Tuesday, 6 October 2020

Watumishi Sekta Ya Maji Watakiwa Kuacha Kuzoea Matatizo Ya Wananchi

...

Na Mohamed Saif, MWANZA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amezitaka Bodi za Wakurugenzi za Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira Nchini kuhakikisha watumishi wanaacha tabia ya kuzoea matatizo ya wananchi na badala yake wayatatue kwa wakati.

Ametoa maelekezo hayo Oktoba 5, 2020 Mkoani Mwanza wakati wa kufungua mafunzo ya Bodi za Wakurugenzi na Menejimenti za Mamlaka 14 za Majisafi na Usafi wa Mazingira kutoka Kanda ya Ziwa.

“Wananchi wakati mwingine wamekuwa na malalamiko mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa huduma ya maji ama kero zingine na wakati huohuo unakuta watumishi wanaopaswa kutatua wamejenga tabia ya kuzoea malalamiko hayo, sasa Bodi mnapaswa kusimamia ili watendaji wasizoee shida za wananchi,” alielekeza Mhandisi Sanga.

Mhandisi Sanga alisisitiza kwamba wajibu wa Bodi za Mamlaka za Maji ni kusimamia shughuli zote za uendeshaji wa Mamlaka kwenye utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

“Natambua Bodi sio watendaji ila wasimamizi, mnapokea taarifa za utendaji  sasa nawasihi msiwe Bodi za kupokea tu taarifa za kila baada ya miezi 3 muende hatua zaidi hasa katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma yenye kiwango,” alisisitiza Katibu Mkuu Sanga.

Alisema lengo la Wizara ya Maji kupitia Mamlaka za Maji kote Nchini ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na toshelevu ya majisafi na salama na kwamba ili kufikia lengo hilo Bodi zinapaswa kuwawajibisha watumishi watakaofanya kazi kinyume na utaratibu.

“Muda mwingine mtumishi anamjibu mwananchi jibu lisiloeleweka na mwananchi hana sehemu nyingine ya kwenda kupeleka malalamiko yake. Mwananchi kama analalamika hapati huduma wakati Bodi ipo, Menejimenti ipo inamaana Bodi haitusaidii. Ninazielekeza Bodi zichukue hatua, mtumishi ambaye hatimizi wajibu wake awajibishwe hata ikibidi kusimamishwa kazi,” alisisitiza Mhandisi Sanga.

Vilevile alizielekeza Bodi kuhakikisha zinajikita kwenye ukaguzi wa mara kwa mara wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao ili kujiridhisha na ujenzi wake badala ya kusubiri taarifa kutoka kwa watendaji hasa ikizingatiwa Serikali inapeleka fedha nyingi kwenye ujenzi wa miradi.

“Zaidi ya asilimia 70 ya matumizi ya Mamlaka za Maji ni ya manunuzi kwa ajili ya miradi ya maendeleo lakini je ni mara ngapi Bodi zinatembelea hii miradi? Ni muhimu Bodi kufika kujionea ujenzi na kukagua thamani halisi ya fedha inayotumika badala ya kuishia kusoma kwenye taarifa za watendaji,” alisisitiza Katibu Mkuu Sanga.

Mhandisi Sanga hakuishia hapo badala yake alizielekeza Mamlaka za Maji zihakikishe zinawasilisha taarifa sahihi kwenye Bodi na lakini pia Bodi nazo kuhakikisha zinakagua vitendea kazi vya kila siku ikiwemo mitambo ya kusukuma maji ili kujiridhisha ufanisi wake kulingana na taarifa zinazotolewa na watendaji.

Aidha, maelekezo mengine ya kiutendaji yaliyotolewa na Katibu Mkuu Sanga ni pamoja na kuhakikisha Mamlaka zinakuwa na mpango wa kupanua utoaji wa huduma katika maeneo yao ya huduma, michango ya fedha kwenye mifuko ya kijamii inawasilishwa kwa wakati, mikakati madhubuti ya kupunguza upotevu wa maji inawekwa.

Vilevile kuhakikisha huduma ya maji na usafi wa mazingira inapatikana kwenye taasisi nyeti kama vituo vya afya, vyuo, magereza pamoja na shule za msingi na sekondari zisizo na huduma hizo.

Alizitaka Bodi kufanyia kazi malakamiko ya watumishi pia, “Bodi inauwezo wa kuajiri na kufukuza sasa ikitokea kuna mtumishi hafanyi vizuri achukuliwe hatua akae pembeni apishe wenye kutaka kufanya kazi,” alielekeza Katibu Mkuu Sanga.

Alisema Bodi zikitimiza wajibu wake inavyopasa, ni dhahiri huduma za maji kote nchini zitaimarika na hivyo kupunguza malalamiko miongoni mwa wananchi na hivyo alizikumbusha katika kutekeleza majukumu yake zihakikishe zinatanguliza maslahi ya wananchi.

Akizungumzia juu ya mafunzo aliyoyafungua, Katibu Mkuu Sanga aliwakumbusha washiriki wote wa mafunzo kuzingatia mada zitakazowasilishwa na wataalam mbalimbali ili kuhakikisha huduma ya maji ina imarika.

“Ni matarajio yangu mtakuwa wasikivu na mtazingatia mafunzo ili hatimaye kwa pamoja mpate dira sahihi ya utekelezaji wa majukumu yenu. Tunasisitiza ushirikiano baina ya Bodi, Menejimenti na watumishi na fanyeni maamuzi yenye maslahi mapana kwa wananchi na sio maslahi binafsi,” alisisitiza Mhandisi Sanga.

Mafunzo hayo ya Siku tatu yanatolewa kwa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira za Maswa, Shinyanga, Bukoba, Mwanza, Kahama, KASHWASA, Musoma, Bunda, Bariadi, Sengerema, Geita, Muleba, Biharamulo na Mugango-Kyabakari. 



Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger