Tuesday, 23 February 2021

Halmashauri Momba Yaikatisha Tamaa NHC Kujenga Nyumba Za Watumishi Songwe

...


Na Munir Shemweta, WANMM SONGWE
Deni la shilingi milioni 384,875,921.01 inalodaiwa Halmashauri ya wilaya ya Momba mkoa wa Songwe na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kuijengea nyumba ishirini za watumishi limelikatisha tamaa shirika hilo kujenga nyumba katika halmashauri za mkoa huo kwa hofu ya kutokulipwa fedha.

Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula tarehe 22 Februari 2021 alipotembelea mkoa wa Songwe kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi katika mko huo.

Mkuu wa mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemus Mwengela wakati wa kikao baina ya Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula na Watendaji wa sekta ya ardhi aliliomba Shirika la Nyumba la Taifa kujenga nyumba katika halmashauri za mkoa wa Songwe na kuziuzia halmashauri  ili kupunguza  uhaba wa nyumba za watumishi.

‘’Ni vizuri sasa Shirika la Nyumba la Taifa likaangalia namna ya kujenga nyumba katika halmashauri za mkoa wa Songwe ili kuopunguza uhaba wa nyumba kwa watumishi’’ alisema Brigedia Jenerali Mwengela.

Meneja Huduma kwa Huduma kwa Jamii wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Muungano Saguya alisema Shirika lake mbali na kufanya kazi ya upangaji miji katika maeneo mbalimbali  limekuwa likijenga nyumba na kuziuzia halmashauri kwa makubalianio ya kulipa kwa awamu  na kutolea mfano wa ujenzi wa nyumba katika halmashauri za Uyui na Busekelo.

Hata hivyo, alisema katika kutekeleza azma Shirika limekumbana na changamoto katika  halmashauri ya wilaya ya Momba mkoa wa Songwe ambapo halmashauri hiyo imeshindwa  kulipa deni lake la Shilingi milioni 384.8 kwa wakati kama ilivyoahidi katika barua yake ya tarehe 5 Novemba 2019 na kulifanya shirika kutafakari namna ya kuendelea na miradi ya aina hiyo katika mkoa wa Songwe.

Akizungumzia suala hilo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula aliitaka halmashauri ya Momba kuhakikisha inalipa deni hilo haraka ili kulifanya shirika kuacha kutumia fedha zake kutekeleza miradi hiyo.

‘’Shirika la Nyumba la Taifa likiendelea kutumia fedha zake kutekeleza miradi litashindwa kutekeleza majukumu yake’’ alisema Naibu Waziri Mabula.

Alisema, kwa sasa Shirika la Nyumba la Taifa linajenga nyumba kulingana na mahitaji ya mteja na lengo kubwa ni kuwawezesha watumishi kuweza kuishi katika nyumba bora na kusisitiza kuwa halmashauri zinatakiwa kuingia mikataba ya ujenzi wa nyumba na NHC  ambapo alisema nyumba hizo ni vitega uchumi vya halmashauri.

Mkuu wa Wilaya ya Momba Juma Irando aliahidi kukaa na Shirika la nyumba la Taifa (NHC) kungalia namna bora ya kuharakisha kulipa deni la halmashauri hiyo ili kuondoa hofu kwa shirika kujenga nyumba za watumishi katika halmashauri za mkoa wa Songwe.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Momba Adrean Jungu aliahidi halmashauri yake kulipa deni hilo haraka katika kipindi cha mwaka huu wa fedha ili kujenga imani kwa Shirika kwa halmashauri nyingine za mkoa huo


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger