Mahakama ya wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga jana June 30, 2021 imemhukumu kifungo cha maisha jela, Baraka Andrea (25) mkazi wa Kata ya Mhongolo ambaye alikuwa mwalimu wa Tuisheni kwa kosa la kumlawiti mwanafunzi wake wa miaka nane.
Akisoma hukumu hiyo hakimu mkazi wa Mahakama hiyo David Msalilwa amesema kutokana na ushahidi na vielelezo vilivyotolewa mbele ya Mahakama vimethibitisha mtuhumiwa huyo kupatikana na hatia bila kuacha shaka yoyote.
Hakimu Mkazi Msalilwa amesema katika kesi hiyo jumla ya mashahidi watatu walitoa ushahidi ambao ni mama mzazi wa mtoto, Mhanga mwenyewe ambaye ni mtoto na taarifa ya vipimo vya daktari ambavyo mtoto huyo alifanyiwa.
Awali kabla ya hukumu hiyo kutolewa mtuhumiwa Baraka Andrea wakati akijitetea alisema shitaka hilo dhidi yake ni la kutengenezwa kwani yeye kabla ya kutuhumiwa kwa kosa hilo alikuwa anamdai laki mbili mama yake mzazi wa mtoto huyo hivyo hakutenda kosa hilo.
Kwa upande wake wakili wa serikali, Satuninus Kamala aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa huyo ili liwe fundisho kwa watu wengine kwani vitendo vya ulawiti kwa watoto havipaswi kufumbiwa macho kwenye jamii.
Hata hivyo mtuhumiwa huyo Baraka Andrea alitenda kosa hilo tarehe 14 Novemba 2020 baada ya kumaliza kumfundisha mtoto huyo na alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza tarehe 30 Novemba 2020.
CHANZO - HUHESO FM
0 comments:
Post a Comment