Friday, 9 July 2021

Mamlaka Na Taasisi Za Serikali Zatakiwa Kuweka Mikakati Ya Kuongeza Ajira Kwa Vijana

...


Na. Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ametoa wito kwa Taasisi na Mamlaka za Umma kuseka mikakati ya kuwawezesha vijana hususani wanaomaliza Vyuo Vikuu na viwango vingine vya elimu kujiajiri na kujikwamua kiuchumi

Alitoa wito Wito huo  jijini Dar es Salaam alipotembelea Mamlaka ya CMSA ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya Taasisi hiyo katika mwendelezo wa ziara zake za kutembelea taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Mhandisi Masauni alisema kuwa iwapo taasisi na mamlaka za Serikali zitajiwekea programu zitakazo wezesha vijana kujiajiri, kutapanua wigo wa vijana hao kujikwamua kiuchumi na kuwa na mchango katika maendeleo ya nchi.

“Nawapongeza kwa kuwa na Programu ya Tuzo kwa wanavyuo kuhusu masuala ya uwekezaji wa dhamana za Serikali ni jambo zuri kwa kuwa inawawezesha vijana kuanzisha kampuni, kufanyabiashara, usimamiaji, utafutaji wa masoko na kutumia Soko la Hisa kuwekeza kwa kuwa baadhi ya kampuni hizo zinauza hisa jambo ambalo linatakiwa kuigwa”, alieleza Mhandisi Masauni

Alisema kuwa kwa muda mrefu Serikali imekuwa inafanya jitihada ya kuangalia namna gani inaweza kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira hususani kwa vijana wanaotimu Vyuo Vikuu na viwango vingine vya elimu, Mamlaka ya CMSA, imetekeleza kwa vitendo kwa kuwasaidia vijana kuwa na uelewa wa uwekezaji na kuwekeza.

Hatua iliyochukuliwa na CMSA inatekeleza maelekezo mbalimbali yametolewa yakiwemo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, kuhusu dhana ya kuangalia mfumo wa elimu, ili kuwasaidia vijana wanaomaliza Vyuo kutumia elimu waliyoipata kutengeneza fursa za kipato, ajira, uwekezaji na biashara.

Mhandisi Masauni alisema kupitia Programu ya Tuzo, vijana wameweza kushiriki kikamilifu katika kuongeza mnyororo wa thamani katika sekta za maendeleo ikiwemo kilimo kuanzia kuzalisha bidhaa za viwandani kupitia kilimo hadi katika masoko ya ndani na nje.

Vilevile ametoa wito kwa Kampuni na Mashirika ambayo Serikali imewekeza hisa zake kujiorodhesha katika Soko la Hisa ili kuongeza ufanisi wake katika kujiendesha kwa mafanikio, kwa kuwa mashirika mengi yamefanya vizuri na kutoa gawio zuri kwa Serikali baada ya kujisajili katika Soko la Hisa la Dar es salaam ikulinganishwa na kabla ya kuchukua hatua hiyo.

Mhandisi Masauni alisema kuwa kati ya kampuni 10 ambazo ni walipaji kodi wakubwa, kampuni saba zimeorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam, hiyo inamaana kuna umuhimu wa kuendelea kulisimamia soko hilo vizuri ili  kuongeza idadi ya kampuni zikiwemo binafsi.

Pia aliipongeza Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kwa namna ilivyoweza kutumia utaratibu wa uwekezaji katika Hati Fungani kuwezesha kutekeleza miradi nchini ikiwemo ile ya kimkakati kwa fedha za ndani, na kufanya wananchi waweze kushiriki katika maendeleo ya nchi.

Alisema kupitia uwekezaji wa Hati Fungani unamsaidia mwananchi kuwa na utaratibu wa kujiwekea akiba kwa Maisha ya baadae, hivyo elimu katika suala hilo ni muhimu ikatilewa kwa nguvu zaidi ili waweze kutambua fursa hizo hatimaye si tu kusaidia Taifa lao lakini pia kila mmoja katika kujiwezesha kiuchumi.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamalaka ya Masoko ya Mitaji ya Dhamana (CMSA), Bw. Nicodemus Mkama, alisema kuwa suala la elimu kwa umma kuhusu uwekezaji katika Hati Fungani na Hisa limepewa kipaumbele, ili kupitia uwekezaji huo waweze kukuza uchumi wao na kushiriki katika kutekeleza miradi mbalimbali nchini

Alisema kuwa hadi kufikia mwezi Juni 2021, thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji ilikuwa Shilingi trilioni 31.1, ambapo uwekezaji katika hisa za kampuni zilizoorodheshwa katika soko la hisa ulikuwa shilingi trilioni 16.5.

Alisema kuwa uwekezaji katika hati fungani zilizoorodheshwa katika soko la hisa ulikuwa shilingi trilioni 13.9 ambapo shilingi trilioni 13.8 ni hati fungani za Serikali na shilingi bilioni 128.8 ni hati fungani za kampuni.

Aidha mafanikio yaliyopatikana kwa njia ya kuuza hisa kwa umma katika soko la awali na hatimaye kuorodheshwa katika soko la hisa ni kuvuka lengo kwa Kampuni ya Bia Tanzania (Tanzania Breweries Ltd - TBL) kwa kupata shilingi bilioni 297.6 ukilinganisha na lengo la shilingi bilioni 121.5 ambayo ni sawa na mafanikio ya asilimia 245.

Kampuni zingine zilizovuka lengo ni pamoja na Benki ya CRDB, Kampuni ya Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE PLC), Benki ya Biashara ya DCB na pia Benki ya NMB ambayo ilivuka lengo kwa kupata shilingi bilioni 41.4 ukilinganisha na lengo la shilingi bilioni 20 sawa na asilimia 207 kwa kutoa hatifungani ya shilingi bilioni 200.

Alisema kwa ujumla mwenendo wa masoko ya mitaji na dhamana katika kipindi kilichoishia Juni 2021 ulikuwa wa kuridhisha, hivyo ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kuendelea na dhamira yake ya kujenga masoko ya mitaji yaliyo imara yenye kutoa mchango mkubwa katika ujenzi wa uchumi wa nchi.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger