Friday 30 December 2016

Mto Ruaha Mkuu wakauka

...

MTO Ruaha Mkuu unaopita ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (Runapa) umekauka maji. Hali hiyo inatishia uhai wa wanyama waliopo katika hifadhi hiyo kubwa kuliko zote nchini.

Gazeti hili lilitembelea hifadhi hiyo wiki iliyopita na kushuhudia wanyama wakihangaika kutafuta maji huku samaki, viboko na mamba ambao maisha yao yanabebwa na mto huo, wakiathiriwa kwa kiasi kikubwa na hali hiyo.

Baadhi ya miti inayoelezwa kuwa na majimaji ilishuhudiwa ikiwa imeanguka ndani ya hifadhi hiyo na maelezo yaliyotolewa na Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Runapa, Moronda Moronda ni kwamba imeharibiwa na Tembo wanaotumia miti hiyo kutuliza kiu ya maji.

Baadhi ya wadau wa mto huo, wamekosoa utekelezaji wa mikakati ya kuunusuru mto huo, wakisema haileti tija pamoja na kurejewa mara kwa mara.

Ofisa wa Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST), Malima Mbigima aliiomba serikali iingilie kati kwa kuyashughulikia masuala yote yanayosababisha mto huo ukauke.

Mbigima alisema nje ya hifadhi hiyo, mto huo umekuwa tegemeo kwa wakazi wengi ambao wamekuwa wakitumia maji yake kwa shughuli za uvuvi na kilimo.

“Hali kadhalika uzalishaji wa umeme katika mabwawa ya Mtera na Kidatu unategemea maji ya mto huu. Licha ya umuhimu huo, kiwango cha maji katika mto huo kimeendele kupungua siku hadi siku,” alisema.

“Mto Ruaha Mkuu wenye urefu wa kilomita 475 unaanzia katika Mlima Kipengere wilayani Makete mkoani Njombe, ukimwaga maji katika ardhi oevu ya Usangu wilayani Mbarali mkoani Mbeya kupitia Runapa hadi katika Mto Rufiji. Mto huu unachangia asilimia 22 ya maji ya Bonde la Rufiji ukiwa na zaidi ya aina 39 za samaki,” alisema.

Alitaja sababu kubwa ya mto huo kukauka kuwa ni shughuli za kibinadamu zinazofanywa kandokando ya vyanzo vya maji ya kwenye vyanzo vya maji vinavyopeleka maji katika mto huo.

Hivi karibuni, wadau wa mto huo waliafikiana katika kikao kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza kupanga mpango wa pamoja utakaotekelezwa kwa pamoja kurejesha mtiririko wa maji katika mto huo kwa mwaka mzima.

Katika Kikao hicho kilichofanywa kwa ushirikiano na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira na Mali Hai Duniani (WWF), kwa mara nyingine wadau hao walikiri ni hatari kubwa kwa mto huo kuachwa uendelee kukauka.

Kaimu Meneja wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Mtera, Lewis Loiloi alisema ikiwa Mto Ruaha utakauka kabisa, basi gridi ya Taifa itaondokewa na megawati 284 za umeme.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger