Kamanda wa Polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi
***
Mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Neema Bayo anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 40 hadi 49 mwenyeji wa Babati mkoani Arusha, amepoteza maisha na wengine wanne kunusurika kifo, baada ya nyumba ya kulala wageni walimokuwa wamelala kuteketea kwa moto.
Moto huo ulitokea usiku wa kuamkia Julai 29 mwaka huu, katika nyumba ya kulala wageni ya New Anti, eneo la Muleba mjini wilaya ya Muleba mkoani Kagera, umeteketeza jengo lote na vitu vyote vilivyokuwa ndani.
Akizungumzia eneo la tukio Kamanda wa Polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi amesema wakati moto ukitokea katika nyumba hiyo kulikuwa na watu watano wakiwamo wageni watatu, mhudumu na mtoto wa mhudumu huyo.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa Shirika la Umeme nchini TANESCO wilaya ya Muleba, Sadam Kaijage amesema kuwa walipokea taarifa kwa simu na kuwahi eneo la tukio ili kudhibiti moto huo usienee zaidi, na kwamba uchunguzi umeanza ili kubaini chanzo cha moto huo.
Naye mhudumu wa hoteli hiyo iliyoteketea kwa moto Farida Mwise amesema kuwa umeme ulikatika saa nne usiku na wakati wanalala hakukuwa na umeme, na alipoamka usiku kumpa mtoto wake uji kabla hajasinzia alisikia kishindo ndipo alipofuatilia akagundua kuwa nyumba inaungua, akakimbia kuwaamsha wateja na kisha kukimbilia nje akiwa amembeba mwanae.
Chanzo - EATV
0 comments:
Post a Comment