Tuesday 20 December 2016

Wahitimu udaktari kupelekwa vituo vya afya

...

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema inakusudia kuwasilisha muswada wa sheria bungeni mwakani, itakayowalazimisha wahitimu wa udaktari kupangiwa kwenye kituo chochote cha afya na Serikali, ambako watafanya kazi katika kipindi kisichopungua miaka miwili.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk Hamis Kigwangalla huenda muswada huo, ukawasilishwa rasmi katika Bunge la Februari mwakani.
Dk Kigwangalla aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya sekta ya afya katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wa serikali ya awamu ya tano na mikakati ya kuboresha zaidi sekta hiyo katika miaka ijayo.
Alisema endapo sheria hiyo mpya itapitishwa na bunge hilo, inakusudia kubadili muundo mzima wa watumishi wa sekta ya afya.
“Sheria hii, itaweka kipindi cha lazima cha national service (utumishi wa umma) na kila daktari anayehitimu kwa sababu amesomeshwa na kodi za watanzania, atalazimika kupangiwa kwenye kituo chochote cha serikali ambako atafanya kazi kwa kipindi kisichopungua miaka miwili kwa lazima”.
Naibu waziri huyo, alisema katika mipango na matarajio ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa 2017, pia wanatarajia kutunga sheria ya kuhakikisha kila mtanzania anakuwa na bima ya afya ya lazima.
Alisema katika kutekeleza azma hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja, serikali imefanikiwa kuwakatia bima wazee wote waliopo nchini wanaokadiriwa kufikia takribani milioni mbili na nusu.
“Bado utaratibu huu wa kuwakatia bima unaendelea katika halmashauri zingine, lakini tunakoelekea tunaweka sheria ili jambo hili lisiwe tu ni agizo la serikali bali litambulike na kutekelezwa kisheria,” alisisitiza Dk Kigwangalla.
Alisema katika sheria hiyo mpya kutakuwa na kifungu cha sheria kitakachobainisha makundi yote yanayotakiwa kukatiwa bima kwa usimamizi wa halmashauri zao.
Aidha Dk Kigwangalla alisema pia wizara hiyo ina mpango wa kuhakikisha inarasimisha suala la matibabu bure kwa makundi maalumu kwa kulitambua kisheria, ili liweze kutekelezwa na kuwafikia walengwa.
Alisema kwa mujibu wa sera ya afya ya taifa, wazee wote wenye miaka zaidi ya 60, watoto wenye umri chini ya miaka mitano pamoja na watu wenye magonjwa sugu kama vile saratani, shinikizo la damu, sukari na pumu wanapaswa kupata huduma bure.
“Jambo hili lipo na linatambulika kisera, lakini leo hii bado makundi haya yanaishia kuwaona madaktari bure lakini wanalipia dawa na wakati mwingine huduma, tutakapoingia na kutunga sheria hii mpya mwakani, hili litakuwa jambo la kisheria, na tutasimamia utekelezaji wa sheria hiyo,” alisisitiza.
Akizungumzia mipango ya wizara hiyo chini ya usimamizi wa serikali ya awamu ya tano, naibu waziri huyo alisema, wizara hiyo imejipanga kuboresha zaidi huduma za afya, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha huduma za afya zinafika hadi vijijini.
Alisema katika kipindi cha awamu ya kwanza ya serikali ya awamu ya tano wizara ya afya, imejipanga kuhakikisha inaongeza vituo vya afya kutoka 489 vilivyopo hadi kufikia vituo vya 1,000 ambavyo vyote au kwa asilimia kubwa vitakuwa pia vinatoa huduma muhimu za upasuaji kwa akinamama na upasuaji wa dharura.
“Kwa mwaka unaokuja matarajio yetu ni kuhakikisha tunaongeza idadi ya vituo vya afya vinavyotoa huduma za upasuaji kwa wajawazito, lakini pia ni lazima kuwe na huduma za uchunguzi wa magonjwa kupitia maabara na huduma za upasuaji,” alifafanua.
Alisema kupitia mpango huo, serikali itajenga timu za upasuaji katika kila kata zitakazokuwa na wataalamu wa kila fani inayotumika katika upasuaji, kuanzia fani ya usingizi, uuguzi katika vyumba vya upasuaji na madaktari wa upasuaji.
“Kwa sasa kuna vituo vya afya 489 na vilivyokuwa vinatoa huduma ya upasuaji ni vituo 113 sasa tunataka vituo vyote vitoe huduma hiyo kwa akinamama na upsuaji wa dharura,” alisisitiza.
Alisema tayari katika mwaka ujao, wizara hiyo imeilekeza mikoa na wilaya zote kutenga angalau kituo kimoja na kukiingiza kwenye bajeti itakayokuja mwakani, ili kuongeza idadi ya vituo vya afya vifikie hadi 700. Pamoja na hayo naibu huyo waziri alibainisha kuwa katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa serikali ya awamu ya tano katika sekta ya afya, kumekuwa na mafanikio makubwa katika sekta hiyo, ikiwemo kuboreshwa kwa huduma za afya na upatikanaji wa vipimo na tiba.
“Katika awamu hii, viongozi wakuu wamekuwa wakifuatilia kwa karibu maendeleo ya sekta ya afya, hata Rais John Magufuli mwenyewe alifanya ziara kadhaa katika hospitali kubwa ikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) hali iliyochangia kuimarika kwa kasi kwa sekta hiyo ya afya,” alisema.
Oktoba mwaka huu, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stella Manyanya alisema serikali iko katika mkakati wa kuwabana wanafunzi wanaopewa mikopo katika fani za kipaumbele, wanapohitimu masomo yao, kutumikia katika utumishi wa umma nchini kwa muda fulani ili kuhakikisha dhamira ya serikali ya kuwapa kipaumbele inatimia.
Fani hizo ni sayansi za tiba na afya, ualimu wa sayansi na hisabati, uhandisi wa viwanda, kilimo, mifugo, mafuta, gesi asilia, sayansi asilia, mabadiliko ya tabianchi, sayansi za ardhi, usanifu majengo na miundombinu.
Hatua hiyo inatokana na serikali kubaini kuwapo wanafunzi wanaosomea fani hizo ili kupata mikopo, lakini baada ya kumaliza hukimbilia kufanya kazi nyingine au nje ya nchi, hivyo upungufu wa wataalamu waliowakusudia kubaki kama ilivyo.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger