Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, ameeleza kuridhishwa na maboresho ya miundombinu ya usalama na afya katika viwanda vya chuma Mkoani Pwani.
Ametoa kauli hiyo mara baada ya kuhitimisha ziara yake katika viwanda vya nondo vya Fujian Hexiangwang na Lodhia Group of Companies vilivyopo Wilaya ya Mkuranga ambapo pamoja na hatua iliyofikiwa, amevitaka viwanda hivyo kufanya maboresho zaidi.
“Nimefarijika sana kuona yale maboresho ambayo wataalam wetu wa OSHA waliyayatoa ili kuboresha hali ya afya na usalama kwa wafanyakazi yametekelezwa kwa zaidi ya asilimia 70. Hata hivyo, bado kuna mambo ambayo tunawataka waendelee kuyaboresha ikiwemo kuweka mtambo wa kukusanya moshi ili usiharibu mazingira pamoja na afya za wafanyakazi,” alisema Waziri Mhagama na kuongeza:
“Kitu kikubwa kilichonifurahisha katika kiwanda hiki cha Lodhia Group of Companies ni jinsi teknolojia wanayotumia katika uzalishaji inavyosaidia katika kukuza uchumi wa nchi; kiwanda hiki sasa kinazalisha nondo adimu zenye ukubwa wa milimita 40 ambazo zinauzwa hata nje ya nchi yetu. Hata hivyo, tumebaini kuwepo kwa mapungufu kadhaa ya kiusalama na afya ikiwemo kutokuwepo kwa mashine za kubebea vyuma chakavu na kuvipeleka katika majiko ya kuyeyushia vyuma hivyo tumewashauri nao wauweke.”
Katika ziara hiyo Waziri aliambatana na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda ambaye amesema ziara hiyo ililenga kufuatilia utekelezaji wa maagizo mbali mbali ambayo Taasisi yake imekuwa ikiyatoa katika viwanda hivyo.
“Katika usimamizi wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi pamoja na kufanya ukaguzi wa kawaida katika maeneo haya kila mwaka pia huwa tunafanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maelekezo ambayo yanatolewa na wakaguzi wetu. Hivyo, leo pia tumekuja kwa ajili ya kufuatilia maagizo ambayo tuliyatoa hivi karibuni tulipokuwa tunafanya uchunguzi wa ajali zilizokuwa zimetokea katika baadhi ya viwanda vya chuma,” amesema Mtendaji Mkuu wa OSHA.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kiwanda cha Lodhia Group of Companies, Salesh Pandit pamoja na wafanyakazi wa viwanda vilivyotembelewa wamemshukuru Waziri na watendaji wa serikali kwa kufanya ziara na kutoa ushauri juu ya masuala mbali mbali yenye kuleta ustawi katika uwekezaji na haki za wafanyakazi.
“Kiukweli tulikuwa na changamoto nyingi sana za kiusalama na afya lakini niwapongeze OSHA ambao baada ya kufanya ukaguzi walipokuwa wakichunguza ajali iliyotokea hapa walishauri maboresho mengi sana muhimu ikiwemo matumizi ya mashine maalum za kupakia vyuma chakavu katika majiko ya kuyeyushia ambapo hapo awali kazi hiyo hatarishi tulikuwa tukiifanya kwa mikono yetu,” alisema Machaga Silvan ambaye ni Mfanyakazi Kiwanda cha Fujian Hexiangwang.
Mwezi Mei mwaka huu zilirepotiwa ajali kadhaa katika baadhi ya viwanda vya chuma vya Dar es Salaam na Pwani ambazo zilipelekea kufanyika uchunguzi wa kina katika mifumo ya usalama na afya katika viwanda vya chuma. Kutokana na uchunguzi huo, wataalam kutoka OSHA walishauri maboresho mbali mbali katika mchakato mzima wa uzalishaji ikiwemo kutumia mashine maalum kupakia vyuma chakavu kwenye majiko ya kuyeyushia malighafi husika.
0 comments:
Post a Comment