Wednesday 21 December 2016

RAIS MAGUFULI AKATAA SHULE ISIITWE JINA AKE

...


Rais John Magufuli amekataa shule ya msingi iliyojengwa hivi karibuni eneo la Bunju, Wilaya ya Kinondoni kuitwa kwa jina lake badala yake ameagiza iitwe kwa jina la Mkuu wa wilaya hiyo, Ally Hapi. 
Taarifa ya badiliko la jina haikutolewa na Idara ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu kama ilivyozoeleka bali na mkuu wa wilaya hiyo wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa mbalimbali vya usafi kwa uongozi wa shule hiyo. 
“Shule hii imejengwa kwa fedha zilizopatikana baada ya Serikali Kuu kubana matumizi. Tukaamua iitwe John Magufuli lakini yeye akatoa agizo shule ipewe jina la mkuu wa wilaya sina budi kukubaliana na hilo,” alisema Hapi. 
Shule hiyo mpya iliyopo Bunju jijini imejengwa kwa lengo la kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Msingi Bunju A ambayo ilikuwa na wanafunzi 3,224.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo mpya, Ali Mwakapalila alisema ingawa inatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi Januari 9 mwakani inakabiliwa na changamoto mbalimbali. 
“Hakuna umeme wala maji, hii inaweza kuleta madhara kwa wanafunzi hasa linapokuja suala la matumizi ya vyoo,” alisema. 
Baada ya hafla hiyo, Hapi alikwenda kwenye kiwanda cha saruji cha Twiga Cement ambako alipokea msaada wa mifuko 600 ya saruji kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa madarasa na majengo mengine. 
Akipokea msaada huo, Hapi alisema msaada kutoka Twiga Cement unaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoipa sekta ya elimu kipaumbele ili kuhakikisha inatolewa katika mazingira bora. 
“Msaada huu umekuja muda muafaka. Tumeshajenga shule ila tunataka kuongeza madarasa, maabara, ofisi ya elimu na kuzungushia uzio ili watoto wawe katika mazingira salama. Lengo ni kuifanya shule hii iwe ya kisasa na itakuwa mfano kwa shule zote za Wilaya ya Kinondoni,” alieleza. 
Pia, Hapi alisema wilaya hiyo ipo kwenye mipango ya kujenga maktaba ya kisasa kwa kushirikiana na kampuni hiyo ya saruji. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Twiga Cement, Alfonso Velez alisema kuchangia katika shughuli za kijamii ni moja ya mambo ambayo wamekuwa wakiyapa kipaumbele zaidi. 
“Kushiriki shughuli za maendeleo katika jamii ni jambo ambalo tunalipenda zaidi. Yalipo maendeleo Twiga Cement ipo pia,” alisema Velez.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger