Monday 27 November 2023

ANDAENI WAINJILISTI WA KUDUMU WATAKAO FANYA KAZI YA KUENEZA INJILI - MCH. MWAZYUNGA

...



Na. Gideon Gregory, Dodoma.

Kiongozi wa Uinjilisti Kanisa la Moravian Nkuhungu Jijini Dodoma Mch. Boaz Mwazyunga ametoa wito kwa kanisa hilo jimbo la Kaskazini kuwa na mpango wa kuandaa wainjilisti wa kudumu ambao pamoja na kazi yao watafanya kazi ya kueneza injili ikiwa ni pamoja na kufungua na kupanda makanisa mapya vijijini.


Mch. Mwazyunga ametoa wito huo leo Novemba 26,2023 wakati akiongoza waumini wa kanisa la Moravian Tanzania jimbo la Kaskazini ushirika wa Nkuhungu kuadhimisha miaka 16 ya kutoa huduma ya kiroho kwa waumini hao nakuongeza kuwa hapaswi kuogopa gharama na kuangalia nani yupo katika maeneo wanayokwenda pamoja na mazingira yaliyopo.


“Wito wangu ni kuona kuwa kanisa linatii agizo la Bwana Yesu Kristo alilosema, basi nendeni mkawafanye mtaifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la baba, na mwana na roho mtakatifu na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi na tazama mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari (Mathayo 28:19-20),”amesema.


Aidha ameongeza kuwa Kanisa hilo limekuwa nyuma kwasababu ya kutokufanya uinjilisti na watu kuwa na dhana ya kuwa kazi ya kufanya uinjilisti ni ya watu au kikundi fulani, kumbe ni kazi hiyo ni ya watu wote.


“Umefika wakati sasa wa kwenda maeneo ya pembezoni na vijiji kununua viwanja na mashamba ili tunapofanya uinjilisti wale tutakaowapa wawe na mahali pa kuanzia kuabudia,”ameongeza.


Awali akitoa mafundisho Mwenyekiti wa Kanisa la Moravian Tanzania jimbo la Kaskazini Mch. Isaac Siame ametoa rai kwa waumini kumruhusu Mungu awatumie katika utumishi wao na kuongeza kuwa wasikubali shetani akawatumia katika mipango yake hovu kwa wanadamu.



Amesema mpango wa Mungu kwa mwanadamu ni kipaumbele tosha katika kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo mwanadamu peke yake hawezi kuzitatua pasipo kumshirikisha Mungu na kutenda yale ambayo yanapendeza mbele Bwana.


Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi Wakili wa Ushirika 2023 Lilian Nzowa amesema tangu ushirika huo uanzishwe umefanikiwa kuongeza wakristo 170 kutoka 58 hapo awali wakati unaanzishwa ongezeko linalojumuisha watu wazima pamoja na watoto.


Sambamba na hayo maeongeza kuwa kwa mwaka 2024 wanatarajia kuanza ujenzi wa jengo la kuabudia linalotarajia kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 2 ambalo litakuwa na uwezo wa kuchukua jumla ya watu 800 kwa ibada moja.


Kanisa la Moravian Tanzania jimbo la Kaskazini wilaya ya Kati ushirika wa Nkuhungu lilianza ibada rasmi Novemba 25,2007 kutoka ushirika wa Dodoma na Mch. Esau Kalinga ndiye aliyeongoza ibada hiyo na kutangaza rasmi kwamba Nkuhungu ni ushirika siyo mtaa.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger