Sunday 23 February 2020

UINGEREZA YAPIGA MARUFUKU UHUSIANO WA MAPENZI KATI YA WAFANYAKAZI NA WANAFUNZI

...
Chuo Kikuu cha London chaanzisha sera ya kupiga marufuku uhusiano wa mapenzi chuoni

Marufuku ya kuwa na uhusiano wa mapenzi kati ya wafanyakazi na wanafunzi katika Chuo Kikuu cha London ni mwamko mpya kwa vyuo vikuu, wachambuzi wamesema.

Makundi ya wanafunzi yamesema kwamba ni imani yao kuwa sera sawia na hiyo zitaanza kutekelezwa na vyuo vingine.

Chuo Kikuu cha London kinaaminika kuwa cha tatu nchini Uingereza kuanzisha marufuku hiyo.

Inasemekana kwamba sera hiyo inalenga kuzuia unyanyasaji kwa walio na madaraka na vitendo vya ngono.

Kelsey Paske, maneja wa kitengo kinachoangazia tabia ya utamaduni, amesema sera hiyo pia inalenga kutatua migogoro ambayo huenda ikazuka kutokana na mahusiano "huenda yakawa na athari mbaya katika mazingira ya kwenye taasisi za masomo".

Sera mpya ya mahusiano katika Chuo Kikuu cha London kwa wafanyakazi, kulingana na gazeti la the Guardian, inakataa "mahusiano ya karibu na ya mapenzi kati ya wafanyakazi na wanafunzi pale ambapo kuna usimamizi wa moja kwa moja".

Uhusiano wa mapenzi kati ya mfanyakazi na mwanafunzi ambaye hamsimamii kimasomo moja kwa moja ni lazima uwekwe wazi na mfanyakazi.

Sera hiyo pia inakataza mahusiano ya mapenzi na wafanyakazi au wanafunzi wenye umri wa chini ya miaka 18 au watu wazima ambao wako katika hatari mfano, yule ambaye atahitaji usaidizi maalumu kwasababu ya ulemavu.

Kukiuka sera hiyo kutachunguzwa na kitengo cha kukabiliana na utovu wa nidhamu chuoni, ambao ni pamoja na uwezekano wa kuchukuliwa kwa hatua kuanzia kupewa onyo rasmi hadi kufutwa kazi au kufukuzwa chuoni.

Dr Anna Bull, wa shirika moja linalopinga vitendo dhidi ya tabia zinazoendeleza ngono katika taassi za shule za juu, amesema kwamba shirika lake linaunga mkono kikamilifu sera hiyo mpya na ni matumaini yao kwamba vyuo vingine vikuu vitafuata mkondo huo.

Alisema kuwa sera hiyo ni moja ya sheria kali Uingereza ambayo pia inatekelezwa na vyuo vikuu vingine viwili vya Greenwich na Roehampton.

Dr Bull ameongeza kuwa vyuo vingi vina sera ambazo zinakemea vikali uhusiano wa mapenzi kati ya wahadhiri na wanafunzi lakini sheria kama hiyo bado huenda ikatoa mwanya kwa wafanyakazi wanaotaka kuwa na uhusiano na wanafunzi ambapo wafanyakazi wanaweza kuitisha vikao nje ya jengo la chuo au hata kuzungumza na mwanafunzi kwa namna inayoashiria kuwa anatafuta uhusiano wa mapenzi.

"Tunaona kwamba huu ni mwito kwa sekta hii kuanza kuwajibika kwa kuhakikisha wanafunzi wanalindwa dhidi ya wahadhiri kutumia vibaya madaraka yao," amesema.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger