Friday 24 November 2023

WAZIRI MKUU AJIONEA HUDUMA ZINAZOTOLEWA NA NSSF

...
#Ni katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha ambayo yanaenda sambamba na elimu ya hifadhi ya jamii

NA MWANDISHI WETU ARUSHA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alitembelea banda la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa, katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha 2023 yanayoendelea katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid, Mkoani Arusha.

Wiki ya Fedha 2023, imebeba kauli mbiu isemayo 'Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo Kiuchumi' ilizinduliwa na Waziri Mkuu, tarehe 22 Novemba, 2023.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma, Lulu Mengele alimueleza Mhe. Waziri Mkuu huduma zinazotolewa katika banda hilo ambazo zinaenda sambamba na elimu ya fedha kwa upande wa kuandikisha wanachama, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao kwa upande wa sekta binafsi na sekta isiyo rasmi.

Lulu alisema NSSF inatumia fursa hiyo kuwakumbusha baadhi waajiri wa sekta binafsi kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati ili kuepusha usumbufu kwa wanachama pindi wanapotoka kwenye ajira kwa mujibu wa sheria ambapo elimu hiyo inaenda pamoja na elimu ya fedha kwa kuwajengea uelewa wanachama wake na jamii kutambua mambo muhimu yanayoweza kuwaendeleza kiuchumi.

Vilevile, Lulu alimueleza Mhe.Waziri Mkuu kuwa NSSF inatumia fursa ya Wiki ya Huduma za Fedha kuendelea kutoa elimu kwa wananchi waliojiajiri wenyewe wakiwemo wakulima, wafugaji, mama lishe, bodaboda kujiunga na kuchangia NSSF kwa ajili ya maisha yao ya sasa na baadaye.

Alisema Mfuko unaendelea kutatua kero mbalimbali za wanachama na wadau wake kwa kuboresha huduma kupitia mifumo mbalimbali ya TEHAMA ambapo kupitia mifumo hiyo wanachama wanaweza kupata taarifa zao popote walipo bila ya kulazimika kufika katika Ofisi za NSSF.

Naye, Furahisha Wabanu, Kaimu Meneja wa NSSF Mkoa wa Arusha, aliwakaribisha wananchi wote kutembelea banda la NSSF kwa ajili ya kupata huduma zote zinazotolewa na Mfuko ikiwemo elimu ya hifadhi ya jamii, kujiunga na kupata kadi zao papo hapo, kupata taarifa zao za michango na kupata elimu kuhusu uwekezaji.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger