Tuesday 27 December 2016

Mkulima achomwa mkuki mdomoni, watokea shingoni

...

MKULIMA na mkazi wa kijiji cha Dodoma Isanga kata ya Masanze wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Augustino Mtitu,amechomwa mkuki mdomoni na kutokea shingoni.

Umemjeruhi hivyo kulazimika kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, kufanyiwa upasuaji kuondoa mkuki huo na kuokoa maisha yake.

Mtitu na wengine wanane walijeruhiwa katika vurugu zilizohusisha jamii ya wafugaji wa Kimasai na wakulima wa kijiji hicho kilichopo wilayani Kilosa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. Alisema mpaka jana watu watatu walikuwa wanashikiliwa na Polisi, na msako unaendelea kuwasaka wale wote waliohusika katika kufanya vurugu hizo.

Tukio hilo ni la Desemba 25, mwaka huu, baada ya mtu huyo kujaribu kuzuia vurugu hizo, zilizokuwa zimetokea baada ya wafugaji hao kulisha mifugo yao katika shamba la maharage na mahindi katika kijiji hicho.

Mtitu akijaribu kuzuia vurugu hizo, aliishia kuchomwa mkuki na mmoja wa wafugaji wa jamii hiyo, ambao baada ya tukio hilo walikimbia kutoka eneo hilo.

Kutokana na tukio hilo, wananchi wenzake waliamua kumkimbiza katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kwa ajili ya matibabu.

Lakini, alihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji na matibabu zaidi ya kuokoa maisha yake.

Baada ya kutokea kwa tukio hilo, muda mfupi baadaye wafugaji hao walirudi tena kijijini hapo, kwa lengo la kuokoa mifugo yao iliyokuwa imekamatwa, na ndipo walipoanzisha tena vurugu kwa kuwashambulia watu wengi wanane akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji pamoja na wa Kitongoji.

Watu watano, kati ya waliojeruhiwa, walikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kupatiwa matibabu. Diwani wa Kata ya Masanze, Bakari Pilo, akizungumza kwa njia ya simu, alisema hilo ni tukio la tatu kutokea kwenye kata yake katika kipindi kifupi.

Alisema vitendo hivyo vinaendelea kuhatarisha usalama wa wananchi, hasa wakulima, kufuatia mamlaka zinazohusika kushindwa kuwahamishia wafugaji katika eneo walilokuwa wametengewa, licha ya suala hilo kupitishwa kwenye vikao vya Baraza la Madiwani.

Stanley Andrea, ambaye ni ndugu wa Mtitu, yupo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro akimuunguza nduguye, alisema kuwa tukio hilo ni la Desemba 25, mwaka huu majira ya saa 5 asubuhi kwenye mashamba ya wakulima baada ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba ya mahindi na maharage ili kulisha mifugo.

Alisema, wakulima wenye mashamba hayo,waliamua kuifukuza mifugo hiyo, lakini wafugaji wa jamii ya Kimasai, waliingilia kati na kuanza kuwapiga kwa fimbo wakulima na kusababisha kutokea kwa vurugu baina ya pande mbili hizo.

Alisema, mfugaji mmoja wa Kimasai alichukua mkuki na kumchoma Mtitu sehemu ya mdomoni na kutokezea shingoni na kuwajeruhi wengine wanane, akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji na wa Kitongoji, ambao baadhi wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Kilosa.

Alisema kuwa vurugu ziliongezeka, pale wafugaji hao waliporudi kijijini hapo kwa ajili ya kuikomboa mifugo yao iliyokuwa inashikiliwa, kabla ya kufika kwa askari polisi kutoka mjini Kilosa.

Muuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Sanifa Mdee, alisema walimpokea mgonjwa huyo akiwa na mkuki mdomoni, ulitokea upande wa shingoni na kuanza kumpatia matibabu na kumtoa mkuki huo, ambapo amelazwa wodi namba moja hospitalini hapo.

Hata hivyo, alisema kutokana na mkuki huo kuchomwa kwa nguvu, ulijeruhi baadhi ya meno yake na kuharibu fizi, hali iliyosababisha jana madaktari kumfanyia upasuaji wa kurekebisha fizi zake, ambapo baada ya kutolewa mkuki huo, hali yake ilikuwa inaendelea vizuri.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger