Wednesday 21 July 2021

Waziri Mkuu Atahadharisha kuhusu corona

...


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa rai kwa viongozi wa dini na waumini waendelee kuvumiliana, kustahamiliana na kushikamana katika kufanya ibada na kuienzi tunu ya amani.

“Tuendelee kufanya ibada, kuwaombea wenzetu waliotangulia mbele za haki, tuoneshane upendo na mshikamano hata baada ya kumalizika kwa masiku haya kumi bora ya Dhul Hijja.”

Waziri Mkuu ametoa rai hiyo leo (Jumatano, Julai 21, 2021) katika Baraza la Eid El Adha lililofanyika katika Msikiti wa Mtoro, Ilala jijini Dar es Salaam.

Amesema kila Mtanzania anapaswa kutambua kwamba anao mchango mkubwa katika kutunza na kuimarisha amani ya nchi, hivyo amewasihi wananchi wote waendelee kuitunza tunu hiyo.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakumbusha na kuwasisitiza wananchi wote waendelee kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa wa UVICO-19.

“Tuendeleze tabia ya kunawa mikono mara kwa mara na maji safi yanayotiririka na sabuni na tukikosa maji tutumie vitakasa mikono. Tuvae barakoa zilizothibitishwa na mamlaka zetu.”

Waziri Mkuu amesema ni vema kwa sasa wananchi wakajiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima na wazingatie kukaa umbali wa mita moja au zaidi kutoka mtu mmoja hadi mwingine.

Amesema wananchi wanatakiwa wafanye mazoezi ya mara kwa mara kulingana na afya zao pamoja na mazingira yanayowazunguka, pia amewasihi wazingatie lishe bora.

“Kwa wale wenye umri mkubwa na wenye uzito uliopitiliza na wenye magonjwa sugu kama moyo, pumu, kisukari na figo wanapaswa kuchukua hatua madhubuti zaidi kujikinga na ugonjwa huu.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewasisitiza wananchi wawahi katika vituo vya kutolea huduma za afya mara waonapo dalili za mafua makali, maumivu ya koo, kichwa kuuma, kupumua kwa shida, kukosa hamu ya kula na kupoteza uwezo wa kunusa harufu mbalimbali.”

Akizungumzia kuhusu chanjo ya Ugonjwa huo, Waziri Mkuu amesema chanjo hiyo ipo tayari nchini mwananchi yoyote anayetaka kuchanjwa akachanje kwa ajili ya kupata kinga dhidi ya ugonjwa huo.

Kwa upande wake, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeir Bin Ally amewataka watanzania kuendelea kuimarisha maadili mema yatakayoisaidia nchi yetu “Pia tumuombe Mwenyezi Mungu ili tuondokane na majanga yanayoikabili nchi yetu na ulimwengu mzima”  

Naye, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA), Sheikh Nuhu Jabir Mruma amesema baraza hilo linatoa wito kwa waislamu na Watanzania kwa ujumla waendelee kuienzi na kuilinda amani wanaposherehekea sikukuu ya Eid Al-Adh’haa.

“Tunafanya hivi kwa kutambua kwamba amani ndio msingi wa maisha bora na yenye furaha kwa mwanadamu. Mwenyezi Mungu anatuelekeza juu ya faida ya amani katika kitabu chake kitukufu cha Qur’an sura ya 16 aya ya 112 na nanukuu “Na Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mji uliokuwa na amani na utulivu, riziki yake ikiufikia kwa nafasi kutoka kila mahali.”

Akizungumzia wimbi la tatu la ugonjwa wa UVIKO-19, Sheikh Mruma ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali hususan Wizara ya Afya kwa namna inavyochukua hatua za kukabiliana na kudhibiti janga hilo.

Amesema hatua hizo zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali zimepunguza kwa kiasi kikubwa kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa huo nchini.”Tunawashukuru Watanzania kwa namna wanavyopokea, kutii na kuyafanyia kazi maelekezo ya viongozi katika kujikinga na kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo.

Pia kiongozi huyo amesema baraza hilo linaendelea kuwahimiza Waislamu na wananchi kwa ujumla waendelee kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kukuza uchumi. “Tunaamini kwa kufanya hivyo ndiyo tutakuwa tumeunga mkono kwa dhati juhudi za Serikali yetu katika kufikia malengo yake ambayo ni huduma bora kwa jamii yote.”

 (Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger