Sunday 23 February 2020

Katibu Wa UVCMM Kata ya Hananasifu Ahukumiwa Miaka Mitatu Jela Baada ya Kugundulika Sio Raia wa Tanzania

...
Katibu wa Umoja wa Vijana CCM Kata ya Hananasifu, Mohamed Nyandu amehukumiwa kulipa faini ya Sh1.5 milioni au kwenda jela miaka mitatu baada ya kukutwa na hatia ya kuishi nchini bila kibali.

Nyandu ambaye imeelezwa kuwa ni raia wa Burundi alikiri kutenda kosa hilo la kuishi nchini kinyume na sheria ya uhamiaji na kutoa taarifa za uongo zikihusisha urai wake.

Hakimu Mwandamizi wa mahakama ya Kinondoni Vicky Mwaikambo amesema kutokana na mshtakiwa huyo kukiri mashtaka yote matatu yanayomkabili hivyo mahakama hiyo imemtia hatiani na kumtaka kulipa faini ya Sh500,000 kila kosa au kwenda jela miaka mitatu na akitoka jela arudishwe nchini Burundi.

Akisomewa hati ya mashtaka na Wakili wa Serikali Idara ya Uhamiaji, Godfrey Ngwijo amedai kuwa tarehe, mwezi na mwaka usiojulikana mshtakiwa huyo ameingia nchini kwa kutumia njia zisizo halali na alikamatwa Januari 20, 2020 na maofisa wa uhamiaji wa wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Amedai kuwa Januari 20, 2020 katika ofisi za uhamiaji wilaya ya Kinondoni mshtakiwa huyo alikamatwa kwa kosa la kuishi nchini isivyo halali wakati akijua yeye ni raia wa Burundi.

Katika shitaka la tatu mshtakiwa huyo alitoa tarifa za uongo zikihusisha uraia wake kwa maofisa wa uhamiaji ili kujipatia kitambulisho cha Taifa cha Tanzania (Nida) wakati akijua yeye si raia wa Tanzania.

Baada ya kumtia hatiani, wakili wa Serikali alidai kuwa hawana rekodi ya makosa ya nyuma hivyo mshitakiwa anavyoonekana amejihusisha na siasa kwa muda mrefu lengo lake ni kitu gani ukizingatia uhalisia wa nchi aliyotoka katika mambo ya usalama.

“Hivyo naiomba mahakama hii impe adhabu kali kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo,”alidai Shija.

Hata hivyo baada ya Hakimu Mwaikambo kumuhukumu kulipa faini ya Sh1.5 milioni lakini mshtakiwa huyo alishindwa kulipa faini hivyo ameenda gerezani kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela. Atarudishwa Burundi baada ya kumaliza kifungo.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger