Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dkt. Charles Msonde akifafanua jambo kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda (Mb) wakati akikagua Mfumo wa kidijitali utakaotumika kusahihisha mitihani ya Vyuo vya Ualimu mwaka huu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda (Mb) akifuatilia kwa makini namna Mfumo wa kidijitali unavyofanya kazi wakati wa ukaguzi wa majaribio ya usahihishaji mitihani kwa kutumia Mfumo huo yaliyofanyika katika ofisi za Baraza la Mitihani Tanzania.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda (Mb) akifafanua jambo kwa baadhi ya wataalamu waliopo katika majaribio ya usahihishaji mitihani kwa kutumia Mfumo wa Kidijitali ulioandaliwa na Baraza la Mitihani Tanzania.
***********
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda (Mb) leo Aprili 18 2022 amekagua na kuridhishwa na majaribio ya Mfumo wa Kidijitali wa Usahihishaji Mitihani ya Kitaifa ya Ualimu ulioandaliwa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA).
Akizungumza mara baada ya kufanya ukaguzi na kujionea Mfumo huo unavyofanya kazi, Prof. Mkenda amesema kukamilika na kufanya kazi kwa mfumo huo kutasaidia Serikali kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zikitumika wakati wa usahihishaji wa mitihani ya kitaifa.
Waziri huyo amesema ameridhishwa pia kuona mafunzo kwa vitendo ya wasahishaji na wakaguzi wakati wa mchakato nzima wa usahihishaji wa mitihani na wahakiki wa ubora wa usahihishaji wake.
"Nimeambiwa Mfumo huu wa usahishaji mitihani ya Ualimu unatarajiwa kuanza rasmi kutumika mwaka huu kwa kusahihisha mitihani ya ualimu ya vyuo vyote na mwakani utaendelea katika hatua nyingiine ya kusahihisha mitihani ya kidato cha sita na tayari waalimu na wakaguzi wameandaliwa na kupatiwa vifaa husika," amesema Waziri Mkenda.
Mkenda amesema mfumo huo ni wa kwanza katika Afrika na umeandaliwa na vijana wa Kitanzania ambao ni wataalamu kutoka Baraza la Mitihani la Tanzania ambapo amesisitiza kwamba lengo la Serikali ni kuiona NECTA inafanya shughuli zake zote kidijitali ifikapo 2025.
Waziri Mkenda ameongezea kuwa kwa kutumia mfumo huo Serikali itaokoa zaidi ya Shilingi bilioni 37 kila mwaka pamoja na kupunguza mlolongo mkubwa wa usahihishaji wa mitihani.
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dkt. Charles Msonde amesema wametengeneza mfumo huo kwa kuzingatia azma ya Serikali ya Awamu ya Sita na maelekezo ya Waziri ya kuona namna bora ya kuandaa mifumo ya kijiditali ambayo inaweza kutumika katika kusahihisha mitihani pamoja na shughuli nyingine za Taasisi hiyo.
Dkt. Msonde amesema kuwa wataalamu wa TEHAMA wa Baraza hilo walianza kazi ambayo imeleta matokeo ya kuanzishwa kwa mfumo huo ambayo unafanyiwa majaribio ili uweze kutumika kusahihisha mitihani ya Ualimu mwaka huu.
"Kwa Mfumo huu tunaendelea kufikia azma ya Wizara yetu ya kuwa na mifumo ili kuendesha shughuli zote kidigitali na kutimiza lengo la Serikali ya Awamu ya Sita la kuwa na uchumi wa kidigitali na kwetu sisi tumeamua shughuli zote za mitihani kuwa za kidijitali ifikapo mwaka 2025," amefafanua Dkt. Msonde.
0 comments:
Post a Comment