Tuesday, 3 December 2024
TBS YATOA ELIMU KUHUSU VIWANGO NA UBORA WA BIDHAA MKOANI SONGWE
TPA YATWAA TUZO YA MWAJIRI BORA WA MWAKA KWENYE SEKTA YA UMMA
Monday, 2 December 2024
WENYE ULEMAVU KUPATIWA MAFUNZO YA UONGOZI
MAAMBUKIZI YA VVU YAPUNGUA NCHINI TANZANIA-WAZIRI MHAGAMA
Leo ni tarehe 1 Desemba 2024, ambapo dunia inaadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani. Kitaifa, maadhimisho haya yamefanyika Mkoani Ruvuma yakiongozwa na mgeni rasmi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango.
Akitoa taarifa yake, Waziri wa Afya nchini, Mheshimiwa Jenista Mhagama, ameeleza juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI.
Amesema, Serikali imeendelea kugharamia dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI (ARVs), hatua inayosaidia wananchi wanaoishi na maambukizi ya virusi hivyo kuendelea na maisha ya kawaida.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, wananchi takriban milioni 1.7 wanaishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI nchini.
Serikali imetumia shilingi bilioni 750 kununua dawa za ARVs, ambapo gharama ya matibabu kwa kila mgonjwa mmoja ni takriban shilingi 400,000 kwa mwaka.
"Maadhimisho haya ni fursa muhimu ya kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa wa UKIMWI na kupunguza unyanyapaa" amesema Mhe. Jenister
Pamoja na hayo amehimiza jamii kuchukua hatua za kinga na matibabu kwa ushirikiano wa karibu na wadau mbalimbali.
Kaulimbiu ya mwaka huu inalenga kuimarisha mshikamano wa kidunia katika kukomesha maambukizi mapya na kuboresha huduma kwa walioathirika.
Sunday, 1 December 2024
DKT.MPANGO -MKAKATI WA SERIKALI NI KUTOKOMEZA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA UKIMWI NCHINI
Siku ya Ukimwi Duniani, Imeadhimishwa Kitaifa leo tarehe 01/12/2024, maadhimisho yamefanyika katika Uwanja wa Majimaji, Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma.
Hafla hii imeongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, ambaye amesisitiza azma ya serikali kuhakikisha inatokomeza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) nchini.
Katika hotuba yake, Mhe. Dkt. Mpango, ameonesha dhamira ya dhati ya Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kupambana na maambukizi mapya ya VVU.
Takwimu zinaonesha kwamba vijana, hasa wa kike, wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa. Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, serikali imeweka mkazo mkubwa katika kutoa elimu kwa vijana ili kuwasaidia kujitambua, kuchukua hatua za kujikinga, na kwa wale wanaoishi na VVU, kuhakikisha wanafuata taratibu kwa kutumia dawa za kupunguza makali ya virusi (ARVs).
Aidha, Mhe. Dkt. Mpango ametoa wito kwa jamii nzima kushirikiana, kuhakikisha kwamba maambukizi mapya yanapungua, kwa kuelimisha vijana kuhusu umuhimu wa afya ya uzazi, matumizi sahihi ya kinga, na upimaji wa afya mara kwa mara.