Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Kagera ACP Maketi Msangi
Na Mbuke Shilagi Kagera.
Jeshi la Polisi Mkoani Kagera limekamata maboksi 66 yenye vifaa vya kusafirishia umeme kwenye laini kubwa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 18.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Kagera ACP Maketi Msangi, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake amesema kuwa maboksi hayo yamekamatwa kwa nyakati tofauti wakati wa zoezi la oparesheni iliyofanyika kati ya tarehe 18 hadi 20 mwezi Aprili mwaka huu.
ACP Msangi amesema kuwa maboksi 11 yalikuwa yametelekezwa kwenye shamba la Kahawa katika kijiji cha Kanazi katika halmashauri ya wilaya ya Bukoba, maboksi 37 yalikamatwa katika nyumba ya kulala wageni iliyopo mtaa wa Jamuhuri kata ya Bilele Manispaa ya Bukoba na maboksi mengine 18 yalikuwa yametelekezwa kituo kikuu cha mabasi ya abiria kilichoko katika manispaa hiyo ya Bukoba.
Kaimu kamanda huyo amesema kuwa jeshi la polisi linaendelea na juhudi za kuwasaka watuhumiwa ili kuwafikisha mahakamani.
0 comments:
Post a Comment