Saturday, 31 July 2021

Mhandisi Masauni Aridhishwa Na Utendaji Wa Shirika La Bima La Taifa

...

 Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amelipongeza Shirika la Bima la Taifa (NIC) kwa kuongeza ufani na kuboresha utendaji kazi wa Shirika hilo na kufanikiwa kuongeza kiwango cha uwekezaji kutoka sh. bilioni 85 mwaka 2018/2019 hadi kufikia shilingi bilioni 245 Mwaka 2020/2021.

Mhandisi Masauni ametoa pongezi hizo alipotembelea Makao Makuu ya Shirika la Bima la Taifa Jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya Shirika hilo ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea Taasisi zote zilizochini ya Wizara ya Fedha na Mipango, baada ya kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Wizara hiyo.

“Moja ya eneo lililonivutia ni namna Shirika hili lilivyoboresha huduma zake na  mapato kwa kutumia mifumo ya TEHAMA, kutoka asilimia 10 za miaka ya nyuma hadi kufikia asilimia 95 katika kipindi cha miaka miwili tu iliyopita” Alisema Mhe. Masauni

Ameuagiza uongozi wa Shirika hilo kuongeza ubunifu na bidii zaidi na kuhakikisha kuwa linakuwa Shirika bora zaidi la Bima hapa nchini, Ukanda wa Afrika Mashariki na nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi kutumia huduma za Bima zinazotolewa na Shirka hilo la Umma na kuahidi kuwa Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea kuliunga mkono na kulisaidia liweze kutimiza malengo yake ya kuwahudumia wananchi kikamilifu.

Akitoa taarifa ya utendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Dkt. Elirehema Doriye alisema katika kipindi kifupi cha miaka miwili iliyopita ambacho NIC imefanya mageuzi na mabadiliko makubwa ya uendeshaji wa Shirika, Shirika limewekeza kiasi hicho cha shilingi bilioni 245 sawa na ufanisi wa silimia 136.05.

“Katika kipindi hicho pia Shirika limelipa madai mbalimbali ya Bima ya Maisha yaliyohakikiwa kwa wateja wetu, kiasi cha shilingi bilioni 15.8 kati ya shilingi bilioni 22.53 ambazo shirika  linadaiwa, hatua iliyosababisha kurejea kwa imani ya wateja na kuvutia wateja wapya kujiunga na huduma zinazotolewa na Shirika, na tunatarajia kulipa madeni yote kabla ya mwaka 2021 kuisha” Alisema Dkt. Doriye

Dkt. Doriye alimweleza Mhe. Masauni kwamba Shirika lake pia linazidai Taasisi na Mashirika mbalimbali ya Umma ambazo hazijalipia Bima za Maisha za mali zao kiasi cha shilingi bilioni 34.42 na kwamba fedha hizo zikipatikana zitaongeza mtaji wa Shirika na uwezo wa kuwahudumia wateja wao.

Aidha, alisema kuwa NIC inaandaa bidhaa mpya ikiwemo kuanzisha Bima ya Mifugo na kubuni bidhaa nyingi zaidi za Kilimo ili kuchangia juhudi za Serikali za kuinua sekta za ufugaji, kilimo na viwanda.
Mwish



Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger