Wednesday 19 October 2016

BAVICHA WATOA TAMKO KUHUSU WANAFUNZI WENGI WA ELIMU YA JUU KUKOSA MIKOPO 2016/2017

...

Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) tumepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa kuwa utawala huu wa Serikali ya CCM, chini ya Rais John Magufuli zaidi ya nusu ya wanafunzi waliodahiliwa kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu mwaka wa masomo 2016/2017, wako katika hatari ya kukosa fursa ya kupata elimu hiyo kwa sababu ambazo hazieleweki hadi sasa.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari na vyanzo vingine, Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) imeweza kudahili takriban wanafunzi wapya 58,000 kwa ajili ya elimu ya juu katika vyuo vikuu mbalimbali nchini kwa mwaka huu wa masomo.

Lakini katika hali ambayo tunajua itaumiza vijana wengi na kuwasikitisha Watanzania, taarifa ambazo zimethibitishwa na Serikali ya Rais Magufuli kupitia kwa Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo, ni kwamba zaidi ya nusu ya idadi hiyo ya waliodahiliwa na TCU kusoma elimu ya juu, hawatapata mikopo!

Hivyo ndoto za kutafuta mafanikio yao, kwa ajili ya jamii zao na taifa letu kwa ujumla zinaelekea kukatiliwa. Hili ni jambo kubwa na zito kwa sababu linagusa moja ya misingi muhimu ya taifa lolote lenye ndoto ya kutaka kuendelea, achilia mbali kuwa taifa lenye uchumi wa kati unaotegemea viwanda.

Kwa mujibu wa Gazeti la The Guardian la Oktoba 18, mwaka huu, Serikali ya CCM, chini ya Rais Magufuli imesema itawakopesha wanafunzi wapatao 24,000, idadi ambayo haifiki hata nusu ya wanafunzi wote waliodahiliwa na TCU.

Hata hivyo kauli hiyo ya Mkurugenzi wa Bodi, tumeichukulia kuwa si ya kweli hata kidogo, bali ya mtu anayejaribu kuficha mambo kwa ajili ya “nusu shari kuliko shari kamili”.

Tunasema hivyo kwa sababu hadi sasa Bodi hiyo hiyo, imeshatoa mikopo kwa wanafunzi 3,966 tu. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 6 tu kati ya wanafunzi wote waliopata udahili wa kusoma elimu ya juu kwa mwaka huu.

Maana yake ni kwamba kuwakopesha vijana wapatao 24,000 ili wasome elimu ya juu bado nayo ni ahadi tu ya maneno, lakini uhalisia uliopo kwa vitendo hadi sasa ni kwamba Serikali ina uwezo wa kuwakopesha vijana wake 3,966 pekee nchi nzima.

Idadi hiyo ambayo serikali imeweza kuwakopesha mikopo, haifiki hata nusu ya jumla ya wanafunzi wanaopaswa kudahiliwa na mojawapo ya vyuo vikuu vikubwa nchini, mathalani Chuo Kikuu Dar es Salaam.

WAMEKOPESHWA CHAKULA NA KULALA, SI KUSOMA!
Aidha, kwa muda mrefu sasa, walau tangu kuanza kwa utaratibu wa serikali kuwakopesha wanafunzi kwa ajili ya elimu ya juu, inaeleweka kuwa HESLB imekuwa ikitoa mikopo kwa ajili ya vitu vitatu; ada, malazi na chakula.

Katika hali ambayo inazidi kushangaza na kuibua maswali kuwa kuna jambo kubwa ambalo linafichwa, BAVICHA tunazo taarifa kuwa hata hao wanafunzi asilimia 6 ambao bodi inadai imeshawapatia mkopo, katika vyuo vingi wamepata fedha kwa ajili ya CHAKULA NA KULALA tu.

Hawajalipiwa fedha ya ada (tuition fees hadi sasa).
Kwa mantiki hiyo ni kwamba, Serikali ya CCM, chini ya Rais Magufuli hadi sasa wiki ya tatu tangu vyuo vifunguliwe si tu kwamba imeshindwa kuwakopesha wanafunzi wote wanaostahili kupata mkopo kwa ajili ya elimu ya juu, bali hata imeshindwa hata kulipa fedha za ada kwa wanafunzi ambao tayari imeshawakopesha. Hali hii ikiendelea tutegemee kuona vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu vikifungwa kwa sababu vitakuwa haviwezi kujiendesha.

Taarifa hizi za Bodi ya Mikopo zinapaswa kulishtua taifa letu na kila Mtanzania aone jinsi ambavyo Serikali ya CCM chini ya Rais John Magufuli haijajipanga na wala haijui inachokifanya katika kuhakikisha inatoa elimu bora kwa Vijana wetu.

Lakini pia zinathibitisha kuwa Serikali ya Rais Magufuli iko katika hali mbaya ya kifedha na hivyo inahitaji msaada wa fikra mpya nje ya CCM kuikwamua vinginevyo tujiandae kwa mwendelezo wa janga kubwa zaidi katika sekta ya elimu.

Tunamtaka Rais John Magufuli kujitokeza hadharani, na kuueleza umma wa Watanzania hatma ya Vijana waliokosa mikopo, na kama ahadi zake alizozitoa wakati wa Kampeni zilikuwa ni ulaghai au ghiliba za kutafuta kura?
 
Pia Rais Magufuli anapaswa kuwaeleza watanzania ikiwa ameshindwa utekelezaji wa ahadi zake ikiwemo Elimu bora, au akubali kuwa yeye ni Muongo kwa sababu wakati wa kampeni alisema nanukuu; “ETI NIWE RAIS HALAFU NISIKIE WANACHUO WAMEKOSA AU WAMECHELWESHEWA MIKOPO YAO, WATANIJUA MIMI NI NANI, KITU CHENYEWE KINAITWA MIKOPO HALAFU UNACHELEWESHA” Mwisho wa kunukuu.

Tunawataka Viongozi wa serikali za wanafunzi katika Vyuo Vikuu vyote nchini, kuungana pamoja ili kudai haki ya wanafunzi wenzao, tukitambua kuwa, baadhi ya Viongozi wa shirikisho la serikali za wanafunzi wa elimu ya Juu (TAHILISO) wamekuwa wakitumika kwa ajili ya CCM badala ya maslahi mahsusi ya wanafunzi na hivyo kuidhoofisha taasisi hii muhimu ya wasomi, hivyo umoja wao ni muhimu katika kuipata haki hii.

Tunatoa wito kwa taasisi mbalimbali za kutetea haki za vijana, asasi za vijana pamoja na mtandao wa wanafunzi Tanzania, kujitokeza hadharani na kuwapigania vijana hawa katika kuhakikisha wanapata haki yao ya msingi ya elimu.

Imetolewa leo Jumatano,19.10.2016
Patrobas Katambi
Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger