Saturday, 26 September 2020

Mwalimu Mkuu akamatwa kwa kumtaka kingono Mwanafunzi

...


 TAKUKURU Mkoa wa Mbeya, inamshikilia Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyeregete iliyoko Wilayani Mbarali, Adelhard Mjingo, (44), kwa tuhuma za kuomba rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wake wa darasa la saba mwenye umri wa miaka 14 kwa ahadi ya kuwa angemsaidia kufaulu mitihani.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini hapa jana, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya, Julieth Matechi, alisema mwalimu huyo alinaswa na makachero wa taasisi hiyo Septemba 23, mwaka huu akiwa na mwanafunzi huyo kwenye moja ya nyumba za kulala wageni jijini.

Alisema taasisi hiyo ilipata taarifa za siri kutoka kwa mmoja wa wananchi kuwa mwalimu huyo amekuwa akiomba rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wake huyo, akimtishia kuwa endapo angekataa, angehakikisha anamfelisha kwenye mtihani wake wa mwisho.

Matechi alisema kuwa siku ya tukio, mwalimu huyo aliaga shuleni kuwa anakwenda kwenye semina ya chanjo katika Mji wa Rujewa wilayani humo na aliondoka pamoja na walimu wenzake, lakini alipofika kwenye ukumbi wa semina, aliandikisha jina na kuomba udhuru kisha akaondoka.

Alisema Makachero wa TAKUKURU walibaini kuwa wakati mwalimu huyo anaondoka shuleni, alimtaka mwanafunzi wake huyo aondoke shuleni na kwenda nyumbani kubadili nguo, ili asijulikane kuwa ni mwanafunzi na akamtaka avae sweta lenye rangi nyekundu kama ishara ya kutambulika kwa dereva bodaboda aliyekuwa ameandaliwa kwenda kumchukua.


Matechi aliongeza kuwa mwalimu huyo alichukua chumba kwenye nyumba ya kulala wageni (jina tunalihifadhi) iliyoko Rujewa na kisha akamtuma dereva bodaboda kwenda kumchukua binti huyo na alipofika, mwalimu alimpokea na kuingia naye chumbani.

Kiongozi huyo wa TAKUKURU alisema mwalimu huyo baada ya kuingia na mwanafunzi huyo chumbani, alimuuliza kama amekula na alipojibiwa kuwa hajala, alitoka na kwenda kumnunulia chipsi na soda kisha akaingia tena chumbani kwa ajili ya kutimiza azma yake.

Alisema kuwa wakati mwalimu huyo akijiandaa kutekeleza uhalifu huo, makachero wa TAKUKURU waliokuwa wanafuatilia tukio hilo, waliingia na kumweka chini ya ulinzi mwalimu huyo.

"Tunaendelea na uchunguzi wa tuhuma hizi, unaendelea kwa mujibu wa sheria na baada ya kukamilika, hatua zitachukuliwa dhidi ya mwalimu huyo ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani,” alisema Matechi.



Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger