Sunday, 26 January 2020

RAS Tabora Awataka Maofisa Tarafa Kuhakikisha Kero Za Wananchi Zinatatuliwa Katika Maeneo Wanayosihi

...
SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imewataka Maofisa Tarafa kutatua kero na migogoro inayowakabili wananchi katika maeneo yao badala ya kuwaacha bila usaidizi na kuwafanya kukimbilia kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kutafuta haki zao.

Kauli hiyo imetolewa  na Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu alipokuwa na Kikao kazi cha siku moja na Maofisa Tarafa wa Tarafa zote za wilaya zote za Mkoa huo.

Alisema ni jukumu la Maofisa hao kuhakikisha wanashughulikia migogoro ya ardhi, kuondoa madai ya wananchi kuombwa rushwa, mauaji na matumizi mabaya ya madaraka inayofanywa na Watendaji walioko chini yao ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma nzuri na wanayotarajia.

Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Tabora alisema ni vema wakasimama vema katika nafasi zao za uongozi ili kuwaondolea adha ya kusafiri umbali mrefu kutoka wanapoishi hadi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kutafuta haki zao.

“Sifurahishwi kuona wananchi wengine ni wazee sana wameshindwa kusaidia kule wanapoishi na kuamua kuja katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kumuona Mkuu wa Mkoa au mimi ili niwasikilize kero zao ambazo kimsingi zilitakiwa kutatuliwa na viongozi walio karibu nao ambao wengine wao ni ninyi Maofisa Tarafa ” alisema.

Makungu alisema kuwa Maofisa Tarafa ndio kiungo kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa ni vema wakahakikisha kuwa shughuli zote zinazofanyika katika maeneo yao ya utawala yanazingatia Sheria za Nchi na zinatolewa kwa haki kwa wananchi wote.

Aidha Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Tabora amewataka Maofisa Tarafa kuhakikisha mapato ya Serikali yanakusanywa na kudhibiti Wafanyabiashara wanaokwepa kodi za Serikali.

Alisema kuna baadhi ya wafanyabiashara bado wanaendesha shughuli bila kulipa kodi zinazotakiwa kwa mujibu wa Sheria.

Mwisho


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger