Friday, 1 October 2021

Waliovamia Eneo La Farm Chamwino Ikulu Wapewa Wiki Mbili Kuondoka

...


 Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Serikali imeagiza wananchi waliovamia eneo la Farm katika kijiji cha Chamwino Ikulu mkoani Dodoma kuondoka katika kipindi cha wiki mbili kuanzia Oktoba 2, 2021 kwa kuwa   kijiji hicho kilishatangazwa eneo la mpango mwaka 1992 kupitia GN Na 263 ya tarehe 25 Juni 1992 ili kuepusha sheria ya ardhi ya vijiji (Sura 114 Toleo la 2002) kutumika.

Agizo hilo limetolewa leo Oktoba 1, 2021 na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Gift Msuya wakati wa kutangaza maamuzi ya timu ya uchunguzi wa mgogoro wa eneo la Farm mbele ya wananchi wa kijiji cha Chamwino mkoani Dodoma.

"Natoa tamko la serikali kwa niaba ya kamati ya ulinzi ya wilaya na wananchi wa kijiji cha Chamwino naagiza wanaokalia maeneo ndani ya eneo la Farm kuondoka ndani ya wiki mbili na watakaokaidi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao" alisema Gift Msuya.

Sehemu ya eneo la shamba la Farm lenye ukubwa  wa ekari 640 lililoanzishwa kati ya mwaka 1971/1972 na Hayati baba wa Taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere kwa lengo la kuwafunza wanakijiji cha Chamwino ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa maziwa, mbuzi, kondoo, nguruwe na kuku lilivamiwa na kuzua mgogoro kati ya wananchi na serikali.

Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya ya Chamwino, mwananchi yeyote aliyeingia ndani ya eneo hilo ni marufuku kufanya shughuli yoyote kama vile ujenzi, kilimo na serikali kupitia idara ya ardhi itaweka mabango katika eneo hilo kuonesha kuwa eneo hilo ni eneo la umma.

‘’Wanaoendelea kufanya ujenzi watakuwa wanajiingiza hasara na wananchi mwenye yeyote mwenye nyaraka za kumilikishwa sehemu ya eneo hilo la Farm afike ofisi ya mkuu wa wilaya na atapatiwa haki yake’’. Alisema Gift Msuya

Kwa upande wake Kamishna wa ardhi nchini Nathaniel Nhonge alisema, kumbukumbu katika eneo hilo zimeweka bayana kuwa, eneo lenye mgogoro la Farm lilitolewa kwa matumizi ya umma na hakuna mabadiliko yaliyofanyika kwenda kwa mtu mmoja mmoja.

"Kimsingi hakuna mtu aliyelipwa fidia ndani ya eneo la Farm na wale wananchi waliolipwa kimakosa wanatakiwa warejeshe fedha". Alisema Nhonge

Alisema, baada ya ripoti ya tume ya uchunguzi kuhusiana na mgogoro huo sasa upimaji utafanyika eneo lililotolewa kwa matumizi ya taasisi za shule ya sekondari Chamwino, Shule ya Msingi Kikwete pamoja na eneo la Mahakama na kuyamilikisha kwa wahusika kuepuka migogoro hapo baadaye.

"Serikali itaweka utaratibu wa kudumu wa kubaini na kulinda maeneo mengine ya aina hii yaliyoko ndani ya Chamwino dhidi ya uvamizi wa wananchi". alisema Kamishna Nhonge.

Hata  hivyo,  baadhi ya wananchi wa kijiji cha Chamwino wameonesha kutoridhishwa na maamuzu hayo kwa kueleza kuwa maeneo hayo walirithi na kuridhiwa na serikali ya kijiji kwa nyakati tofauti ingawa hawakuwa na nyaraka zozote zinazoonesha kumilikishwa maeneo hayo.

Eneo la Farm katika kijiji cha Chamwino mkoani Dodoma limekuwa kwenye mgogoro wa muda mrefu uliosababisha kuundwa kwa timu maalum ya kushughulikia mgogoro huo.

Wakati wa kushughulikia mgogoro timu ya uchunguzi ilielezwa kuwa, shamba la Farm lilitolewa kwa serikali ya kijiji miaka ya 1971/1972 kwa matumizi ya mradi wa mifugo na baada ya mradi kufa mwaka 1995 baadhi ya wananchi waliokuwa eneo hilo kabla ya Farm kuanzishwa walirudi kwenye eneo hilo na wengine waliomba serikali ya kijiji kwa ajili ya kulima shamba hilo kwa muda.

Hata hivyo, Serikali ya kijiji cha Chamwino ilitoa sehemu ya eneo hilo kujengwa shule ya Sekondari ya Chanwino mwaka 1995 na sehemu ya shamba hilo lililotolewa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi Kikwete 2007.

Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Kijiji Na 4/1999 kifungu cha 13 (7) inaeleza kuwa ardhi iliyotengwa na halmashauri ya kijiji au mkutano wa kijiji kwa matumizi ya jumuiya/umma au ardhi ambayo wenyeji wa eneo husika wanaitumia kama ardhi ya kijiji ya umma kabla ya kutungwa kwa sheria ya ardhi, ardhi hiyo ni ya ardhi ya kijiji. Pia sheria ya ardhi ya mwaka 1999 kifungu cha 12 (1) inakataza ardhi ya jumla kutolewa kwa mtu binafsi.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger