Saturday, 26 September 2020

Taasisi Za Umma Kote Nchini Zatakiwa Kuzingatia Kikamilifu Sheria Ya Serikali Mtandao

...


 Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma
Taasisi za umma nchini zimetakiwa kuzingatia kikamilifu Sheria ya Serikali Mtandao ya mwaka 2019  na Kanuni zake za mwaka 2020 katika kutekeleza jitihada za Serikali Mtandao mahala pa kazi.

Hayo, yameelezwa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini, ACP Ibrahim Mahumi kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt. Laurean Ndumbaro wakati akifungua mafunzo kwa Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini yaliyohusu kujenga uelewa katika utekelezaji wa Sheria ya Serikali Mtandao na Kanuni zake.

 ACP Mahumi ameeleza kuwa, Serikali kupitia Tangazo Na. 964 la tarehe 6/12/2019, ilitangaza kuwa tarehe 15 Disemba 2019 ni siku ya kuanza kutumika rasmi kwa Sheria hii ya Serikali Mtandao na Kanuni zake zilizopitishwa mwanzoni mwa mwaka 2020 ambazo nazo zimeanza kutumika katika kutekeleza sheria hii.

“Tambueni kuwa Sheria hii inaweka msingi wa kisheria wa utekelezaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 na kuanzisha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) yenye jukumu la kusimamia, kuratibu na kuendeleza utekelezaji wa Serikali Mtandao, pamoja na kusimamia uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika taasisi za umma,” ACP Mahumi amesisitiza.

 Aidha, ACP Mahumi amesema kuwa mafunzo haya ni moja ya jitihada za kuongeza uelewa wa mambo ya kuzingatia wakati wa kutumia TEHAMA katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika taasisi za umma na utoaji wa huduma kwa umma, kwa lengo la kuongeza tija na kutoa huduma bora zinazopatikana kwa urahisi. “Nazipongeza taasisi za umma ambazo zimefanikiwa kuboresha utendaji kazi na kutoa huduma zao kwa umma kwa kutumia TEHAMA, ingawa tunaelewa kumekuwa na changamoto katika eneo hili, kama vile uwepo wa mifumo isiyoongea na urudufu.

Hivyo, sheria hii itasaidia kutatua baadhi ya changamoto hizo, ikiwa ni pamoja na kuiwezesha Mamlaka ya Serikali Mtandao kutoa viwango na miongozo ya kitaalamu vya serikali mtandao kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa jitihada mbalimbali za serikali mtandao katika taasisi za umma,” ACP Mahumi ameongeza.

ACP Mahumi ameendelea kusisitiza umuhimu wa kuzingatia vipengele vyote vinavyohusu usalama wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA kama vilivyoainishwa katika Sheria ya Serikali Mtandao na Kanuni zake. Uzingatiaji huo utahakikisha usalama wa taarifa za Serikali zilizomo katika mifumo na miundombinu ya TEHAMA inayotumika katika taasisi za umma.

 Ingawa mafunzo haya yametolewa kwa Wakuu wa Idara/Vitengo vya TEHAMA, ACP Mahumi amewaasa wakuu hao kuhakikisha na wao wanakuwa walimu kwa kusaidia kuwaelewesha watumishi wenzao katika taasisi zao kuifahamu na kuizingatia sheria hii na kanuni zake wakati wa utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Dkt. Jabiri Kuwe Bakari  amezitaka Taasisi za umma  kuzingatia sera, sheria, kanuni, viwango na miongozo ya serikali mtandao wakati wa kusanifu, kujenga na kuendesha mifumo na miundombinu ya TEHAMA kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa umma  huku akizungumzia manufaa ya sheria hiyo .

Aidha, Dkt. Bakari ameeleza kuwa uzingatiaji wa sheria hii na kanuni zake utasaidia kuwezesha matumizi sahihi ya TEHAMA katika taasisi za umma yakayopelekea kuboreka kwa utendaji kazi na kutoa huduma bora zinazopatikana kwa urahisi na haraka, na hivyo kuwa na Serikali ya Kidigitali iliyo imara na endelevu.

 “Napenda kuwafahamisha kuwa sheria hii inaelekeza kuwa taasisi za umma zinazohusika na ujenzi wa miundombinu ya Serikali kama vile barabara, reli na majengo kuhakikisha kuwa yanawekewa mazingira wezeshi kwa ajili ya kupitisha miundombinu ya TEHAMA kuanzia wakati wa kuandaa michoro ya ujenzi wa miundombinu hiyo”.

Pia, Dkt. Bakari amefafanua kuwa taasisi za umma zinatakiwa kuwasilisha mapendekezo na nyaraka zote zinazohusu miradi ya TEHAMA kabla ya kuanza utekelezaji kwa ajili ya kuhakikiwa na kupishwa na Mamlaka, na baadae kuwasilisha taarifa za maendeleo ya utekelezaji, pamoja na taarifa ya mwisho baada ya kukamilika kwa mradi husika.

Aidha, Dkt. Bakari ameongeza kuwa, pamoja na kupitishwa kwa sheria hii, Waziri mwenye dhamana ya kusimamia serikali mtandao ana mamlaka ya kutoa viwango na miongozo kwa ajili ya kusimamia matumizi ya TEHAMA kwenye taasisi za umma, ikiwemo miamala ya kielektroni kwa lengo la kuifanya Serikali kuwa ya Kidigitali zaidi inayo boresha utendaji kazi na utoaji huduma, na kubainisha zaidi kuwa uzingatiaji wake utawezesha kuondoa urudufu na kufanya mifumo ya taasisi za umma kuongea na kubadilidhana taarifa.

 “Hivyo basi kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Serikali Mtandao na Kanuni zake, itasaidia kuwa na matumizi sahihi ya TEHAMA miongoni mwa taasisi za umma, hivyo kuwa na utendaji kazi wenye tija na ufanisi na utoaji wa huduma zinazopatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu” amebainisha.

 Naye mkurugenzi wa TEHAMA Serikalini ,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Priscus Kuwango amesema wao kama wasimamizi wa sheria  watahakikisha wanasimamia kwa weledi  katika kuleta ufanisi wa Matumizi ya TEHAMA Serikalini.

MWISHO.

 


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger