Na Hamida Kamchalla, TANGA.
BAADHI ya watu wenye ulemavu Mkoa wa Tanga wameshindwa kurejesha mikopo ya asilimia mbili inayotolewa na halmashauri kwa kukosa elimu juu ya ufanyaji biashara na ulipaji kodi.
Mwenyekiti wa Umoja wa Miradi kwa Viziwi Tanzania (UMIVITA) Ally Nassoro ameyasema hayo wakati wa mafunzo ya elimu ya mlipa kodi kwa watu wenye ulemavu yaliyotolewa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) Mkoa wa Tanga.
Amesema mikopo hiyo ni mzuri na inawasaidia sana katika kuendesha biashara zao na kujikwamua na umasikini, ambapo wengine wanafanikiwa kurejesha na baadhi kushinda huku wakiishia hata kuhama makazi yao.
"Wanaoshindwa kurejesha wanawanyima wenzao haki ya kupata mkopo, Sheria ya mkopo inasema kopa halafu rejesha, kwahiyo nikwambie wale wote ambao hawajalipa walipe ili wenzao wapqte" amesema.
Mwenyekiti huyo amebainisha kwamba elimu waliyopata itawanufaisha pakubwa kwani awali hawakuwa na uelewa kuhusu masuala mbalimbali yanayotokana na ulipaji wa kodi.
"Watu wenye ulemavu walikuwa hawaelewi kanuni au sheria zinavyosaidia katika kulipa kodi, lakini pia walikuwa na shida ya ulipaji wa kodi na vipengele wanavyotakiwa kuvitumia, hivyo tumefurahi kupata elimu hii kwasababu itatusaidia kufuatilia ulipaji wa kodi kama inavyotakiwa" amesema.
Naye Ofisa Mkuu Msimamizi wa Kodi kitengo cha Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano Tanga, Flavian Byabato amesema kwa kushirikiana na UMIVITA wamewiwa kuwapa elimu ya kodi watu wenye ulemavu ili kuwaongeze uelewa.
"Siku ya leo ikiwa ni muendelezo wa TRA kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari na kutoa elimu ya kodi kwa wadau wetu ili waelewe zaidi masuala mbalimbali yanayohusiana na kodi, lakini pia ni katika kuendeleza nchi yetu kupitia maendeleo,
"Na maendeleo yanafika kutokana na kulipa kodi, kwahiyo tukawiwa kushirikiana na chama hiki kutoa hii elimu ya kodi kwa manufaa yao lakini pia na serikali" amesema Byabato.
Byabato amesema elimu waliyotoa ni pamoja na usajili wa biashara, kulipa kodi stahiki sambamba na hayo wamewajulisha haki ambazo wanazo katika masuala mbalimbali ya kodi ikiwemo kupewa taarifa na elimu ya kodi.
"Lakini wana haki ya kupewa hati safi ya ulipaji kodi baada ya kukamilisha taratibu mbalimbali ikiwemo matumizi sahihi ya mashine za kielektroniki (EFD) na utoaji wa risiti,
"Tunashkuru kwamba wameitikia vema na tunategemea kuwa huu ni mwanzo wa hatua ya kukamilisha wajibu wao, tunategemea watakuwa walipaji waziri wa kodi na kuweza kueneza hii elimu ambayo wameipata" amesema.
Kwa upande wake Katibu wa Shirikisho la watu wenye ulemavu Mkoa wa Tanga (SHIVIAWATA) Subira Hoza amesema kabla ya kupata elimu hiyo watu wenye ualbino Mkoa walikuwa wanafahamu kuhusu elimu ya mlipa kodi kwa asilimia 30.
"Lakini leo tumejifunza mambo mengi sana, hasa kuhusu ulipaji kodi kwa mtu mwenye kupata kiwango cha juu na chini, lakini pia kuhusu misamaha ya kodi, kwamba wapi wanapaswa kusamehewa na wapi walipe" ,amebainisha.
0 comments:
Post a Comment