Balozi wa Kenya katika Umoja wa Mataifa amesema, katika kipindi cha urais wa mwezi mmoja wa nchi hiyo kwenye Baraza la Usalama la umoja huo mnamo mwezi huu wa Oktoba, itaitishwa mikutano minne ya ngazi ya juu ambapo miwili itahutubiwa na Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo na mingine miwili itakuwa ni ya ngazi ya mawaziri itakayohutubiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa taifa hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya kwenye Umoja huo Balozi Martin Kimani amesema, Rais Uhuru ataongoza mijadala ya ngazi ya juu kuhusu ujenzi na uendelezaji wa amani pamoja na hali ya mambo katika Ukanda wa Maziwa Makuu.
Kwa upande wake Balozi Omamo ataongoza mijadala kuhusu Wanawake, amani na usalama pamoja na Mashariki ya Kati.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, ambaye naye pia alishiriki katika mkutano huo na waandishi wa habari ametoa msimamo wa nchi yake kuhusu wakimbizi raia wa Somalia iliowapatia hifadhi na kueleza kwamba, “kambi za wakimbizi hazipaswi kuwa ndio suala la kudumu. Kwa mtazamo wetu wa haki za binadamu, ni ukiukwaji mkubwa wa haki kuwaweka watu katika mazingira tata kwenye kambi maisha yao yote.”
Mwezi Aprili mwaka huu wa 2021, Kenya ilitangaza kuwa itafunga kambi za Daadab na Kakuma ifikapo mwezi Juni mwaka 2022, hatua ambayo ilifuatiwa na mazungumzo kati ya serikali ya nchi hiyo na Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR Fillipo Grandi ambapo pande hizo mbili zilikubaliana kuwa kambi si suluhisho la kudumu na zinafanyia kazi mpango wa kusaidia wakimbizi kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa wakimbizi, Global Compact on Refugees.
Kenya imeanza uanachama wake kwenye Baraza la Usalama tarehe Mosi mwezi Januari mwaka huu, uanachama utakaodumu kwa miaka miwili. Hata hivyo urais wa Baraza ni kwa mwezi mmoja miongoni mwa nchi 15 wanachama wa Baraza hilo la Usalama.
Credit:Parstoday
0 comments:
Post a Comment