Sunday 23 October 2016

Majambazi wanne wauawa Katika Mapambano Makali Mkuranga

...


Jeshi la Polisi Mkoa wa Temeke limeua watu wanne wanaodhaniwa kuwa ni majambazi katika wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Gilles Muroto alisema tukio hilo ni la Oktoba 21 baada ya polisi kupata taarifa za kuwepo kwa kundi la watu wanaodhaniwa ni majambazi.

Alisema baada ya taarifa, kikosi kazi cha Polisi cha Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kilifanya ufuatiliaji na kubaini nyumba ambayo haijakamilika imezungushiwa uzio na muda wote mlango wa uzio huo ulikuwa umefungwa.

Aliongeza kuwa uchunguzi wa kina, ulifanyika na kubaini kuwa kweli kundi hilo, lipo ndani ya nyumba hiyo na kwamba muda mwingi mlango wa uzio, hufungwa na kuongeza kuwa majira ya saa tano askari wa kikosi kazi cha mkoa huo na mkoa wa Pwani, kilizingira nyumba hiyo.

“Baada ya kujipanga mlango wa uzio huo uligongwa na kutoa amri ya kuwataka walioko ndani ya nyumba hiyo wafungue mlango na kujisalimisha, lakini tulishangaa baada ya amri hiyo ghafla milio ya risasi ilianza kutoka ndani ya nyumba hiyo,” alisema Muroto.

Aliongeza kuwa baada ya milio hiyo, askari ambao walikuwa makini na wakiwa wamezingira nyumba hiyo wakiwa wamejipanga katika miundo ya mapigano, walianza mashambulizi kujibu mashambulio hayo.

Alisema majibizano yaliendelea na watu hao waliokuwa wanashambulia kutoka ndani, walivunja uzio na watu wanaokadiriwa kuwa zaidi ya watano walitoka huku wakiwa wanashambulia.

Muroto alisema askari waliendelea kupambana nao na kufanikiwa kuwajeruhi baadhi yao, na wengine walifanikiwa kutoroka na silaha zao.

“Mashambulizi kutoka ndani yalitulia na askari waliingia ndani ya uzio, kwa kuwa yalikuwa mapambano ya nguvu walikuta majambazi watatu wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 na 30 wakiwa wamejeruhiwa kwa risasi na hali zao zilikuwa mbaya na tuliwapeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili lakini walibainika kuwa tayari wameshakufa na miili yao imehifadhiwa hapo ikisubiri kutambuliwa,” alisema.

Alisema baada ya kufanya upekuzi, polisi walikuta silaha moja aina ya short gun pump action yenye MV.51516 R na namba ya usajili TZ car 99987 na risasi tano ndani ya magazini yake.

Risasi nyingine sita za short gun zilikutwa ndani ya mfuko wa plastiki pamoja na risasi nane za pistol.

Aidha alisema katika tukio hili, ilibainika kuwa kuna askari mmoja alijeruhiwa bega lake la kushoto na lilikuwa jeraha kubwa la risasi, hivyo alipelekwa katika Hospitali ya Muhimbili ambako amelazwa na anaendelea kupata matibabu akisubiri kufanyiwa upasuaji.

Muroto alisema ufuatiliaji wa majambazi, walitoroka eneo la mapambano uliendelea kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji cha Mtambani, ambapo majira ya saa tatu asubuhi jambazi mmoja alipatikana akiwa mahututi na juhudi za kumfikisha hospitali zilifanyika. Hata hivyo, alikufa akiwa njiani.

”Tunawashukuru wananchi wote wema kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha kwa Jeshi la Polisi, kwa kuliunga mkono katika kufichua wahalifu na kupambana na wahalifu, nitoe tahadhari kuwa mkoa huu ukifanya tukio ujue utashughulikiwa kabla hujakamilisha na ukifanikiwa kukamilisha azma yako haitachukua muda utakamatwa,” alisisitiza.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger