Sheikh wa Mkoa Mwanza, Hassan Kabeke ametoa rai kwa wanandoa kuacha kuishi kwa mazoea na badala yake kila siku waifanye ndoa kuwa kitu kipya kinachowapa furaha maishani huku wakilea familia kwa kuzingatia maadili na misingi bora.
Sheikh Kabeke alitoa rai hiyo wakati akitoa nasaha kwenye kongamano la malezi bora, tabia njema na misingi ya ndoa lililofanyika katika Msikiti wa Nyehunge Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema.
Sheikh Kabeke alisema kuna baadhi ya wanandoa wanaume kwa wanawake wanaleta mazoea kwenye ndoa na matokeo yake ni ndoa zao kuvunjika na kusababisha watoto kukosa malezi ya wazazi wa pande zote mbili jambo ambalo ni hatari kwani husababisha watoto kukimbilia mitaani.
"Ndoa haizoeleki, kila siku unatakiwa kuifanya iwe mpya, kuna baadhi ya wanaume na wanawake wanaleta mazoea kwenye ndoa na matokeo yake hazidumu. Tumekuja kupeana elimu hii ili turejeshe misingi ya ndoa kwani yapo mazoea ya kudhani mke au mme ni kiburudisho matokeo yake ndoa zinafungwa mwezi wa Shaaban na kuvunjika baada ya Ramadhan" alitahadharisha Sheikh Kabeke
Wakichangia mada kwenye kongamano hilo baadhi ya washiriki akiwemo Bi. Rehema Fundi na Seif Sungura waliomba BAKWATA kuendelea kutoa elimu ya malezi bora ili kurejesha misingi ya ndoa iliyopotea hatua itakayosaidia kutibu changamoto ya ndoa nyingi kuvunjika mapema.
Kongamano hilo ni mwendelezo wa makongamano ya 'malezi bora, tabia njema na misingi ya ndoa' yaliyoandaliwa na BAKWATA Mkoa Mwanza kwa kushirikiana na Shirika la KIVULINI katika Wilaya za Mkoa Mwanza katika kipindi cha mwezi wa Ramadhan lengo likiwa ni kurejesha maadili katika jamii, kutokomeza ukatili wa kijinsia na kuondoa watoto wa mitaani ambapo maoni yaliyokusanywa kwenye makongamano hayo yatawasilishwa katika Kamati ya MTAKUWWA mkoani Mwanza kwa ajili ya utekelezaji.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Sheikh wa Mkoa Mwanza, Hassan Kaneke akizungumza kwenye kongamano la malezi bora, tabia njema na misingi ya ndoa lililofanyika katika Msikiti wa Masjid Tanbih Nyehunge katika Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema ambapo pamoja na mambo mengine aliwahimiza wanandoa kuishi kwa kuthaminiana lakini pia kuwa na utamaduni wa kupeana zawadi ili kusisimua mahaba miongoni mwao.
Sheikh wa Buchosa, Ahmed Jaha akichangia mada kwenye kongamano hilo ambapo aliwahimiza waumini wa dini ya kiislamu kuzingatia mafundisho ya Mwenyezi Mungu na maelekezo ya Mtume Mohamed hatua itakayosaidia kuishi kwa amani bila mifarakano.
Mmoja wa washiriki wa kongamano hilo, Seif Sungura akichangia mada juu ya nini kifanyike kudumisha misingi ya ndoa ambapo alihimiza elimu zaidi kuendelea kutolewa kwa wanandoa kabla na baada ya kufunga ndoa.
Naye Zawadi Yusuph alisema darasa la ndoa ni muhimu kabla ya vijana kufunga ndoa na hivyo kuomba BAKWATA kuhakikisha hilo lunatekelezeka.
Kwa upande wake Bi. Rehema Fundi aliwahimiza wanawake kuwa watulivu na kuzingatia misingi ya ndoa hatua itakayosaidia kuishi kwa maelewano na waume zao na ndoa zao kudumu.
Katika Kongamano hilo, Sheikh wa Mkoa Mwanza Hassan Kabeke (kushoto) alimtangaza rasmi Omari Bausi kuwa Sheikh wa Kata ya Nyakaliro wilayani Sengerema baada ya aliyekuwa Sheikh wa Kata hiyo ambaye ni baba mzazi wa Sheikh Omari Bausi kufariki dunia. Uamuzi huo ulipitishwa na Halmashauri Kuu ya BAKWATA Mkoa Mwanza.
Picha ya pamoja
Sheikh wa Mkoa Mwanza, Hassan Kabeke na ujumbe alioambatana nao alifika katika malalo ya aliyekuwa Sheikh wa Kata ya Nyakaliro kwa ajili ya kumsomea dua.
0 comments:
Post a Comment