Thursday, 2 January 2020

Upande wa Jamhuri wakataa Kabendera kumzika Mama yake...Mahakama Kuamua

...
Upande wa Serikali umempa pole Mwandishi wa Habari, Erick Kabendera kwa kufiwa na Mama yake mzazi, Verdiana Mujwahuzi huku ukipinga maombi yake ya kutaka ashiriki Ibada ya mazishi ya mama yake.

Hayo yamebainika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati Kabendera anayekabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha alipofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kesi yake.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amemueleza Hakimu Mkazi, Janeth Mtega kwamba Jamhuri inampa pole Kabendera kwa kufiwa na Mama yake mzazi.

“Hata sisi tuna masikitiko makubwa na tunampa pole nyingi Kabendera kwa kufiwa na Mama yake mzazi, lakini mahakama isifungwe mikono kwa maombi yaliyowasilishwa ya kutaka kushiriki msiba,”amesema Wankyo.

Wankyo amedai kuwa maombi ya Kabendera kupitia mawakili wake yamewasilishwa wakati ambao si sahihi kwa sababu mahakama haina mamlaka na pia Mkurugenzi wa Mashitaka hajaipa kibali ya kusikiliza kesi hiyo.

“Katika macho ya kisheria mahakama yako haina mamlaka, hata sisi tuna masikitiko makubwa lakini mahakama isifungwe mikono,” amesema.

Kuhusu mwenendo wa kesi, upelelezi unaendelea na shauri limefika hatua nzuri ya maelewano baina ya mshitakiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka (DPP).

Kukataliwa kwa Kabendera kushiriki mazishi ya Mama yake, kumeibuka kutokana na maombi aliyoyatoa Kabendera kupitia Mawakili wake akiwemo Jebra Kambole.

Wakili Kambole amedai wanaiomba mahakama hiyo imruhusu Kabendera akashiriki Ibada ya Mazishi ya Mama yake mzazi katika Kanisa la Roman Katoliki lilipo Changombe majira ya mchana.

Kambole ameieleza mahakama kuwa suala la kushiriki sala ya mwisho ya msiba ni haki ya Binadamu, suala la faragha.

“Kushindwa kuudhuria maziko ya Mama yake tutakuwa tumemuadhibu adhabu kubwa tena kwa kuangalia uhusiano wa mshitakiwa na mama yake mzazi kwani alikuwa akimuuguza na ni vizuri akatoa heshima ya mwisho,”ameeleza.

Wakili Jebra amedai kuwa ni muhimu kwa Kabendera kushiriki kwa sababu Mama mzazi ni mmoja, akifa anaagwa mara moja.

“Jamhuri haitaathirika kwa lolote kwa sababu mshitakiwa atakuwa chini ya ulinzi na ibada itakuwa mchana kanisani na Temeke sio mbali na gerezani, tunaomba akatoe heshima ya mwisho,” ameomba.

Baada ya kutoa hoja hizo, Hakimu Mtega ameahirisha kesi hiyo hadi saa 8:45 mchana kwa ajili ya kutoa uamuzi kama Kabendera ashiriki Ibada ya mazishi ya Mama yake mzazi ama lah.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger