WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Ufundi iweke mpango maalumu wa kuongeza wataalamu zaidi katika sekta ya
afya ndani ya nchi ili kuipunguzia Serikali gharama za kusomesha
wataalam hao nje ya nchi.
Ametoa
agizo hilo Ijumaa, Septemba 2, 2016 wakati alipokagua maendeleo ya
mradi wa ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya na Sayansi
ya Tiba Muhimbili (MUHAS) na Ujenzi wa Kituo cha Tiba cha Kimataifa cha
Muhimbili katika eneo la Mloganzila.
Amesema
Serikali zilizotangulia zimefanya kazi kubwa na nchi imefikia hatua
nzuri ya kuongeza wataalam ndani ya nchi ambao watakwenda kutatua
changamoto ya upungufu wa madaktari bingwa kwenye hospitali za mikoa na
wilaya.
Waziri
Mkuu amesema ujenzi wa kituo hicho cha tiba cha kimataifa pia
utawapunguzia wananchi adha ya kutafuta fedha za kwenda kupata matibabu
nje ya nchi. Tayari upasuaji mkubwa wa magonjwa ya moyo umeanza
kufanyika nchini.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Bw.
Humphrey Polepole awasake watu wote waliohusika na wizi wa lita 1,000 za
mafuta ya kuendeshea mitambo katika karakana ya mkandarasi anayejenga
Kampasi hiyo.
“Wafanyakazi
waache wizi. Lita 1,000 zinaondokaje katika karakana ya mkandarasi? Hii
kampuni inayolinda kama imeshindwa kazi iondolewe na Mkuu wa wilaya
usimhurumie mwizi,” amesisitiza.
Kwa
upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce
Ndalichako amesema kukamilika kwa kampasi ya Mloganzila kutasaidia
upatikanaji wa madaktari bingwa wengi nchini ambao watapunguza gharama
za kupeleka wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Awali,
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Ephata Kaaya alisema kukamilika kwa
hospitali pamoja na kampasi yote ya chuo kutawezesha kupunguza kwa kiasi
kikubwa uhaba wa wataalamu wa afya nchini.
Amesema
hospitali hiyo itatumika kutoa huduma za afya za kitaalam zaidi kwa
magonjwa mbalimbali, hivyo kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje
ya nchi kwa matibabu. Pia itapunguza msongamano wa wagonjwa katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Ujenzi
wa mradi huo umegharimu Dola za Kimarekani milioni 61, ambapo Serikali
imetoa Dola milioni 18 na Serikali ya Korea imetoa mkopo wa Dola milioni
43. Kukamilika kwa ujenzi wa kampasi hiyo ya Mloganzila kutawezesha
chuo kuongeza idadi ya udahili wa wanafunzi wa fani ya afya kutoka 4,010
hadi 15,000.
Prof.
Kaaya amesema mkataba wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa mradi huo
ulisainiwa tarehe 12, Desemba, 2014 na ujenzi ulianza mwezi Julai, 2015
na unatarajiwa kukamilika Oktoba, 2016.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
0 comments:
Post a Comment