Friday, 19 February 2021

RAIS MAGUFULI : WATANZANIA TUENDELEE KUMUOMBA MUNGU DHIDI YA CORONA..TUSITISHANE... HATUTAWEKA LOCKDOWN

...

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akiwa amekaa kwa majonzi wakati mwili wa Aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Injinia John Kijazi ulipowasili kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 19,2021 ambako ataongoza shughuli za kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Marehemu Mara baada ya kumalizika kwa ibada ya kuaga.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu kuliepusha Taifa la Tanzania dhidi ya Ugonjwa wa Corona na kusisitiza kuwa hatatangaza Lockdown.

Rais Magufuli ameyasema hayo wakati akiongoza waombozaji kuaga mwili wa Aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Injinia John Kijazi kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 19,2021.

"Tusitishane na kuogopeshana Mungu yupo, Mungu ndiyo muweza wa yote, Tuendelee kusimama na Mungu, tulishiinda Corona mwaka jana. Naomba Tusimame na Mungu, ",amesema Rais Magufuli.

"Magojwa yapo na yataendelea kuwepo, magonjwa ya vifua, magonjwa ya kupumua na kadhalika yatakuwepo na hayakuanzia hapa, Zipo Nchi ambazo zimepoteza watu wake wengi. Sisi Tanzania Mungu ametusaidia sana mwaka uliopita, tuendelee kuchukua tahadhari huku tukimuomba Mungu. Mungu Hashindwi",amesema Rais Magufuli.

"Naomba tusitegmee nguvu za ubinadamu, bali tumtegemee Mungu. Narudia ndugu zangu tujue Mungu yupo. Mungu ndiyo muweza wa yote. Nashukuru viongozi wa dini mmeendelea kulihubiri hilo. Tuendelee ndugu zangu kusimama na Mungu. Tulishinda mwaka jana, inawezakana hili ni jaribu jingine, nalo tukisimama na Mungu tutashinda", - Rais Magufuli.

Tusitishane na kuogopeshana, tutashindwa kufika. Inawezekana kuna mahali tumemkosea Mungu. Inawezeakana kuna mahali tunapata jaribu kama wana wa Israel walivyokuwa wanaenda Kaanani. Tusimame na Mungu ndugu zangu Watanzania. Kufa tutakufa tu,unaweza kufa kwa malaria,ukafa kwa Kansa,ukafa kwa magonjwa mengine kwa sababu kufa kupo lakini Kamwe tusimuache Mungu",amesema Rais Magufuli. Huo ndiyo wito wangu"

"Tusimame na Mungu ndugu zetu Waislamu walitangaza muda wao wa kuomba na niliambiwa na Mufti,niwaombe tena Watanzania kama kuna mahali tumetereka tuendelee kumuomba Mungu. Tuanze leo kwa ndugu zetu Waislamu,kesho Jumamosi kwa ndugu zetu Wasabato wanaosali Jumamosi na Jumapili kwa ndugu zetu Wakristo kwa kumuomba kufunga kwa siku tatu. Mimi nina uhakika tutashinda. Nataka niwape nguvu hiyo ndugu zangu Watanzania"


"Naomba  Viongozi wa dini muendelee kusisitiza maombi. Tulishinda mwaka jana, tutashinda mwaka huu, tutashinda miaka yote  kwa sababu kamwe Mungu hajaweza kuliacha taifa hili.Tumeshinda mwaka jana na tukaingia kwenye uchumi wa kati na Corona ipo,uchumi ukaendelea kupanda na Corona ipo,miradi ikaendelea kutekelezwa wala hatukuweka Lockdown hata sasa hatutaweka Lockdown kwa sababu tunajua Mungu yupo siku zote. Taifa hili lipo mikononi mwa Mungu",amesema Rais Magufuli.

“Natoa pole kwa Watanzania wote kwa vifo vyote viwili, cha Maalim Seif pamoja na cha Balozi Kijazi, Jana nilimtuma Makamu wa Rais na Dkt. Bashiru waniwakilishe kwenye mazishi ya Maalim Seif". Kijazi ameondoka hapa duniani kama Shujaa, Maalim Seif kaondoka hapa duniani kama shujaa",amesema Rais Magufuli.

“Balozi Kijazi na Maalim Seif wametangulia zamu yetu sisi bado, Watanzania katika matatizo yoyote yanapotokea yatufanye tuwe wamoja, hofu ni mbaya, ukiona kitu hauwezi kukitatua wewe, mwambie Mungu ndiye muweza, tumekuwa tunatishana sana, tusitishane",- Rais Magufuli

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amesitikitishwa na watu wanaozusha taarifa za uongo kwamba Waziri wa Fedha,  Dk. Philip Mpango amefariki dunia huku akisoma SMS aliyotumiwa na Dk. Mpango kuhusu hali anayoendelea nayo.

"Imefikia mahali sasa tunatishana sana.Leo asubuhi nilitumiwa Meseji na Waziri wa Fedha Dk. Mpango ambaye amelazwa Dodoma na ninaomba niiosome hapa kwa faida ya wale waliokuwa wana Twitt kwamba amekufa",amesema.

Rais Magufuli amesema katika SMS hiyo, Dkt. Mpango amemueleza Rais Magufuli kuwa kwa Neema ya Mungu anaendelea vizuri, anakula vizuri na anaendelea kufanya mazoezi ya kifua na kutembea na kwamba wale waliomzushia mtandaoni kuwa amefariki dunia amewaombea kwa Yesu wakati wa Sala ya Jioni jana.

Share:

Related Posts:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © 2025 MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger