Watanzania wametakiwa kunywa maziwa kwa kuwa ni chakula bora kwa afya ya binadamu na kwamba hitaji la soko la maziwa kadri linavyoongezeka serikali itaweza kufikia azma ya falsafa ya uchumi unaotegemea viwanda.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema hayo mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro akiwa katika mazungumzo na Katibu Tawala wa mkoa huo Dkt. Khatibu Kazungu pamoja na baadhi ya viongozi wa mkoa na mwakilishi kutoka Bodi ya Maziwa nchini (TDB), kuhusu programu ya mradi wa kitaifa wa unywaji maziwa shuleni utakaoadhamishwa kitaifa tarehe 30 Septemba 2020 Mkoani Kilimanjaro.
Prof. Gabriel amesema mradi huo ambao umeingia nchini mwaka 2007 ukijumuisha nchi sabini hadi sasa kwa utaratibu wa Shirika la Chakula Duniani (FAO), umelenga kusaidia kuwapatia watoto afya nzuri wakiwa masomoni, kuwafanya watoto kupenda shule na kujenga hamasa kwa watoto wakiwa wakubwa waweze kushiriki na kujua umuhimu wa kunywa maziwa.
“Wito ni kwamba programu hii inasaidia sana kuwajengea watoto afya nzuri, lakini pia kusaidia watoto wapende kwenda shuleni kwa maana ya uwepo wa maziwa shuleni ni kivutio kimojawapo, lakini pia kujenga hamasa vijana wetu wanapokuwa wakubwa waweze kushiriki na kutambua umuhimu wa kunywa maziwa katika mhimili mzima wa afya zetu.” Amesema Prof. Gabriel.
Aidha, Prof. Gabriel amefafanua kuwa kwa sasa Tanzania inazalisha maziwa lita Bilioni 3.04 kwa mwaka, hivyo miradi ya namna hii ina umuhimu wake hasa kwa ajili ya mipango endeleveu ya maziwa pamoja na uwepo wa ongezeko la viwanda vya kuchakata maziwa nchini na kufikia falsafa ya serikali ya kufikia uchumi unaotokana na viwanda.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Khatibu Kazungu amesema mkoa huo umepata faraja kupewa nafasi ya kuandaa tukio hilo kubwa la kidunia kwa mara ya pili na kwamba mkuu wa mkoa huo anatarajia kuwa mgeni rasmi wakati wa maadhimisho hayo.
Ameongeza kuwa suala la unywaji wa maziwa ni muhimu kwa ajili ya afya ya binadamu na kwamba watoto wengi wamekuwa wakienda shuleni wakiwa hawajapata chakula asubuhi, hivyo uwepo wa maziwa shuleni kutawafanya watoto waweze kuchangamsha akili zao.
Programu ya mradi wa kitaifa wa unywaji wa maziwa shuleni, mwaka huu umebeba kauli mbiu “Glasi Moja ya Maziwa kila siku kwa Afya na Elimu Bora”.
Maadhimisho hayo yamebeba madhumuni ya kuwa na siku moja ambayo fikra za watu wote zitaelekezwa kwenye manufaa ya mpango wa maziwa shuleni na hivyo kuhamasisha kuanzishwa kwa mpango huo.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment