na klabu hiyo. (Mail on Sunday)David de Gea
Chelsea wameambiwa kuwa ni lazma walipe pauni milioni 30 ikiwa wanataka beki mjerumani Mats Hummels, 30, mwezi Januari. (Sun on Sunday)

Meneja wa Juventus Massimiliano Allegri amekana madai kuwa anataka kuwa meneja mpya wa msimu ujao. (Mail on Sunday)

Meneja wa Watford Javi Gracia anasema sio jambo la kushangaza kuwa Abdoulaye Doucoure, 25 anahusishwa na kuhama licha ya yeye kutarajia raia huyo wa Ufransa kuendelea kubaki kwa muda zaidi. (Independent)Nathaniel Clyne
Cardiff wanaongoza mbio za kumwinda beki wa Liverpool Nathaniel Clyne, licha ya Fulham na Leicester nao kuwa na nia ya kumsaini kiungo huyo wa miaka 27 raia wa England. (Sunday Mirror)

Mlinzi wa Manchester United raia wa Italia Matteo Darmian, 29, analengwa na Inter Milan na Lazio. (Calciomercato)

Lazio watajia kuwasaini mlinzi wa Chelsea raia wa Italia Davide Zappacosta, 26 ikiwa Manchester United watakataa kumuuza Darmian. (Sunday Mirror)

Arsenal wamejiunga na mahasimu wao Tottenham kutaka kumsiani beki wa Norwich City mwennye miaka 18 Max Aarons. (Sunday Mirror)Davide Zappacosta

Liverpool wanammezea mate kiungo wa kati wa Trabzonspor Abdulkadir Omur, 19, lakini wanakabaliwa na ushindani kutoka Manchester City and Roma. (Fotomac, via Star on Sunday)

Meneja wa Southampton Ralph Hasenhuttl anataka kumiania beki wa Olympiakos na Norway Omar Elabdellaoui, 27, mwezi Januari. (Mail on Sunday)

Beki wa Leicester City raia wa Australia Callum Elder, 23, anajifunza na Ipswich Town na anatarajiwa kujiunga kwa mkopo mwezi Januari. (East Anglian Daily Times)
Share:

CCM WAANIKA SIFA ZA WAGOMBEA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA 2019

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema atakayejihusisha na vitendo vya rushwa katika mchakato wa chama hicho tawala kusaka wagombea wake katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, atapoteza sifa za kugombea.

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Desemba 30, 2018 alipokutana na wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya za Muleba na Biharamulo mkoani Kagera.

Amesema kila kiongozi wa CCM atakayejitokeza kugombea uenyekiti wa kijiji au mtaa, lazima awe mwadilifu na mwaminifu.

Amebainisha kuwa baadhi ya wagombea wanatumia majukwaa kupinga rushwa licha ya kuwa wanajihusisha nayo, ikiwa ni pamoja na kukiuka maadili ndani ya chama.


"Makatibu wa CCM kila ngazi hata nyie msiwe wa kupokea rushwa kupitisha majina ya wagombea wasiokuwa na sifa lazima kiongozi afuate miiko na ahadi za mwanachama,” amesema Bashiru.
Share:

VIGOGO WACHANGA FEDHA KUIPONGEZA YANGA,WAFUNGA MWAKA BILA KUFUNGWA

Baada ya kufanikiwa kuibuka na ushindi dhidi ya Mbeya City jumla ya mabao 2-1 hapo jana katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, wadau wa klabu ya Yanga wamechanga kiasi cha Sh. 960,000 kuwapongeza wachezaji kwa ushindi.

Mashabiki hao kutoka Wilaya ya Mbozi wakiongozwa na waziri wa kilimo Japhet Hasunga pamoja na mkuu wa mkoa wa Lindi Erasto Zambi wamechangia kiasi hicho cha pesa kama motisha kwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi kutokana na kushinda mchezo huo.

Wadau hao wachache waliamua kuchangishana fedha kutoka mifukoni mwao ambazo waliwagawia kiasi cha Sh 35,000 kila mchezaji na Sh 30,000 kwa kila mmoja katika benchi la ufundi la klabu hiyo kama shukurani zao kwa kuwafanya mashabiki wao kufunga mwaka kwa furaha.

Yanga inaongoza ligi mpaka sasa ikiwa na jumla ya pointi 50 baada ya kushuka dimbani michezo 18, ikimuacha mpinzani wake Azam FC aliye katika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi 10.

Pia imeweka rekodi ya kutopoteza mchezo wowote mpaka sasa, ikiwa imeshinda michezo 15 na kwenda sare michezo miwili, huku ikiondoka na ushindi mfululizo katika mechi zake saba za mwisho.
Share:

MBUNGE NACHINGWEA ALIA NA KASI NDOGO MALIPO YA KOROSHO

Na Bakari Chijumba, Mtwara Mbunge wa jimbo la Nachingwea Mkoani Lindi, Hassani Massala amefika mjini Mtwara ambapo ni kituo kikuu cha malipo kwa wakulima wote wa korosho kwa kipindi hiki, Lengo likiwa ni kufuatilia kuhusu Hoja za wakulima wa Korosho kwenye jimboni lake, kwa madai licha ya takwimu mbalimbali anazozipata lakini bado kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wakulima, hivyo kumlazimu kama mwakilishi afuatilie. Akizungumza na mtandao wa DarMpya hii Leo, katika eneo la uwanja wa ndege mjini Mtwara, Masala amesema kwenye jimbo lake la Nachingwea, bado kumekuwa na malalamiko kutoka…

Source

Share:

MABAKI YA MWILI WA MSTAAFU ALIYEPOTEA BAADA KUPOKEA MAFAO YAPATIKANA MAKABURINI



 Inawezekana likawa ni moja ya tukio la nadra kutokea nchini. Alison Mcharo aliyepotea mwaka 2006 imebainika kuwa aliuawa na kuzikwa katika makaburi ya familia yake.

Mcharo aliyekuwa mkazi wa Kijiji cha Mpinji, Kata ya Mamba Myamba wilayani Same, alipotea baada ya kupokea mafao yake ya kustaafu kazi ya ualimu.

Inadaiwa kuwa Mcharo alitoweka baada ya kufika nyumbani na hakuonekana tena.

Jana, Polisi Mkoa wa Kilimanjaro walisema kuwa wamewatia mbaroni mkewe, Nasemba Alison (80) na mtoto wake, Orgenes Alison (45) wakiwatuhumu kwa mauaji hayo.

Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Hamis Issah alisema mabaki ya mwili wa Mcharo yaligunduliwa Jumapili iliyopita, jirani na kaburi la baba yake mzazi.

Kamanda Issah alidai kuwa uchunguzi wa awali uliofanywa na polisi unaonyesha kuwapo kwa ushiriki wa mkewe katika kupanga na kutekeleza mauaji hayo kwa kile alichodai ni tamaa ya fedha.

Haikufahamika mara moja kiasi cha fedha ambacho marehemu alilipwa baada ya kustaafu.

“Uchunguzi wetu wa awali umebaini marehemu aliuawa baada ya kukabidhiwa mafao yake na waliohusika waliingia tamaa baada ya kuona fedha nyingi alizokuwa amekabidhiwa.

“Baada ya kupokea mafao yake na kurudi nyumbani, ndipo aliuawa lakini taarifa ikatolewa kuwa amepotea. Mkewe baada ya kuhojiwa amejieleza vizuri...,” alidai kamanda huyo.

Alisema ripoti ya kupotea kwake ilitolewa polisi mwaka 2006 na kipindi chote cha miaka 12, alitafutwa bila mafanikio hadi Jumapili iliyopita mabaki ya mwili wake yalipoonekana.

Mwili wake uligundulikaje?

Kugundulika kwa mabaki ya mtu anayedaiwa kuwa ni Mcharo kulianzia kwenye kifo cha mama yake mzazi ambaye alikuwa ameacha wosia kuwa azikwe jirani na alipozikwa mumewe.

Kamanda Issah alisema ndugu na jamaa walikwenda kuchimba kaburi eneo ambalo marehemu aliacha wosia, lakini walishtuka kukuta mabaki ya mwili wa mtu mwingine katika eneo hilo.

“Kulikuwa hakuna alama yoyote kama kuna kaburi, lakini cha ajabu walikuta mabaki ya mtu, hapo waliacha kuchimba kaburi na kutoa taarifa Polisi kwa sababu ukikuta kaburi huwezi kuendelea kuchimba.

“Baada ya polisi kupata taarifa hizo tuliomba kibali cha Mahakama na tulipochimba eneo lile, kweli yalionekana mabaki ya mwanadamu na kulionekana kuna tai na shati.

“Hizo nguo zilitambuliwa kuwa ni za mwalimu Mcharo ambaye alidaiwa kupotea na alikuwa hajulikani alipo tangu mwaka, 2006.

“Jambo lingine lililotushangaza tulipofukua kaburi, tulikuta mabaki yale yamekaa mkao ambao si wa maiti inavyozikwa. Ilikuwa kwenye mkao ambao si wenyewe kama taratibu za maziko zilivyo,” alidai Kamanda Issah.

Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi wa kisayansi ikiwamo kuchukua sampuli za mifupa ili kuthibitisha kisayansi kuwa ni ndiye.
Na  Florah Temba, Mwananchi 
Share:

MANAIBU WAZIRI BITEKO NA MAVUNDE WAWACHARUKIA WAZALISHA KOKOTO MKOANI DODOMA

Naibu Waziri wa Madini Mh Dotto Biteko na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana na Ajira Mh Anthony Mavunde  leo wametembelea kwa kushtukiza katika migodi ya machimbo ya kokoto katika eneo la Chigongwe Jiji la Dodoma ili kujionea shughuli za uchimbaji na usagaji mawe kufuatia agizo la Waziri Mkuu Mh Kassim Majaliwa Majaliwa la kutaka wazalishaji wa kokoto waliopata tenda ya kusambaza kokoto katika ujenzi wa mji wa serikali kuongeza kasi ya uzalishaji ili iendane sambamba na kasi ya ujenzi ambapo mahitaji ya kokoto yamekuwa makubwa sana. Baada ya…

Source

Share:

DKT.BASHIRU ALLY ATOA SIKU TATU KWA UONGOZI WA KCU, WAWE WAMEWALIPA WAKULIMA WA KAHAWA FEDHA ZAO.

  Na, Mwandishi wetu, Kagera. Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi taifa Dkt Bashiru Ally amewapa muda wa siku tatu viongozi wa chama kikuu cha ushirika KCU (T)199 LTD Mkoani Kagera, kuhakikisha kinawalipa wakulima wa zao la kahawa fedha za awali kabla hawajachukuliwa hatua. Dkt Bashiru Ally ametoa maagizo hayo wakati akizungumza na wajumbe wa halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi kwenye kikao utendaji kazi kilichowahusisha wajumbe kutoka halmashauri za Biharamulo na Muleba. Amesema kuwa wapo baadhi ya wakulima wanadai fedha zao tangu msimu uanze Mwezi Mei mwaka huu hadi…

Source

Share:

MTOTO AFICHWA KABATINI KWA MIEZI MITANO DODOMA

Katika hali isiyokuwa ya kawaida mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi mitano, jijini Dodoma amefungiwa kabatini na mwajiri wa mama mzazi wa mtoto huyo ambaye alikuwa akifanya kazi za ndani.

Akithibitisha kupokelewa kwa mtoto huyo katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt. Ibenzi amesema kuwa mtoto amefikishwa hospitali siku tatu zilizopita na kwamba atatibiwa kwanza tatizo la ukosefu wa lishe (utapiamlo).

Dkt. Ibenzi amesema kuwa mama wa mtoto huyo alifikishwa hospitalini hapo akiwa hajitambui kwa kile kilichodaiwa kupigwa na mwajiri wake hadi kupoteza fahamu.

"Mtoto anaendelea na matibabu kwakuwa bado tunamfanyia uchunguzi zaidi ikiwemo kufuatilia kama alipotiwa chanjo zote stahiki, na sisi tunatibu wagonjwa tu, mambo mengine watayafuatilia wahusika", amesema Dkt. Ibenzi.

Taarifa za awali zinadai kuwa binti huyo alipata ujauzito akiwa nyumbani kwa mwajiri wake anayedaiwa kuwa ni mwalimu wa shule ya msingi jijini humo ambaye alimtaka kufanya siri ili majirani wasifahamu kama yeye ni mjamzito.

Baadaye alifanikiwa kujifungua na kuendelea kufanya siri na mtoto kuhifadhiwa kabatini, hadi hapo juzi ambapo inadaiwa alimpiga binti huyo hadi kupoteza fahamu ndipo majirani walipofika eneo la tukio na kugundua kulikuwa na mtoto mchanga ndani ya kabati.
Chanzo:Eatv


Share:

OLE WAO WANAOHUJUMU MIUNDOMBINU YA UMEME – WAZIRI KALEMANI

  Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani jana (Desemba 29, 2018) amefanya ziara wilayani Kwimba, Mkoa wa Mwanza na kutoa onyo kali kwa watu wenye tabia ya kuhujumu miundombinu ya umeme pamoja na vishoka. Akizungumza kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Ngulla na Ibindo, akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme, kuwasha umeme na kuzungumza na wananchi; Waziri Kalemani alitahadharisha kuwa serikali haitamvumilia yeyote atakayebainika kufanya hayo. “Mtu atakayebainika akikata nguzo, akiiba nyaya, akichezea transfoma kiasi cha kukosesha umeme wananchi, Mkuu wa Wilaya wa eneo husika…

Source

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger