Saturday, 31 October 2020

POLISI WATOA ONYO MAANDAMANO BAADA YA WAPINZANI KUKATAA MATOKEO YA UCHAGUZI MKUU TANZANIA

...

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, CP Liberatus Sabas.
***
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, CP Liberatus Sabas, amesema kuwa jeshi la polisi halitamvumilia mtu yeyote awe kiongozi wa chama au mfuasi, atakayefanya maandamano batili na kama kuna yeyote ambaye hakuridhika na matokeo afuate taratibu za kisheria kudai haki zao kama zipo.

CP Sabas ametoa kauli hiyo hii leo Oktoba 31,2020, na kuwasihi akina mama kuongea na watoto wao kwamba, wasithubutu kushiriki katika maandamano hayo na wasije wakarubuniwa na watu ambao hawana nia nzuri na Taifa.

"Nasisitiza kwamba jeshi la polisi halitakuwa na simile kwa yeyote atakayejihusisha na chokochoko hizi ambazo tunaziona zinaanza kuanzishwa na watu hawa ambao hawalitakii mema Taifa hili, nawaomba akina mama mkanye mwanao kwa sababu mwisho wa siku mtoto atakapopata matatizo atakulilia mama, sasa kabla matatizo hayajamfika nakuomba mkanye mwanao", amesema CP Sabas.

Kauli hiyo ya jeshi la polisi imekuja baada ya Vyama vya ACT Wazalendo na Chadema kutangaza kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu katika ngazi ya udiwani, ubunge, uwakilishi na urais na kutaka urudiwe.

Vyama hivyo vimetoa tamko lao leo Jumamosi Oktoba 31 2020, ikiwa ni muda mfupi tangu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imtangaze John Magufuli wa CCM kuwa mshindi wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano, na siku kadhaa baada ya chombo kama hicho Zanzibar kumtangaza Dk Hussein Mwinyi kuwa rais wa visiwa hivyo.

Pia tamko hilo limekuja baada ya matokeo ya ubunge kuonyesha kuwa kati ya viti 256, ACT Wazalendo imeshinda viti vinne, CUF vitatu na Chadema kimoja.

Via Mwananchi
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger