MWANAUME mmoja nchini Kenya, Stephen Nyangeri Mauti mwenye umri wa miaka 25, ameshtakiwa kwa tuhuma za kumuua mkewe Faith Nyatich ambaye alimuoa Agosti, mwaka huu alipomtusi kwamba hajiwezi chumbani.
Baada ya miezi miwili tayari ndoa yao ilikuwa imegeuka kuwa chungu ndipo Faith akatoroka kwenda eneo la Kiserian, kaunti ya Kajiado na kuishi na mwanaume mwingine.
Mbele ya Hakimu mwandamizi Bernard Ochoi, wakili wa upande wa mashtaka James Gachoka aliieleza Mahakama kuwa, ili kumfanya arudi nyumbani, Nyangeri alimpigia Faith (marehemu) simu na kumsihi arudi nyumbani kwa vile alikuwa hajisikii vizuri.
Aliporudi, Faith alimkuta mumewe katika makazi yao mtaani Kangemi, alimpikia maakuli ya mchana siku hiyo.
Baada ya kupiga stori, wawili hao walitoka kwenda kutembea katika soko la Kangemi kununua vyakula na bidhaa nyinginezo kisha alirejea katika makazi yao.
Faith alipika chakula cha jioni, walikula kisha wakakesha pamoja, asubuhi ya Oktoba 3, 2021, Faith aliandaa kifungua kinywa, walipokuwa wanachangamkia brekifasti wawili walijadiliana mambo mbali mbali.
Ni wakati huo, Nyangeri, alimsihi mkewe Faith, asitoroke tena kuishi na mwanaume mwingine kama alivyokua amefanya hapo awali.
Faith alimfokea na kumkejeli Nyangeri na kumtusi, “wewe hujiwezi kitandani. Wewe ni bwege tu ndio maana nilikutoroka.”
Hasira ilimpanda Nyangeri na mara moja akanyanyuka kutoka kwenye kiti alichokalia kisha kumkaba koo Faith. Faith alipiga kelele lakini mumewe alimfunika mdomo kwa kiganja cha mkono wake wa kulia. Faith alinyamaza na kulegea.
Mshtakiwa alidhani Faith amenyamaza lakini akaona ameanza kufifia.
Aliwaita majirani kumsaidia kumpeleka hospitali. “Madaktari katika zahanati ya Kangemi walimweleza Nyangeri mkewe amekata kamba tayari,” mahakama imeelezwa.
Watu waliokuwa wamemsaidia Nyangeri kumpeleka Faith hospitali ndiyo walimshikilia kisha wakaita polisi ambao walimkamata.
Hakimu Ochoi aliamuru mshtakiwa apelekwe katika hospitali ya kumfanyia uchunguzi wa afya ya akili kabla ya hukumu kupitishwa ambapo mshtakiwa atarudishwa kortini Novemba 22, 2021.
0 comments:
Post a Comment