Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linapenda kukanusha taarifa zinazoendelea kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, zinazoelezea kuhitajika kwa vijana wa JKT kundi la kujitolea Operesheni Kikwete na Operesheni Magufuli kukusanyika katika Kambi ya JKT Mgulani jijini Dar es Salaam tarehe 08 Julai 2019 kwa ajili ya usaili.
Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa yanazikanusha taarifa hizo za uzushi zenye lengo la kuwachanganya vijana wetu ambao wamehitimu mafunzo ya JKT na kurejea makwao.
Siku zote JKT imekuwa ikisisitiza kuwa vijana wanaojiunga na mafunzo ya JKT ni vyema wakatambua kuwa mafunzo hayo hayana uhusiano wa kupatiwa ajira kwenye vyombo vya ulinzi na usalama mara wamalizapo mkataba, bali mafunzo hayo yanawajengea uwezo wa kujuwa stadi za kazi na stadi za maisha.
Jeshi la Kujenga Taifa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wanafatilia kwa karibu kikundi kidogo chenye tabia ya kusambaza taarifa potofu na za uvumi zinazohusu JKT.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Habari na Uhusiano
Makao Makuu ya JKT
Tarehe 03 Julai 2019.