Monday, 26 October 2020

Mama Samia : CCM imefanya kazi kubwa ya kuleta maendeleo Zanzibar

...


Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema hakuna shaka kazi iliyofanywa na serikali ya CCM itatoa matunda makubwa kutokana na hatua kubwa za maendeleo ziliofanyika kisiwani Pemba, kuanzia ujenzi wa barabara kutoka Kengeja- Hole na ujenzi wa hoteli za kitalii zilizozalisha ajira za kutosha.
Samia ameyasema hayo katika mkutano wa kufunga kampeni za CCM kwa upande wa Pemba, uliofanyika katika uwanja wa Gombani ya Kale, Chake Chake Kusini Pemba.

Alibainisha kuwa, Awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ndani ya miaka 10 ya Rais Dk. Ali Mohameed Shein, imefanyakazi nzuri ikiwemo kuongeza pato la taifa na ukuaji uchumi kwa wastani wa asilimia saba.

Alisema serikali ya Rais Dk. Shein imefanikiwa kupunguza utegemezi wa bajeti kwa kutegemea wahisani kutoka asilimia 30 hadi kufikia asilimia 5.7.

Akizungumzia mapinduzi ya Zanzibar, Samia alisema wananchi wanapaswa kuyalinda mapinduzi hayo na sasa kazi iliyopo ni kuleta mapinduzi ya kiuchumi ndani ya Zanzibar.

“Nataka kusema sisi tuliozaliwa masikini, leo tunaweza kusema mbele ya wananchi. Ungekuwa utawala ule tusingeweza kusimama hapa. Mambo mengi yamefanyika tangu mapinduzi hadi sasa. Tumefungua dira ya mpango wa maendeleo ya Zanzibar, miaka 30 ijayo ambayo kuna mambo yanayopaswa kutekelezwa na kizazi kipya.

“Ndani ya dira hiyo, yapo mambo ambayo Dk. Mwinyi anapaswa kuyetekeleza. Kila watu na zama zao. Dk. Shein anamaliza, mawazo na maono mapya ya Dk. Mwinyi, yataingia kuanza kuleta maendeleo ya Zanzibar yetu,” aliwaeleza wananchi katika mkutano huo.

Alisema CCM ndio chama kilicholeta muungano kupitia CCM na ASP, ambapo umetoa fursa nyingi kwa bara na Zanzibar kunufaika ikiwemo kutumia ardhi na bahari.

Samia alisema muungano umetoa fursa kwa Zanziba kuingia kwenye mabaraza ya kutunga sheria kwa uwiano sawia na sasa umefikia kuwa muungano wa watu kwa kujenga udugu wa damu.

Alisema CCM ndio chama chenye mifumo thabiti ya kuendesha serikali kwa kuwaletea wananchi maendeleo.

Mgombea mwenza huyo wa urais, alibainisha kuwa mgombea urais wa Zanzibar, Dk. Mwinyi amekidhi sifa za kuwa kiongozi wa Zanzibar kwa sababu ni kiongozi mwenye hekima, busara, mtu wa kutulia na kiongozi mwenye kujiheshimu na kuheshimu watu.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger