Monday, 19 October 2020

China: Tuheshimiane, Tuache Kuingilia Masuala Ya Ndani Ya Nchi Nyingine

...


China imetoa wito kwa mataifa mengine duniani kuheshimiana na kuacha kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine kwa kisingizio chochote kile na kueleza kuridhishwa kwake na namna mchakato wa Uchaguzi mkuu unavyoendelea hapa nchini.

Kauli hiyo imetolea na Balozi wa China hapa Nchini Mhe. Wang Ke Jijini Dar es Salaam wakati wa mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge na kuongeza kuwa ni lazima Mataifa yote yaendeleze mahusiano mema miongoni mwao na kutoingilia masuala ya ndani ya Mataifa mengine.  

"Ni vyema Mataifa yote yakaendeleza mahusiano mema miongoni mwao na kuhakikisha kuwa hayaingilii masuala ya ndani kati ya Taifa moja na jingine," Amesema Balozi Wang Ke.  

Aidha Balozi Wang Ke ameongeza kuwa China itaendelea kuheshimu masuala ya ndani ya Mataifa yote Tanzania ikiwemo na kueleza kuridhika kwake na mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu zinavyoendelea nchini na kuwatakia Watanzania kila la heri katika uchaguzi huo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi,Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesema  ushirikiano iliopo baina ya Tanzania na China kisiasa, kiuchumi na kijamii ni madhubuti na imara na kwamba Tanzania itaendelea pia kuheshimu mashirikiano na mataifa mengine.  

Aidha Katibu Mkuu Balozi Brigedia Jenerali Ibuge ameishukuru China kwa Ushirikiano wake wa kimkakati kwa Tanzania na kwamba uhusiano huo utaendelea kudumishwa kwa maslahi ya pande zote mbili.

"Serikali ya Tanzania kwa kweli inaishukuru China kwa Ushirikiano wake wa kimkakati na tunakuahidi kwamba uhusiano wetu utaendelea kudumishwa kwa maslahi mapana ya pande zote mbili," amesema Balozi Ibuge.




Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger