Tuesday, 5 November 2019

Shehena Ya Mifuko Isiyokidhi Viwango Yakamatwa

...
Ofisi ya Makamu wa Rais inaendelea kusimamia marufuku ya katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki kwa kushirikiana na Kikosi kazi cha Kitaifa. 

Kwa siku za hivi karibuni kumekuwepo na wimbi la uzalishaji, utengezaji na uingizaji na usambazaji wa mifuko isiyokidhi viwango vilivyowekwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Kikosi kazi cha Kitaifa cha kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki pamoja na Kamati za Mikoa na Wilaya wanaendesha oparesheni maalumu nchi nzima kwa lengo la kusaka mifuko isiyokidhi viwango.

Tarehe 30/10/2019 NEMC ilikamata marobota 21 katika Wilaya ya Misenyi, Mkoani Kagera na marobota 7 Mkoani Arusha ambayo yanashikiliwa katika kituo cha polisi cha Arusha. Upelelezi wa mashauri haya bado unaendelea.

Tarehe 4/11/2019 Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi kwa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mwanza wamekamata shehena ya mifuko isiyokidhi viwango gunia 8 yenye thamani ya Shilingi 10,000,000/-  Mifuko hiyo iliingia kupitia bandari bubu ya Bwiru jijini Mwanza ikitokea nchi jirani. Watuhumiwa watafikishwa mahakamani na mifuko hiyo itateketezwa kwa mujibu wa sheria kama itakavyoelekezwa na NEMC.

Ofisi ya Makamu wa Rais, inatoa wito kwa wafanyabiashara wote wanaojihusisha na uingizaji, usambazaji na uuzaji wa mifuko mbadala kuhakikisha wanazingatia matakwa ya Sheria. Aidha, wafanyabiashara wanasisitizwa kuacha kuzalisha, kuingiza nchini, kuuza na kusambaza mifuko isiyokidhi viwango. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote wanaokiuka agizo hilo.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger