Kijana mwenye umri wa miaka 21 amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja gerezani au kulipa faini ya KSh 100,000 sawa na shilingi 2,100,000/- za Tanzania kwa tuhuma za kushiriki wizi dukani.
Alvin Linus Chivondo alishtakiwa kwa kuiba kilo 5 za mchele, lita 5 za mafuta ya kupikia, kilo 2 za sukari, asali na majani ya chai bidhaa zote zenye thamani ya KSh 3,165 sawa na shilingi 66,000 za Tanzania kutoka kwa duka la jumla la Naivas karibu na Moi Avenue nchini Kenya.
Akiwa mbele ya hakimu mkuu wa Mahakama ya Milimani Wendy Micheni mnamo Jumatano, Aprili 13,2022 Chivondo alikiri mashtaka mawili ya kuiba na kumiliki bidhaa za wizi.
Mshukiwa huyo ambaye husukuma mkokoteni jijini aliiarifu mahakama kwamba yeye na familia yake walikuwa wamelala njaa kwa siku tatu.
"Nina mtoto wa miezi minne na nilikuwa nimeshindwa kuilisha familia yangu. Unaona niliiba tu chakula. Tangu nilipopoteza ajira yangu sijakuwa na uwezo wa kuilisha familia yangu,” alijitetea.
Mahakama iliambiwa kuwa Chivondo alijifanya mteja, akaokota bidhaa kisha kuvipakia kwenye begi alilokuwa nalo.
Hata hivyo, alinaswa na wafanyakazi wa duka wanaosimamia kamera za CCTV, alipojaribu kutoka katika duka hilo bila kulipa.
Korti iliarifiwa kwamba mshukiwa alikuwa ameshikwa hapo awali akiiba dukani humo na kusamehewa.
0 comments:
Post a Comment