Na.Mwandishi Wetu-MAELEZO
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mpya, Bw. Charles Kichere amesema kuwa ataendelea kutekeleza majukumu ambayo yameachwa na CAG aliyemaliza muda wake Prof.Mussa Assad kwani Ofisi hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya watanzania.
Akizungumza katika makabidhiano Kichere alisema kuwa Ofisi ya CAG ni nguzo muhimu kwa watanzani kwani ndiyo ofisi inayolinda na kuangalia matumizi sahihi ya kodi yao wanayolipa kila siku.
“Tutaendelea kuifanyakazi ambayo imefanywa na Prof.Assad na timu yake, nitahakikisha kushirikiana na wafanyakazi wa Ofisi hii kuifanya kazi hii ya kulinda mapato ya kodi ya watanzania”, Alisema Kichere.
Kichere alisema kuwa katika kutekeleza majukumu hayo mapya atahakikisha kuwa atalinda Kodi ya watanzania wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara na wafanyakazi ili fedha inayopataikana kwenye kodi iweze kuwanufaisha wote.
Aliwahakikishia watanzania kuwa hakuna kodi inayotolewa na watanzania ambayo itapotea kwa hiyo ataangalia na kuilinda kwaajili ya kuwaletea maendeleo.
“Nataka kufanya kazi kulinda maslahi ya watanzania nimefanyakazi Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA najua ugumu wa kukusanya kodi na kupata mapato, kwa hiyo nitahakikisha kuwa nailinda kodi ya wananchi kwa wivu mkubwa sana”, Alisisitiza Kichere.