MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kazi ya ujenzi wa daraja la Sibiti imekamilika.
"Nimepita pale darajani leo na kukagua ujenzi, kazi imekamilika yaliyobakia ni matengenezo madogo na kuboresha mapito ya mifugo ambayo yamejengwa chini ya daraja kwa pembeni ili iweze kwenda ng’ambo ya pili kupata maji bila kupita juu ya daraja,” amesema.
Ametoa kauli hiyo jana mchana (Jumatano, Septemba 16, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Mwanhuzi, wilayani Meatu, mkoani Simiyu kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya stendi ya Mwanhuzi.
"Tulipoanza ujenzi wa barabara, tulianza kuunganisha mikoa kwa mikoa na sasa tuko kwenye hatua ya kuunganisha wilaya kwa wilaya kwa kiwango cha lami."
"Hapa Meatu tuna barabara ya kutoka Busega hadi Bariadi kupitia Maswa na Shinyanga ambayo inaunganisha pia mikoa ya Shinyanga na Simiyu lakini pia inaunganisha wilaya za Maswa na Meatu."
"Lakini daraja nililolikagua leo linapitiwa na barabara ya kutoka Bariadi-Meatu-Mkalama (pale Gumanga) na inaenda kuuunganisha na Singida Vijijini pale Iguguno. Barabara hii iko kwenye Ilani ya CCM uk. 75 na inasomeka Bariadi-Kisesa-Mwandoya-Ngoboko-Mwanhuzi-Sibiti-Mkalama-Iguguno."
Amesema barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 289 ambayo itajengwa kwa kiwango cha lami inaunganisha wilaya za Bariadi na Meatu, Meatu na Mkalama, na Mkalama na Singida Vijijini.
"Hili daraja limeisha na kazi iliyobakia ni ya kuweka lami kilometa 17 kutoka darajani kuelekea Mkalama na kilometa nane kutoka darajani kuelekea Meatu."
Amesema maboresho ya miundombinu yanayofanyika nchini kote yanamwezesha Mtanzania achague aina gani ya usafiri atumie pindi akitaka kwenda mahali.
"Maboresho haya yatamsaidia Mtanzania akitaka kusafiri aamue mwenyewe anataka atumie usafiri gani. Reli zimefufuliwa na mpya zinajengwa, meli zinajengwa, ndege zimeshanunuliwa japokuwa wanazisema lakini wanazipanda."
Alitumia fursa hiyo kumwombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Meatu, Bi. Leah Komanya na mgombea udiwani wa kata ya Mwanhuzi, Bw. Igupuli Gambanabi.
Katika hatua nyingine, aliyekuwa mbunge wa Meatu, Bw. Juma Salum amesema anawaunga mkono wagombea waliopitishwa na CCM na wala hajawatuma watu waseme vinginevyo.
"Kuna watu wanapitapita huko na wanatumia jina langu, wanasema nimewatuma. Naomba mnikome sababu situmiki hivyo. Nawaombeni sana wale wafuasi wangu tumuunge mkono Leah Komanya kwani ndiye aliyepitishwa na Chama cha Mapinduzi," alisema.
"Ninaomba kura zetu zote tumpe Dkt. John Pombe Magufuli. Tumwoneshe shukrani zetu kwa mambo mazuri aliyotufanyia wana-Meatu. Leo Waziri Mkuu umepita kwenye daraja ambalo yeye katujengea, tuna kila sababu ya kumshukuru kwa kumpa kura zetu za ndiyo," alisema.
Mheshimiwa Majaliwa anaendelea na ziara yake katika jimbo la Kisesa.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
0 comments:
Post a Comment