Monday 13 November 2023

TANZANIA YANADI VIVUTIO VYAKE KWA WATALII NA WAWEKEZAJI MAHIRI DUNIANI

...


Na Happiness Shayo- Arusha 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amewahakikishia kundi maalum la wawekezaji na watalii mahiri duniani zaidi ya 150 kutoka nchini Marekani na nchi nyingine duniani lililowasili nchini Novemba 4,2023 kuwa Tanzania  itaendelea kushirikiana nao  kikamilifu katika jitihada za kukuza uchumi wa Tanzania kupitia sekta ya utalii

Akizungumza katika hafla iliyofanyika leo Novemba 12,2023 katika ukumbi wa Hoteli ya Mout Meru jijini Arusha, Mhe.Kairuki  amesema moja ya lengo kuu la hafla hiyo  ni kuitangaza Tanzania kama kivutio cha utalii na pia soko la utalii la kuvutia na la uhakika kwa wageni wa Marekani. 

“Serikali ya Tanzania inahimiza uwekezaji katika miundombinu na maendeleo ya masoko ya utalii na hii ni  fursa nzuri kwa makampuni ya Marekani kuongeza mauzo na kupata maeneo ya kimkakati ya kukuza uwekezaji barani Afrika” Mhe. Kairuki amesisitiza.

Aidha Mhe. Kairuki ametumia fursa hiyo kuyakaribisha makampuni ya Marekani kushiriki katika kukuza sekta ya utalii ya Tanzania. 

Amefafanua kuwa  Sekta ya utalii  nchini Tanzania huzalisha zaidi ya dola Bilioni 2.6 katika pato la Taifa pamoja na kutoa ajira zaidi milioni 1.5 kwa wananchi wake.

Kuhusu ongezeko la Idadi ya watalii wanaotembelea nchini Tanzania Mhe. Kairuki amesema mwaka jana ulikuwa mwaka wa rekodi kwa utalii nchini Tanzania, ambapo zaidi ya wageni milioni moja walikuja kufurahia maeneo ya ikolojia ambapo jumla  watalii 100,600 walikuwa ni kutoka nchini Marekani.

Amesema ongezeko la idadi ya watalii linatokana na kuongezeka kwa utangazaji wa Utalii kupitia Filamu ya “Tanzania the Royal Tour”  pamoja na matangazo ya television ya  CNN ambapo vivutio vya utalii vinaendelea kutangazwa duniani kote.

 Katika hatua nyingine, Mhe. Kairuki amesema Tanzania itakaribisha kikundi cha wachezaji 120 maarufu wa tenisi na wapenda tenisi kutoka Marekani ambao watakuwa kwenye McEnroe Luxury Safari Tour, na Mashindano ya Tenisi yatakayofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mwezi Desemba,2023.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger