Waziri wa Madini Doto Biteko
Waziri wa Madini Doto Biteko
Na Dinna Maningo, Tarime
WAZIRI wa Madini ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Bukombe Doto Biteko ametoa wiki mbili kwa Serikali ya mkoa wa Mara ambayo imeuzuia Mgodi wa North Mara kutoa fedha za Uwajibikaji wa makampuni kwa Jamii ( CSR) kwa ajili ya kujenga miradi katika vijiji vinavyozunguka Mgodi,kuhakikisha fedha zinatolewa ili ziendelee kutekeleza Miradi ya maendeleo.
Biteko ameyasema hayo Februari,24,2022 wakati alipotembelea bomba la maji taka katika mgodi huo lililopasuka maeneo ya barabara binafsi ya mgodi na kuzua taharuki kwa wananchi.
"RC tumeongea nae kasema baada ya wiki mbili watakuwa wamekamilisha uchunguzi na miradi itaanza kutekelezwa,viongozi wasikilizeni watu wa chini hata kama hajui kiswahili wekeni mkalimani,watu wana maswali lakini hakuna anayewajibu.
"Kitu kinachojenga mahusiano kati ya wananchi na mgodi ni fedha za CSR mna Bilioni 5.6 bado na ya mwaka jana Bilioni moja zipo tu wakati kule halmashauri ya Bukombe kupata Bilioni moja ni kazi,nyie mnakaa na fedha za miradi,fedha zitolewe miradi itekelezwe",amesema Biteko.
Biteko amesema kuwa kutotolewa kwa fedha hizo ni kuusababishia mgodi kulaumiwa na wananchi wakati tatizo lipo kwa viongozi jambo ambalo linavunja mahusiano baina ya mgodi na vijiji vinavyozunguka mgodi.
Biteko ameutaka mgodi kujenga mahusiano mazuri na wananchi nakwamba nafasi kubwa za uongozi katika mgodi zinaongozwa na watanzania "kama afisa mahusiano wa mgodi hawezi,toa weka wengine,meneja wa huu mgodi ni mtanzania na tumewaweka kwakuwa ndiyo wanajua tamaduni zetu,tumeachiwa mgodi kuendesha wenyewe tatizo likitokea tusiwalaumu wazungu"
Mbunge wa Jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara amesema kuwa kitendo cha RC Mara kuzuia fedha kumekwamisha miradi mbalimbali kutotekelezwa baada ya kukosekana kwa fedha ukiwemo mradi wa maji kijiji cha Nyangoto unaonjengwa kwa fedha za CSR sh.Milioni 998,uliosimama baada ya mkandarasi kampuni ya Gokona kutolipwa fedha za ujenzi licha ya kuanza ujenzi kwa fedha zake ujenzi uliofikia asilimia 34.
"Tunamshukuru Waziri Biteko kufika na mwafaka kautoa kilio chetu ilikuwa ni pesa zilizozuiliwa zitolewe zifanye kazi wakati huo serikali ya Mara ikiendelea na uchunguzi wake wa matumizi mabaya ya fedha za CSR",amesema Waitara.
Mkuu wa mkoa wa Mara Ally Hapi amesema kuwa yeye anachopambana nacho ni utoaji wa fedha zinazolenga kwenye miradi lakini zinaishia kwenye matumbo ya watu akisisitiza kuwa fedha za CSR zilizopita ni wizi mtupu na kwamba Serikali ya mkoa huo itasimama imara.
"Tunachotaka tukikubaliana mradi ujengwe,ujengwe sisi tunajenga kituo cha afya kwa milioni 300 lakini kuna kijiji kimejenga kituo cha afya kwa Milioni 800 hakijakamilika,wananchi msitumike kama kichaka,fedha zinatumika nyingi kuliko mradi,nataka fedha zifanye kazi fedha za CSR za 2019 kuna fedha milioni 300 zilitengwa kutekeleza mradi hazijatumika unaomba tena fedha"amesema Hapi.
RC Hapi amesema kuwa wamejipanga vizuri ndani ya muda mfupi miradi itatekelezwa ukiwemo mradi wa maji Nyangoto ambao ameambiwa kuwa umeshafanyiwa usanifu na utajengwa na kwamba yeye hawezi kubariki wizi hivyo watu waache janjajanja na watekeleze miradi kwa ufanisi na kwa haraka.
0 comments:
Post a Comment