Thursday 29 December 2016

Mapya Yaibuka Sakata la Kijana Aliyefariki Baada ya Nyoka wake Kuuawa na Wananchi

...

Tukio  la kushangaza lililohusishwa na kifo cha Denis Komba (24) baada ya nyoka aliyekuwa naye kuuawa, limechukua sura mpya baada ya mambo kadhaa kuibuka.

Hayo ni pamoja na familia kudai mzoga wa nyoka na kwenda nao kuuzika nyumbani, jambo lililoendelea kuhusisha suala hilo na imani za kishirikina.

Imeelezwa kuwa familia ilielezwa na mganga wa kienyeji kuwa mwili uliohifadhiwa hospitali, si wa mtoto wao, jambo lililowafanya kuuchukua mzoga wa nyoka na kwenda kuuweka katika mfuko wa sarandusi (kiroba) na kuuzika.

Hata hivyo, mashuhuda walieleza kuwa, familia hiyo ilikikata kichwa cha nyoka na kukizika kivyake na kiwiliwili sehemu nyingine huku mwili wa Komba ambaye naye alizikwa jana, ukizikwa katika kaburi eneo lingine tofauti. Tukio hilo ni la juzi na lilimhusu Komba, mkazi wa Mateka, manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Nyumbani kwao ni kilometa tano kutoka katikati ya mji wa Songea. Kabla ya maziko, baadhi ya vijana waliokuwa wamebeba jeneza, walikuwa wakikimbia nalo mwendo wa mchakamchaka huku wakiimba “mkimbize mkimbize nyoka awahi asije kudhuru watu wengine”.

Katika maziko hayo, hakuna ndugu aliyeonekana kulia wala hakukuwa na ibada yoyote wakati jina la marehemu linadhihirisha kuwa ni wa imani ya Kikristo. 
Wakati hayo yakiendelea msibani, baadhi ya watu wake wa karibu walidai alikuwa na tabia ya kucheza na nyoka mara kwa mara.

Hata hivyo, baba mzazi alikana kumuona mwanawe na nyoka. Naye daktari aliyechunguza mwili, alisema kifo cha Komba kinatokana na kugongwa na nyoka mwenye sumu kali, lakini hakuna jeraha wala alama yoyote iliyoonekana katika mwili huo.

Habari zinaeleza kuwa juzi familia ilikwenda kuzungumza na watu wa Idara ya Maliasili, waliochukua mzoga wa nyoka kwa uchunguzi kama nyara ya serikali. Walikubaliana kuwa familia itakwenda kuufukia na ndipo Maliasili walimrudisha nyoka hadi eneo la tukio na familia kumchukua.

Ilielezwa kuwa hatua hiyo, inatokana na madai kuwa kuna mganga amehusisha mzoga wa nyoka huyo na mwili wa Komba.

Watu wa karibu wa familia hiyo, ambao hawakutaka kutaja majina yao wakiwemo mafundi seremala na majirani, walieleza kuwa familia wakiongozwa na baba mzazi Sevelin Komba, walirudi eneo la tukio baada ya kutoka kwa mganga wa kienyeji na kumchukua nyoka na kumpeleka nyumbani.

Habari zinaeleza kuwa familia baada ya tukio hilo, walikwenda kwa mtaalamu wa mambo ya asili (mganga wa kienyeji) ambaye hakufahamika mara moja na kuelezwa kwa nini wamekubali kumuacha mtoto wao akiteseka juani kwani mwili walioupeleka nyumbani kutoka hospitali si wa Denis (Komba).

Aidha familia baada ya kumchukua nyoka huyo eneo la tukio alikouawa, baada ya kufikishwa nyumbani alikatwa kichwa kwa makubaliano ya familia ya marehemu na kiwiliwili kuzikwa tofauti na kichwa katika mfuko wa sarandusi. Baba mzazi alikanusha suala hilo la kwenda kwa mganga.

Katika maziko hayo, hakukuwa na chakula wala matanga na watu wengi walijitokeza ili kushuhudia kitakachoendelea.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger