Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Tanzania ikiwa inaadhimisha miaka 63 ya Uhuru wake,Katibu wa siasa na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma Jawadu Mohamed amewataka wananchi kuendelea kuwa na umoja na mshikamano katika kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kuhakikisha kuwa taifa linaendelea kupiga hatua kubwa katika nyanja zote za kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Aidha ameeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 63 ya Uhuru kuwa ni pamoja na kuondoa ujinga, maradhi na umasikini vitu vilivyokuwa kama adui wa maendeleo nchini.
Hayo yameelezwa leo December 9,2024 Jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Tanganyika ambapo amesema kuwa chama cha Mapinduzi kimefanikiwa kuleta mabadiliko makubwa na ya kudumu kwa wananchi wake na kwamba mafanikio haya ni matokeo ya juhudi za pamoja kati ya chama hicho na wananchi.
Ameeleza kuwa hatua muhimu zimepigwa katika kuboresha huduma za afya, elimu, na kubuni fursa za kiuchumi kwa wananchi na kwamba Serikali imekuwa ikianzisha sera na miradi mingi ya kijamii ambayo imewezesha kupunguza umasikini na kuboresha maisha ya wananchi, hasa katika maeneo ya vijijini.
Katibu Mwenezi huyo ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka 63 ya uhuru, Serikali imefanikiwa kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa ya milipuko, kama vile malaria, kipindupindu na mengineyo ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya afya, kwa kujenga zahanati na vituo vya afya kila pembe ya nchi, na kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote, hasa wale wa vijijini.
Kwa upande wa sekta ya elimu, Katibu Mwenezi huyo ameleza kuwa Tanzania imefanikiwa kutoa elimu bure kwa watoto wote, ambapo karibu kila mtoto nchini anapata elimu ya msingi na sekondari.
"Ndani ya miaka hii 63 ya Uhuru tumeshuhudia mapinduzi makubwa kwenye sekta ya elimu,Serikali imejenga shule mpya, kuajiri walimu wengi, na kuongeza rasilimali za elimu ili kuhakikisha kuwa kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu bora,
“Leo hii, tunajivunia kuwa na idadi kubwa ya wahitimu wa vyuo vikuu, wataalamu wa sayansi na teknolojia, na wataalamu wa afya, ambao wanachangia katika maendeleo ya taifa letu,” anafafanua
Ameleza kuwa kupambana na umasikini ni moja ya changamoto kubwa zilizokabiliana na taifa tangu kupata uhuru.
Hata hivyo, amesema kuwa juhudi za serikali katika kuboresha kilimo, viwanda, na miundombinu zimeleta matokeo chanya kwa wananchi.
"Kwa mfano, serikali imeimarisha mifumo ya kilimo cha kisasa na mikopo kwa wakulima, ikiwemo kuanzisha miradi ya maji na barabara, ili kuboresha maisha ya watu katika vijiji na miji midogo. Matokeo ya jitihada hizi ni ongezeko la uzalishaji wa chakula na bidhaa nyingine za kilimo, na hivyo kutoa fursa nyingi za ajira na kuongeza pato la taifa, "amesisitiza.
Hata hivyo amesema licha ya mafanikio hayo, bado kuna changamoto zinazokabiliana na nchi, lakini amesisitiza kuwa Serikali kupitia Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kushirikiana na Serikali kuhakikisha kuwa Tanzania inafikia malengo yake ya kuwa na uchumi wa kati na wa viwanda, huku wananchi wakinufaika na mafanikio hayo.
"Maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru ni nafasi nzuri ya kutafakari na kujivunia kile kilichopatikana,tunapaswa kuangalia mbele na kufanya kazi kwa juhudi ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu, huu ni wakati wa kujivunia mafanikio yetu, lakini pia ni wakati wa kuendelea kujitahidi kufikia malengo makubwa zaidi kwa ajili ya taifa letu na vizazi vijavyo,” amesema
0 comments:
Post a Comment