RAIS
John Magufuli, amemtaka Dk. Ali Mohamed Shein, kumpa tuzo Jecha Salim,
mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Zanzibar, kutokana na kile alichokiita
kazi nzuri aliyoifanya visiwani humo mwaka jana, kwa kufuta matokeo ya
uchaguzi mkuu.
Rais Magufuli aliyasema hayo jana
jioni, katika ziara yake ya kikazi visiwani Pemba. Wakati Rais Magufuli
akichaguliwa katika uchaguzi wa Oktoba mwaka jana, Dk. Shein
alichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar kufuatia uchaguzi wa marudio
uliofanyika Machi mwaka huu.
“Nampongeza
sana Jecha kwa kazi nzuri aliyofanya kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar,
na kwa kweli Dk. Shein kama kuna tuzo zako utakazotoa, naomba usimsahau
kumpa na Jecha,” alisema Rais Magufuli.
Rai Magufuli pia alimtaka
Rais huyo wa Zanzibar kumtaarifu yeye ili awashughulikie watu wote
wanaomsumbua visiwani humo au wanaoonekana kumzidi nguvu.
“Rais
Shein kama kuna mtu unaona anakusumbua wewe au anakupa tabu nijulishe
mimi tu, hata dakika tano hazitapita nitamshughulikia,” ameeleza.
Kauli
hiyo inakuja, ikiwa ni zaidi ya miezi kumi sasa tangu hali ya mahusiano
baina ya wananchi wa Zanzibar iwe tete, tangu pale Jecha Salim Jecha,
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi visiwani humo (ZEC) alipotangaza kufuta
matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Mahusiano
hayo mabaya yamesababisha, wafuasi wa vyama vya CUF na CCM vyenye nguvu
zaidi visiwani humo, kufikia hatua ya kusitisha ushirikiano katika
shuguli za kiuchumi na kijamii ikiwemo kutohudhuria misiba na kutonunua
bidhaa za mtu wasiyeendana naye kiitikadi.
“Niombe
vyombo vya ulinzi na usalama wafuatilie hao wanaokatakata na kuchoma
karafuu washughulikiwe bila huruma. Atakayejaribu kuichezea amani,
atacheza yeye tena mchezo asiojua kuucheza,” aling’aka Rais Magufuli.
Tangu kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka jana visiwani Zanzibar, hali ya usalama imekuwa si ya kuridhisha.
Nyumba na mashamba ya karafuu yamekuwa yakichomwa moto, huku baadhi ya watu wakitiwa mbaroni na vyombo vya dola kwa tuhuma hizo
0 comments:
Post a Comment